Kama
una chumba rasmi cha kulia chakula na kina nafasi ya kutosha, uwezekano ni kuwa
tayari una kabati la vyombo kama sehemu ya muonekano mzima wa chumba hicho,
kwani kwa asili kabati la vyombo linawekwa kwenye chumba cha kula chakula.
Ingawaje kabati hili linakusaidia kuhifadhi vyombo vyako vya thamani kwa pia ni
pambo kwenye chumba cha chakula.
Kwa
ajili kabati la vyombo ni zito na ni fenicha kubwa, watu wengi hawapendi
kulisogeza mara kwa mara, hata kama wana uwezo wa kufanya hivyo. Pia kwa
nyongeza mara nyingi ni kuwa kabati la vyombo linafiti eneo moja tu la chumba
cha chakula. Familia ambazo zina watoto wadogo nyumbani zinatakiwa kuwa makini
kwani watoto wanaweza kupamba juu au kuliangusha na likasababisha ajali kama
ambavyo tulishawahi kusikia wakati fulani kwenye maisha yetu ajali ya mtoto kuangukiwa
na kabati la vyombo.
Makabati
ya vyombo yako ya mitindo miwili; yale ya milango mpaka chini na yale ya milango
nusu na eneo la chini droo. Kwa hiyo ni uamuzi wako kuamua ni la mtindo upi
unataka. Pia kama una chumba cha chakula kikubwa, kabati kubwa la vyombo ni
bora zaidi ili kuleta uwiano wa chumba. Na kama una eneo dogo la chumba cha
chakula kabati dogo la vyombo ndio linafaa zaidi. Na kiukweli wengi wenye vyumba
vidogo vya chakula wanapenda kubuni kabati la vyombo ambalo linafiti kwenye kona
ya chumba, ili kutumia nafasi ambayo vinginevyo ingekaa bure, anasema mbunifu
wa ndani dada Agripina.
Ni
vizuri rangi ya kabati la vyombo ifanane na ya fenicha nyingine za chumba cha
kulia chakula. Wengi wanapenda kabati la vyombo libaki na ile rangi asili ya
mbao badala ya kuongezea rangi nyingine. Na endapo watapenda kuongeza rangi
basi chaguo namba moja ni rangi nyeusi, anasema fundi seremala anayetengeneza
makabati ya vyombo, ndugu Mmasi.
Kabati
la vyombo lengo lake namba moja ni kuhifadhi vyombo vyako vya thamani kwa namna
ambayo italeta mvuto, na ndio maana mbele huwa ni la kioo. Kanuni hapa ni
kuleta uwiano wa kuhifadhi vyombo mbalimbali na kuvutia. Kuwezesha hili
unatakiwa kugawanya vyombo vyako kwenye makundi kuendana na muonekano, na kuamua
ni vipi uweke kwenye eneo la maonyesho ambalo ni eneo la vioo. Kwa mfano, kundi
la sahani, kundi la vikombe, kundi la mabakuli, kundi la majagi, kundi la
visosi, kundi la glasi, kundi la matrei na kundi la sahani mojamoja za kupambia.
Hala
tafuta uwiano wa vyombo hivi kwenye kabati, kama umeweka sahani ya kupambia
upande mmoja hakikisha kuwa unaweka na wa pili.
Ingawa
kabati la vyombo ni kwa ajili ya vyombo bado linaweza kupambwa kwa kutumia
hivyohivyo vyombo vyako hasa kwenye zile sehemu zinazoonekana, kwani kama
tujuavyo makabati ya vyombo ya kuvutia yana milango ya vioo. Kwa hivyo kabati
hili unawekea vyombo vyako na vilevile mapambo ya ladha yako.
Kupamba
kabati la vyombo kwa njia ya kuvutia ni kuwa na vyombo vyote vinavyoonekana
viwe kwenye rangi za kufanana. Kwa mfano kama kabati lako lina vyombo vya
mapambo vya rangi za bluu na nyeupe, fikiria kuendelea kuongeza vyombo vya
michoro yenye rangi hizohizo kama vile glass, vyungu au vesi, majagi, sahani na
vikombe vya bluu. Ukichanganya vyombo vya rangi mbalimbali kabati halileti muonekano
wa kuvutia, anasema Agripina.
Hakikisha
kuna uwiano wa rangi kwenye kabati zima. Kama kabati lako ni kubwa na lina
sehemu ya vioo ya kutosha unaweza kuamua kupambia kwa kuongeza vitu vya msimu
uliopo. Njia moja ya kufanya hivi ni kutenga shelfu au juu ya kabati kuweka
vitu hivi vya msimu na sehemu nyingine yote ya kabati iliyobakia kubaki katika
mpangilio wa awali. Hivi vitu vya msimu vinaweza kuwa ni kwa mtindo wa mabakuli
makubwa, matrei au vesi.
Kabati
la vyombo si tu kwa ajili ya vyombo, unaweza kuweka humo vitu vyako vya kuvutia
ambavyo ungependa kuvihifadhi lakini sio kwenye kificho. Vitu hivi ni kama vile
vitambaa vya meza, album za picha vitu vilivyofumwa kwa jinsi ya kuvutia
machoni na kadhalika.
Vtu
vya silva kwa maana ya vijiko, visu, uma na vinginevyo viwekwe kwenye droo za
kabati lako la vyombo.
Kabati
la vyombo liliopangwa na kupambwa vizuri ni ongezeko muhimu katika chumba cha
kulia chakula, fanya kabati hili liwe kitovu cha chumba hiki.
Makala
hii imeandaliwa na Vivi, kwa maoni tembelea www.vivimachange.blogspot.com
No comments:
Post a Comment