Jinsi ya kufanana na mazingira ya nyumbani kwako
Kila mtu anachagua ni vipi anataka
mazingira ya nyumbani kwake yawe. Ingawa tunaweza tusijali kuhusu uchaguzi huo
lakini mazingira yetu ni dili kubwa kutuhusu. Una nafasi ya kutengeneza mazingira
ambayo yatarahisisha maisha yako ama yatayafanya yazidi kuwa magumu.
Kuna kanuni ya kwanza ya msingi kuwa
katika kila kitu kilichopo kwenye eneo linalokuzunguka kina nguvu fulani iwe
kitu hicho kina uhai ama hakina. Ni kama watu wa kale walivyoamini kuwa kila kitu
kina uhai. Kanuni ya pili ni kuwa kila kitu kwenye mazingira yetu kinahusiana
na kitu kingine. Inawezekana kwa mtizamo wa kiroho au wa kisayansi. Na kanuni
ya tatu ni kuwa kila kitu kinabadilika kila wakati.
Sasa basi kama kila kitu kwenye
mazingira yako kina uhai na kimeunganishwa na wewe basi mabadiliko yakitokea
kwenye eneo lako nawe unaguswa. Mazingira yako yanakugusa nawe unayaakisi. Hii
ni kama usemi kuwa kila kitu kwenye mazingira yako kinaongea na wewe. Je vitu
vya mazingira yako vinasema yale ambayo unapenda kusikia, je vinakusaidia
kupata kile unachotaka kupata katika maisha.
Fikiria jinsi unavyoingia nyumbani
kwako na kukumbuka usemi kuwa unachokutana nacho mwanzo kinakugusa zaidi . Kama
unaingilia varanda iliyojaa makorokoro kila mara unapoingia nyumbani kuna
uwezekano mkubwa wa kuchoka hapo hapo nje hata kabla hujafika ndani. Vilevile kama
unatembea kuelekea karibia na kizuizi unaanza kujifikiria kuwa inahitaji nguvu
kupita pale. Pia kama unafungua mlango wa ofisi asubuhi na kukutana na meza
iliyojaa nyaraka, unaweza kujisikia kama siku yako tayari imejaa na hakuna
nafasi ya kuanza kitu kipya kwa siku hiyo.
Tembelea kila chumba nyumbani kwako.
Je kuna kitu kinakuambia kuwa maisha ni mazuri na yamejaa fursa? Au una picha
usiyoipenda, fenicha ambayo haijakaa sawa au rangi ya ukuta ambayo inakupa
ukakasi kuitazama? Kila mara unapooana vitu kama hivi, unapotembelea chumba
hiki unapata ujumbe hasi. Hata kama akili yako itazoea kuona hivyo lakini
dhamira itakuwa inakereka.
Mkusanyiko wa picha unaweza kuwa
chanzo cha ujumbe hasi. Hakikisha ni za kumbukumbu na hisia nzuri za watu hao
kwako. Zinaweza kuwa ni picha nzuri sana kwa kuonekana kwa macho lakini kama
mojawapo inakukumbusha tukio au wakati wa huzuni basi iondoe. Weka zile zinazokufanya uwe na tabasamu. Watu
mara nyingi wana picha kwenye kuta zao kwa sababu tu hawana kitu kingine cha
kuweka hapo na sio kwamba ni kwa kuwa wanakipenda kilichopo. Sanaa ukutani
inaweza kuwa nzuri sana ila kama ukiitazama haikubariki haina faida kwako.
Badala yake inakupa ujumbe hasi na kukunyonya nguvu kila unapoiona. Ni vyema
kuiondoa na kuacha nafasi kwa kitu ambacho kinakupa mtizamo chanya katika
maisha.
Kuchukua hatua hii mbele zaidi,
fikiria ni nini unakipenda kwenye maisha. Mfano mzuri ni mtu anayetaka kuwa na
uhusiano. Mara nyingi picha atakazoweka nyumbani kwake na hasa chumba cha
kulala ni za akiwa singo. Chumba hicho kitakuwa na taa moja tu ya kivuli na
hata kimeza cha kando kimoja. Vyote hivi vinatoa ujumbe kuwa mhusika hana mtu.
Badala ya vitu vilivyopo kwenye seti kwa mfano picha yenye watu wawili, na taa
mbili za vivuli vinaleta alama za mahusiano.
Mazingira ya mahali unapoishi
yanahusika katika kila eneo la maisha yako. Kama unahitaji akili tulivu
hakikisha kuwa mazingira yako hayakupi kinyume na matakwa yako kwa kuwa na vitu
ambavyo haviko mahali pake. Pia kama unataka kuwa mbunifu zaidi angalia kama je
kuna nafasi zaidi ya kuweza kuwa hivyo? Kama unahitaji miundo mbinu safi je
njia ya kuendea mlangoni kwako ni wazi, safi na inakaribisha?
Unavyotembea kwenye mazingira ya
nyumbani kwako angalia kila kitu kwa jicho la ziada. Ondoa kila kitu ambacho
huwezi ukasimama na kushuhudia kuwa unakipenda na ni kitu ungependa kuwa nacho.
Unaweza usiwe na kiti kingine cha kuweka kwenye hiyo sehemu ulipotoa kile usichokipenda,
lakini kama kinakuletea tukio la huzuni bado, potelea mbali kitoe tu. Kinaziba kile
unachokipenda na pia hicho usichokipenda kinakuletea hisia mbaya. Kwa kuamini
utapata kingine unatengeneza uwezekano. Kuwa makini na hivyo vitu vinavyoongea na
wewe furaha na kuvipa nafasi ya heshima nyumbani kwako.
Katika nyakati hizi za mihangaiko
mingi, ni muhimu kuwa mazingira yako hayakuongezei vikwazo kwenye dunia yako.
Hii inahusu hata taarifa za habari kwenye matukio ya mauaji, ajali na mengi ya
kutisha. Fuatilia ni nini kiko kwenye vyumba vya watoto. Kama mazingira ya
vyumba vyao yanaongea amani, watakua wakiwa wanajifunza amani.
Kwa kuwa makini na kila kitu kwenye
mazingira yako unatengeneza makazi ambayo yanafanana na wewe kwa kukupa ujumbe
chanya na zenye kukutia nguvu. Kuwa kitu kimoja na makazi yako unakuwa na
mtizamo chanya zaidi katika maisha. Mtazamo chaya unagusa kila kitu kwenye
maisha yako. Yasikilize mazingitra yako.
Makala hii imeandaliwa na Vivi Machange ambaye
ana mapenzi makubwa juu ya muonekano wa makazi. Kwa maoni au maswali tuma
kwenda 0755 200023 au viviobed@yahoo.co.uk