WATU watano wamevamia na kuvunja madirisha ya Kanisa
Katoliki la Mtakatifu Joseph, Parokia ya Malolo na kuiba chombo kinachotumika
kuhifadhia ekaristi takatifu (TABERNACULO).
Imeelezwa kuwa majambazi hayo yalidhani chombo hicho kimetengenezwa
kwa dhahabu.
Tukio hilo lilitokea juzi, saa 8:30 usiku, baada ya
majambazi hayo kuvunja madirisha ya kanisa hilo.
Kanisa hilo ni miongoni mwa makanisa makongwe na yenye
historia kubwa hapa nchini, ambalo lilijengwa mwaka 1939.
Paroko wa kanisa hilo, Theophan Membe, alisema siku ya
tukio alikuwa Lindi kuhudhuria misa takatifu ya mapadre wa jimbo la Lindi,
iliyoongozwa na Askofu wa jimbo hilo Mhashamu Bruno Ngonyani.
Alisema baada ya tukio hilo alitoa taarifa kwa Mwenyekiti
wa Kigango cha Malolo, Cleophas Nnonjela, na badaye walitoa taarifa polisi.
Membe alisema parokia ya Malolo ni miongoni mwa parokia
zilizotoa wasomi wengi mkoani Lindi kutokana na historia yake.
Membe alisema baada ya wahusika kukiri kama wameiba,
askofu wa jimbo anaondoa dhambi ya mauti kutoka kwa waumini kwenda kwa wezi
hao.
Alisema kutokana na kuibiwa kifaa hicho, waumini wa
kigango hicho watakosa baadhi ya huduma ikiwemo ibada ya Jumapili, misa ya kila
siku asubuhi, misa ya katekista na upigwaji wa kengele zinazoashiria saa kwa
waumini.
Alisema katika kipindi hicho huduma za ubatizo,
kipaimara, komunio takatifu, kitubio, misa za mazishi, mpako kwa wagonjwa,
sherehe za ndoa na masuala yote ya msingi yanayohusu Kanisa Katoliki
hayatakuwepo.
UHURU ONLINE
No comments:
Post a Comment