Thursday, March 20, 2014

my article for newspaper: kaunta za jiko

Mambo ya kuzingatia kabla ya kununua kaunta za jiko

Kaunta za jiko zinahusika mno katika muonekano wa chumba hicho, lakini pia ni kwa umuhimu mkubwa wa kuwa na sehemu ya kufanyia kazi. Kaunta nzuri zinatakiwa ziwe imara, kuweza kuhimili matumizi ya kila siku, kumwagikiwa na vitu na kuhimili mgusano na vyombo vya kupikia vyenye moto kuwekwa juu yake.

Ukiondoa sakafu, kaunta ya jiko ni sehemu inayotumika zaidi ndani ya nyumba. Ni sehemu tunayoandalia chakula, tunayoweka funguo, barua na bili zilizoingia nyumbani na hata wakati mwingine tunaweka hapo magazeti. Hatuwezi kukataa umuhimu wake hasa kwa matumizi. Hata hivyo kwa ajili ni kitovu basi, muonekano wa kishirika na vifaa vingine hapo jikoni kama makabati, jokofu, jiko na sakafu unahusu. Lakini ni kaunta zako za jikoni ndio zinakuwa kipaumbele kwa ajili ni eneo ambalo macho yanaelekea moja kwa moja.

Kabla ya kununua kaunta za jiko hatua ya kwanza ni kufanya utafiti. Kuna aina lukuki sokoni kwa maana ya mitindo na vifaa vilivyotengenezea, kwa hiyo chukua muda wako kuchunguza aina mbalimbali. Kila aina inawakilisha faida na hasara, kwa hivyo sio vyema kukurupuka.
Kama ni swala la umaridadi au uimara, utunzaji au gharama, kila vifaa vilivyotengenezea kaunta vina faida na hasara zake. Nunua kaunta inayokubaliana na mahitaji yako kwa maana ya staili na matumizi. Kujifunza jinsi ya kununua kaunta ya jiko ni mchakato muhimu pale unapojenga au kurekebisha chumba cha jiko. Kaunta sahihi itakubaliana na bajeti yako , mtindo wako wa maisha na muonekano wa mapambo yako ya ndani.
Zifuatazo ni baadhi ya aina za vifaa vinavyotengenezea kaunta za jiko kama zinavyoelezewa na mtaalamu wa maboresho ya nyumbani Bwana Deo Minja. Na anaelezea faida na hasara ya kila aina.

Marble ni jiwe muhimu la asili linalotumika kwa wingi kutengenezea kaunta za jiko. Jiwe hili kiasili lina michoro mbalimbali inayolipa jiko kiwango na hisia za asili. Hata siku moja kaunta ya aina hii haikuangushi jikoni. Utunzaji wake na usafishaji ni rahisi ila unashauriwa kutokata vyakula kwa kisu juu ya marble moja kwa moja kwani inaweza kukwaruzika hivyo kuharibu muonekano. Kaunta hizi ni laini, rahisi kusafishika na haipitishi maji wala joto. Ukitembelea kwenye kila nyumba zenye majiko la kisasa, nyingi zitakuwa na kauta za jiko za aina ya marble.

Jiwe lingine maarufu kwa ajili ya kutengenezea kauta za jiko ni granite. Jiwe hili linafanya jiko lionekane la kifahari na huwa linakuja kwa rangi zaidi ya 3000, anasema Minja. Linadumu maisha ni ni la pili kwa ugumu baada ya almasi. Changamoto yake kubwa ni kuwa ni gharama kubwa

Kaunta za jiko za marumaru ni imara na rahisi kusafishika. Marumaru kwa kawaida inaongeza uhai wa mahali. Pia sio gharama na kuna aina na rangi mbalimbali kwa nyumba za kawaida. Changamoto yake ni kuwa kwa vile zile marumaru ni kipande vidogodogo vinavyounganishwa pamoja, basi wakati mwingine kaunta inakosa levo na pia ni rahisi kuwa na mipasuko na ile grout inayowekwa katikati ya mistari huwa inashika uchafu kirahisi mno

Kaunta nyingine za jiko ni zile za kujaladia kwa mfano formica. Ziumetengenezwa kwa vifaa vya plastiki vyenye sehemu ya juu  laini ambayo inakuwa rahsi kusafisha. Faida yake ni kwamba ni bei rahisi na zipo za rangi mbalimbali. Hasara yake ni kuwa mikwaruzo na mipasuko hairekebishiki.

