Thursday, May 8, 2014

my article for newspaper: mpangilio wa chumba cha kulala cha wakuu wa familia

Huenda wewe na mwenza wako mnaishi maisha yenye kazi nyingi (busy) ambayo mara nyingi yanapingana na kuwa na muda mzuri wa kukaa pamoja. Hakika mnajua hisia zenu zinavyokuwa kwa ajili ya kukosa muda huo muhimu. Ndio maana ni vyema kuwa na chumba cha kulala ambacho mkiwa pamoja kama wanandoa itawezekana kufurahia ule muda mchache mnaokuwa pamoja. Kwa lengo la makala hii chumba cha wakuu wa familia ni kile cha  baba na mama wa familia – ni koloni lao hapo nyumbani kama wengine wanavyoweza kusema. Wazazi mkiwa ndio nguzo ya familia basi mnahitaji chumba cha kipekee. Mnaokaa kwenye chumba hiki ndio mnaolipa bili na kufanya kazi kwa bidii ili mfanikiwe katika hilo. Kwa nini chumba chenu kisiwe maalumu? Wakuu wa familia mnastahili chumba hiki!

Je wewe mkuu wa familia unakipenda chumba chako cha kulala? Chumba hiki kiwe kama mahali patakatifu kwa wanandoa au yeyote anayelala mule. Chumba kiheshimiwe kisiwe ni ofisi ya nyumbani. Chumba cha kulala cha wakuu wa familia ni sehemu ya kupumzika hivyo vitu kama kompyuta havina nafasi kwenye chumba hiki. Ni nini cha kwanza unachokiona mara baada ya kufungua mlango wa chumba hiki, na ni nini unachokiona cha kwanza mara baada ya kufungua macho asubuhi. Chumba hiki kiwe ni sehemu huru pasipo na usumbufu kama wa kufua, ndoo za maji, kompyuta au midoli ya watoto. Chumba hiki sio stoo!                          

Midoli imekuwa ni tatizo kwenye chumba cha kulala hasa kwa wazazi wanaokimbia mchakamchaka wa maisha ya kila siku. Midoli inaishia chumba cha wazazi na hata kitandani.  Kuwa wazi  na kuweka mipaka juu ya chumba hiki na hata midoli ya watoto isijazane chumbani kwako na kitandani. Kwa ujumla watoto wawe na sehemu ya kucheza na kuweka midoli yao. Chumba cha kulala cha wakuu wa familia ni cha watu wazima ndani ya familia.

Fenicha kuu kwenye chumba hiki ni kitanda. Kimsingi, kitanda kina lengo moja kuu: kufagilia usingizi wenye afya. Chumba cha kulala cha wakuu wa familia kinahitaji kitanda chenye kukidhi vigezo vya usingizi bora. Kama matangazo tuseme ya magodoro yanavyoonyesha ni kuwa tunatumia theluthi moja ya maisha yetu kulala. Sasa kwa nini godoro, malazi na fremu ya kitanda visiwe maalumu. Kuna njia nyingi ya kupata kitanda bora kwa bajeti yeyote. Kitanda chenye fremu ya chuma tuu kilichosogezwa karibia na ukuta hakikidhi vigezo. Kila kitanda kinahitaji bodi la kichwani (makala zijazo tutaongelea umuhimu wa bodi hili) ambayo yanapatikana kwa saizi na mitindo mbalimbali.

Kwa kuwa msisitizo wa chumba hiki ni kwa wanandoa,  kama kuna sehemu kubwa weka sofa au viti viwili vya kukalia badala ya kimoja. Mara zote fikiria vitu viwili viwili. Kama wewe ni mwanaume au mwanamke uliye singo lakini ndio mkuu wa familia weka picha ya peke yako kusisitiza utambulisho wako kuwa huna mtu. Kama mnaolala humo mko kwenye mahusiano basi mambo ni kwa seti kama vile taa za vivuli mbili, vimeza vya kando viwili na hata kama mishumaa basi miwili.  Kumbuka unatengeneza mandhari ya kupumzika na kuondoa msongo wa mawazo wa siku nzima. 

Chagua sanaa inayoelezea uhusiano wenu iwe ni picha ya ngalawa, ndege au hata maneno ya kimahaba. Sio sawa kuweka picha za marafiki, mababu na hata wanafamilia wengine kwenye chumba hiki. Tatizo ni kuwa chumba kinaanza kuonekana kinguvu kimezidiwa na vitu. Watu wote hawa wana haja gani chumbani kwako. Pambeni chumba cha kulala kwa picha zenu nyie wanandoa mnaolala humo.
Chumba hiki kamwe kisiwe na mrundikano, weka kero za maisha ya kila siku mbali na mahali hapa patakatifu. Kama kabati lako la nguo limefurika, punguza ubakize zile ambazo haswa unazivaa. Pia fikiria kupunguza kiasi cha fenicha ili kuwe na nafasi chumba kisionekane kusongamana. Sakafu ionekane peupe isijazane vitu.  

Zingatia kile unachokiona kwanza mara baada ya kuingia chumba chako cha kulala. Kanuni inasema kuwa mlango usiwe usawa mmoja na kitanda, kwa maana ya kuwa ukiwa umelala kitandani uuone mkango lakini ukifungua mlango macho yasione kitanda moja kwa moja. Mlango ukiwa namna hii unawapa walalaji kujiamini zaidi kuwa wanamiliki chumba na usingizi unakuwa mwororo.
Vifaa vya umeme leo hii ni changamoto kwenye chumba cha kulala. Kompyuta, luninga na vifaa vingine vya umeme vinatuzunguka na kutunyonya nguvu kwa  kuleta nguvu ya uvutano mithili ya sumaku ambayo baadaye inaleta msongo wa mawazo. Ili kupumzisha mwili na kuuweka katika afya njema basi ni vyema kuwa mbali na vifaa vya umeme katika chumba cha kulala. Kama hamna jinsi kuwa ni lazima vifaa hivi viwepo chumbani basi sio tu vizime na kuacha vijitaa vinawaka bali chomoa kabisa kwenye umeme wakati wa kulala.

Kumbuka kuwa kila kitu kwenye nyumba tunazoishi kinatupa ujumbe. Chumba chako cha kulala wewe mkuu wa familia kinakupa ujumbe gani? Je kinakukumbusha majukumu yote unayohitajika kukamilisha au kinakupa hisia za utulivu na kukukaribisha kupumzika? Je kinakushawishi kuwasha luninga au kinakuleta kwenye faragha? Je kinaongeza msongo wa mawazo kwenye maisha yako? Au kinakupa pumziko la nafsi hata kama uko singo? Kama ndio basi umeweka mpangilio wa chumba cha kulala ambacho ni kama mahali patakatifu.

Makala hii imeandaliwa na Vivi Machange ambaye ana mapenzi makubwa juu ya muonekano wa makazi. Kwa maoni au maswali tuma kwenda 0755 200023 au viviobed@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment