CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimejigamba kitatoka katika
vikao vyake muhimu vya Kamati Kuu (CCM) na Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC)
vinavyoanza mjini hapa leo kikiwa imara kuliko hapo awali.
Kauli hiyo imetolewa na Katibu wa Itikadi na Uenezi Chama
cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Nape Nnauye wakati akijibu swali kuhusiana na vikao
vizito vya chama hicho vinavyoanza leo.
Nnauye alikuwa anaelezea maandalizi ya vikao vya kamati
kuu kinachotarajia kuanza leo na halmashauri kuu ambayo itaanza kikao chake cha
siku mbili kesho. Katibu huyo amesema
wajumbe wa vikao hivyo ambavyo vitatoa
mwelekeo wa sura ya uchaguzi itakavyokuwa ndani na nje ya chama hicho
wameshaanza kuwasili mjini hapa.
Ajenda muhimu katika mikutano hiyo ni ratiba ya uchaguzi
pamoja na kuwapata wagombea wa chama hicho ngazi zote. Ajenda nyingine ni hali
ya kisiasa nchini na kutolewa kwa ratiba ya uchaguzi.
Pia vikao hivyo vinatarajia kutoa ratiba ya mchakato wa
uchaguzi wa Urais na wagombea wengine, kutengeneza kanuni za kuwapata wagombea.
Mambo mengine ni kupanga tarehe ya kuchukua fomu, kuzunguka kutafuta wadhamini
na masuala mengine ambayo yanakigusa chama.
Mambo yanayotarajiwa kujadiliwa katika vikao hivyo ni
pamoja na hatma ya makada wanaotaka kuwania kiti cha Urais ambao walitangaza
nia kabla ya wakati na wakatolewa karipio na chama hicho cha kuwataka watulie
na kusubiri muda mwafaka.
Tayari kamati ndogo ya Udhibiti na Nidhamu ya CCM chini
ya Mwenyekiti wake, Philip Mangula ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa CCM
-Taifa, imeshafanya vikao vyake mjini Dodoma kupitia taarifa za utekelezaji wa
adhabu kwa makada sita wa chama hicho wanaodaiwa kuanza kampeni kuwania urais
mwaka 2015 kabla ya wakati.
Makada hao waliozuiwa kujihusisha na kampeni kwa miezi
12, huku mienendo yao ya kisiasa ikifuatiliwa ni January Makamba, Waziri Mkuu
wa zamani, Edward Lowassa na Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye.
Wengine ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Kimataifa, Bernard Membe, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Uhusiano na Uratibu),
Steven Wassira na aliyewahi kuwa Waziri wa Nishati na Madini ambaye ni Mbunge
wa Sengerema, William Ngeleja.
HABARI LEO
No comments:
Post a Comment