Kaunta za mbao zinaleta muonekano mzuri na zipo za mitindo na rangi mabalimbali. Mbao ngumu kama vile mkongo na mninga ndio zinazotumiaka zaidi kwa ajili ya kaunta. Ni rahisi kusafisha na changamoto yake ni kuwa zinahitajika kufanyiwa maboresho ya mara kwa mara. Ubaya wa kaunta za mbao ni kuwa zinaharibiwa na maji na baada ya muda zinashika madoa.

Kaunta za chuma kisichoshika kutu kwa jiko lako nacho ni chaguo zuri. Zinahimili joto na ni imara. Na kwa sababu zinajengewa kwa matakwa yako inawezekana pasionekane viungio vyovyote kwenye kaunta yako. Zinafaa kuwekea sufuria za moto na ni rahisi kusafishika. Changamoto yake ni kuwa zina kelele, zinaweza kubonyea na huwezi kukatia juu yake.

Kama una  chumba cha jiko chenye umbo lisilo la kawaida hasa kona, zege inaweza kuwa chaguo zuri kwa ajili ya kaunta za jiko lako. Faida zake ni kwamba zinahimili joto na mikwaruzo. Na hazihitaji utunzaji kivile, zinaweza kuwekwa rangi na urembo wa aina mbalimbali ila changamoto yake ni kuwa  kama tunavyojua zege ni saruji kwa hivyo nyufa zinaweza kutokea na ule muonekano wa zege chumba kinaonekana kama cha kiwandani zaidi.

Baada ya kujua aina zote hizi za vifaa vya kutengenezea kaunta za jiko kama tulivyoelezwa na Bwana Minja kifuatacho ni kuangalia bajeti yako. Bajeti ndio kikwazo namba moja kwenye kuchagua kaunta za jiko. Kwa mfano kaunta za granite na marble zinaweza kuwa gharama mara 3 zaidi ya zile za kujaladia.

Jambo la pili la kuzingatia kabla ya kunua vifaa vyako vya kujengea kaunta za jiko ni umaridadi. Kaunta zote zinatakiwa zitimize lengo la msingi ambalo ni kuweza kuwa na eneo la kufanyia kazi wakati wa kuandaa chakula, hata hivyo kuna upande wa umaridadi. Kama huna uhakika wa muonekano wa kaunta unayotaka basi angalia maeneo mengine ya jiko kama vile makabati ili kuweza kuleta uwiano na kaunta.

Jambo la tatu na kubwa kuliko ni kuamua sasa kununua kifaa cha aina hii ili kutengenezea kaunta za jiko lako. Gharama, uimara na muonekano unatofautiana kwa kila aina ya vifaa vya kutengnezea kaunta.

Haijalishi ni aina gani ya kaunta ya jiko utakayoamua kuweka nyumbani kwako, mara zote hakikisha kuwa unapitia kwa mtaalam. Inatatiza, inakula muda, na kama nia yako kuu ni kufanya eneo hili lionekane maridadi wakati huo huo likitumika, unataka kuwa na uhakika wa usimikaji sahihi.

Makala hii imeandaliwa na Vivi O. Machange.  Vivi ni mjasiriamali  upande wa usafi wa nguo, mazulia na magari; pia ana mapenzi makubwa juu ya muonekano wa nyumba. Kwa maoni au maswali tuma kwenda 0755 200023 au viviobed@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment