Tuesday, October 11, 2016

Namna ya kuleta ushirika wa rangi za pazia na za viti/sofa

 
Aidha unapamba upya au ni bahati kwamba ndio umekamisha ujenzi wa nyumba yako, bila shaka ni wakati wa kufikiria rangi za vitu ambavyo utahitaji kwenye kila chumba. Vyumba vikubwa kama vile sebule na chumba cha kulala cha wakuu wa familia ni
kati ya ambavyo vinatakiwa kuwa na ushirikiano kati ya rangi za pazia na viti.

Kuchagua rangi ambazo zitashirikiana kati ya vitu hivi viwili ni muhimu ili kuleta muonekano wa kuvutia na sio tu shangalabaghala kama upinde wa mvua.
Unapochagua rangi na michoro ya kitambaa cha pazia ni vyema kushirikisha pia rangi na machoro iliyopo kwenye viti na sofa unapotaka kuweka pazia hizo.

Kwa kawaida pazia zinatakiwa kuwa nzito na zisizoangaza, unataka kulala katika chumba ambacho seti yake ya pazia hairuhusu mwanga chumbani au hata kukuondolea faragha. Itapendeza kama utachagua ambazo zina ushirika na vitambaa vilivyotengenezea viti na sofa ambapo vinatakiwa kuwa imara, rahisi kusafishika, visivyodaka uchafu kirahisi na pia visivyopauka na vinene kuliko vitambaa vya mavazi.

Njia zifuatazo zitakuwezesha kutengeneza ushirika kati ya rangi na michoro ya pazia na viti.

Kutumia kitambaa kinachofanana
Njia nyepesi zaidi ya kuleta ushirikiano kati ya pazia na viti ni kwa kutumia kitambaa kinachofanana kwenye vitu hivi viwili. Hii inakifanya chumba kiwe na umoja kwa upande wa rangi na michoro, inapendeza sana pale hizo pazia na viti vikiwa pande tofauti za chumba. Kama rangi ya pazia ni nzito, namna nyingine ni kutumia  kwenye viti au sofa kitambaa ambacho kina rangi ya familia moja. Kwa mfano pazia za bluu nzito zinaweza zikashirikishwa na vitambaa vya viti vya bluu nyepesi.

Rangi zinazoshabihiana
Rangi za pazia na viti zinaweza kushirikiana kwa kutumia rangi ambazo zinaendana badala ya zile zinazofanana. Rangi zinazoendana huwa ni tofauti kabisa lakini zikiwa pamoja zinaleta mvuto kwa mfano bluu na nyeupe, zambarau na njano, nyekundu na nyeupe na pia majenta na chungwa. Kutumia rangi za seti hizi kwenye pazia na viti kunakifanya chumba kisionekane kulipuka sana ukilinganisha kile ambacho rangi za pazia na viti zinafanana. Hapo ndio utaona kila jambo lina faida na changamoto zake.

Rangi ya kitu kingine
Pazia na viti inaweza kuwekwa kwa jinsi ambayo italeta ushirikiano kwa kutumia kitu cha tatu kilichopo hapo chumbani. Kwa mfano kwa kushirikisha rangi ya fenicha au zulia.

Rangi isiyoegemea upande wowote
Kushirikisha viti na sofa za rangi kwa pazia za rangi isiyoegemea upande wowote kama vile, krimu, kijivu au nyeusi ni njia nyingine ya kuleta ushirika wa rangi chumbani. Hapa pazia zinachukua nafasi ya kutuliza zile rangi za sofa au viti. Kama rangi ya kuta pia ni isiyoegemea upande wowote basi sofa na viti vinapewa nafasi ya kuchomoza na kuwa kitovu cha jicho.


Hakika hizi njia nne zitakuwezesha kutengeneza ushirika mzuri kati ya rangi za pazia na zile za viti na sofa.

No comments:

Post a Comment