Tuesday, May 26, 2015

Mengi Hajaridhishwa na Majibu ya Ikulu Kuhusu Usalama Wake

Mwenyekiti Mtendaji wa IPP, Dk. Reginald Mengi, ameeleza kusikitishwa dhidi ya majibu yaliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais Ikulu kuhusu taarifa za kamchafua zilizochapishwa na gazeti la Taifa Imara Machi 20, mwaka huu.

Dk. Mengi, alisema
jana kuwa majibu yaliyotolewa na Mkurugenzi wa Kurugenzi hiyo, Salva Rweyemamu, siyo ya busara kwani yanapuuza usalama wa maisha yake.

“Majibu haya ya Salva yanaongeza hofu ya usalama wa maisha yangu jambo ambalo siyo dogo na la kupuuzwa kama anavyoona yeye,” alisema Dk. Mengi na kuongeza:

“Ukiangalia, ukisoma kiundani majibu ya barua ya Rweyemamu, nina kila sababu ya kuhofia usalama wa maisha yangu. Shughuli zake Ikulu ni za kuheshimiwa, lakini awe na busara katika shughuli zake….kunishauri eti niende polisi kuhusu suala hilo ni kama kunifanya nionekane sina busara kama yeye.”

Alisema uhai wa mtu siyo jambo dogo wala siyo la kupuuzwa na kwamba busara ilihitajika katika kushughulikia suala hilo, lakini haikuwa hivyo kwani majibu hayo yamesababisha tatizo hilo dhidi ya usalama wa maisha yake kuwa pale pale.

Machi 23, mwaka huu, gazeti la Taifa Imara, lilichapisha habari iliyoeleza kuwa, Kiongozi Mkuu wa ACT Wazalendo, Zitto Kabwe, alimchongea Dk. Mengi kwa Rais Kikwete, kwamba ndiye kinara wa kuihujumu serikali yake na alikuwa anamshawishi Zitto kujiunga na mipango hiyo.

Habari  hiyo iliendelea kudai kuwa, Dk. Mengi aliapa kumshughulikia Rais Kikwete kwa nguvu zake zote amalizapo muda wake wa urais huku Rais Kikwete naye akiapa kupambana na yeye (Dk. Mengi).

Aprili 17 mwaka huu, katika mkutano wake na waandishi wa habari, Dk. Mengi alisema, tuhuma  hizo dhidi yake zilimshtua sana na kumpa hofu kubwa kwa usalama wa maisha yake hivyo kuilaumu kurugenzi ya mawasiliano Ikulu  na Idara ya Habari (Maelezo) kwa kukaa kimya zaidi ya wiki tatu bila kutoa ufafanuzi wowote kuhusu habari hiyo ambayo pia inamhusu Rais na kuiacha kusambaa.

“Nilitoa kauli kwamba, tuhuma hizo dhidi yangu zilinishtua sana na kwamba tamko la Mheshimiwa Rais kwamba atapambana nami lilinipa hofu kubwa kuhusu usalama wa maisha yangu,” alisema Dk. Mengi.

 Dk. Mengi alisema majibu yaliyotolewa na kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais Ikulu, yalieleza kuwa Rais hakuwahi kuwa na mawasiliano na Zitto Kabwe kama ilivyoelezwa na kwamba haikufanya lolote kutokana na kubanwa na majukumu, hivyo kupuuza habari hizo kwa kuziona ni ndogo na za upuuzi.

“Salva hakufanya lolote eti kutokana na kuwa na majukumu mengi na alipuuza habari hizo kwa sababu aliziona ni jambo dogo na upuuzi,” alifafanua Dk. Mengi na kuongeza:

“Bwana Rweyemamu alisema pia kwamba alinishangaa kwa kutokutoa taarifa katika kituo chochote cha Polisi kuhusu hofu ya usalama wa maisha yangu. Majibu haya ya Salva yanaongeza hofu ya usalama wa maisha yangu, jambo ambalo siyo dogo na la kupuuzwa kama anavyoona yeye.”


CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment