Saturday, May 23, 2015

Waliokacha JKT bila ridhaa ya jeshi upo uwezekano wa kwenda mwezi ujao - HUSSEIN MWINYI

Waziri wa Ujenzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk Hussein Mwinyi
WAZIRI wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk Hussein Mwinyi amesema vijana wote waliohitimu kidato cha sita mwaka 2013/14, 2014/15 na kutojiunga na mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) bila ridhaa ya jeshi hilo, wanaendelea kusakwa na kuorodheshwa kwenye orodha ya watoro na upo uwezekano wa wao kwenda mafunzo hayo mapema mwezi ujao.
Akiwasilisha hotuba ya wizara hiyo bungeni jana ya Makadiro ya Mapato na Matumizi ya fedha kwa mwaka 2015/16, Dk Mwinyi alisema mafunzo ya JKT kwa wahitimu hao hutolewa kwa mujibu wa Sheria, ambapo ni ya kuwajengea uzalendo, ukakamavu, maadili mema, utaifa na kutoa stadi za kazi.

Alisema kwa mwaka 2014/15 jumla ya vijana waliopata mafunzo hayo kwa mujibu wa sheria ni 31,635 ambayo ni sawa na ongezeko la vijana 15,632, ukilinganisha na vijana 16,003 waliohitimu mafunzo hayo mwaka 2013/14 .

“Hata hivyo idadi hiyo ni pungufu ikilinganishwa na idadi ya vijana 41,000 waliohitimu kidato cha sita, waliostahili kujiunga na mafunzo hayo, na sababu zilizofanya upungufu huo ni pamoja na kalenda ya awamu ya pili ya mafunzo kugongana na kalenda ya kuanza mihula ya masomo ya elimu ya juu”, alisema Dk Mwinyi.

Na kuongeza vijana waliopaswa kujiunga na mafunzo hayo ila hawakujiunga bila ridhaa ya jeshi, wameingizwa kwenye orodha ya watoro wa jeshi hilo na kwamba wizara inaangalia uwezekano wa kuiwezesha JKT, kuchukua kundi hilo wakiwemo watoro, kuanza kwa mkupuo mmoja mafunzo hayo Juni hadi Agosti mwaka huu.

“Tunatafuta uwezekano wa kuiwezesha JKT, kuwachukua watoro wa mafunzo hayo na wale walioshindwa kujiunga kwa kugongana kwa mihula ya masomo, kuingia mafunzoni kwa mkupuo mmoja kuanzia mwezi Juni hadi Agosti mwaka huu, ili wawahi muhula wa masomo kwa elimu ya juu”, alisema Dk Mwinyi.

Hivyo aliwataka vijana wote waliohitimu kidato cha sita na kupaswa kujiunga na JKT, na hawakufanya hivyo bila sababu wala kupata ridhaa ya jeshi hilo wafahamu wako kwenye orodha ya watoro wa jeshi hilo na kwamba ni lazima watapaswa kwenda mafunzoni.

HABARI LEO

No comments:

Post a Comment