Friday, May 22, 2015

UGONJWA WA AJABU MEATU....Dalili zake ni kuumwa kichwa, kikohozi kikavu, mwili kulegea, kuchanganyikiwa akili pamoja na kupoteza fahamu....Sampuli zimepelekwa Nairobi kwa uchunguzi..

IDADI ya wagonjwa ambao wameugua ugonjwa wa ajabu katika kata 6 za wilaya ya Meatu mkoani Simiyu imezidi kuongezeka hadi kufikia 1,048.

Mganga Mkuu wa wilaya ya Meatu,
Dkt. Adamu Jimisha, alisema kwamba awali wagonjwa waliokuwepo ni 80 lakini idadi imeongezeka hadi kufikia 1,048 ambao walifikishwa kituo cha afya Mwandoya.

Dkt. Jimishi alitoa taarifa hiyo jana mbele ya kamati ya ulinzi na usalama ya Mkoa, iliyoongozwa na Mkuu wa Mkoa, Elaston Mbwilo, wakati ilipowatembelea baadhi ya wagonjwa waliolazwa katika kituo hicho cha afya pamoja na kata za Mwabusalu, Lingeka, Mwakisandu, Tindabuligi na Lubiga ambazo zimekumbwa na ugonjwa huo.

Alisema bado hali za baadhi ya wagonjwa zimeendelea kubaki zile zile, ambazo ni kuumwa kichwa, kikohozi kikavu, mwili kulegea, kuchanganyikiwa akili pamoja na kupoteza fahamu.

Aliongeza kuwa wagonjwa hao wanatibiwa na kuruhusiwa kwenda nyumbani pindi wanapopata nafuu au kupona kabisa. Alisema baadhi yao walikutwa na magonjwa mbalimbali kama malaria na minyoo.

Alisema wataalam wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii wakiambatana na timu ya Mkoa akiwemo Mganga Mkuu wa Mkoa, Mtaalam wa Maabara na Daktari mmoja walichukua sampuli kwa ajili ya kupelekwa Nairobi kwa uchunguzi.

Alisema timu hiyo ilipeleka vipimo hivyo Mei 15, mwaka huu kwa ajili ya kubaini aina gani ya ugonjwa, ambapo timu hiyo iliahidi kutoa majibu mwishoni mwa wiki.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa aliwataka wananchi kuwapeleka mapema hospitali watu watakaoonekana na dalili za ugonjwa huo.

MAJIRA

No comments:

Post a Comment