Kwa lengo la kutengeneza sebule yenye hisia ya utulivu,
muonekano wa usafi na kiwango njia mojawapo ni kwa kutumia rangi za familia ya
bluu. Mara zote bluu
imekuwa ni rangi freshi na inafanya ndani kuwe na uhai. Usishangae ni kwanini
sebule za bluu zinaonekana nadhifu na maridadi ziadi.
Rangi
mbalimbali zilizo kwenye familia ya bluu zinafanya ndani kupendeze na bila
shaka kuvutie. Unaweza kutumia bluu ukutani, kwenye zulia, pazia au
vifaa
vingine kama vile taa za vivuli, mito ya mapambo, mapambo ya kwenye shelfu,
mezani na ya kwenye kabati la maonyesho na hata bluu kwenye fenicha. Vitu hivi vinavyoweza
kuwa na rangi moja ya bluu au miguso ya bluu katika muundo wa maua au michoro
yake vinaifanya sebule kuwa na muonekano wa kisasa.
Mandhari inakuwa ya kuvutia kiasi kwamba
unatamani kutumia siku nzima ukiwa umekaa sebuleni.
Bluu
ni rangi tulivu ya asili, japo sio siri kuwa wengi wanashindwa kupendezesha
sebule kwa kutumia rangi hii. Sababu zinaweza kuwa mbalimbali kama vile
kutokufahamu ni kwa namna gani wanaweza kuishirikisha na rangi nyingine na
rangi hizo ni zipi. Inachukua nguvu ndogo tu ya kuchagua na kuoanisha rangi
nyingine tulivu zinazoendana na bluu kama vile kijivu, zambarau, nyeusi, krimu
na nyeupe. Au kama unataka kuonyesha msisitizo wa ndani mwako, oanisha bluu na
rangi za metaliki au damu ya mzee.
Pazia
zenye michoro au maua ya bluu ni ongezeko lenye kuvutia sebuleni. Pazia za maua ya bluu sebuleni zinapendeza
pale ambapo kuta zina rangi ya krimu au nyeupe kwani inatengeneza muonekano wa
utulivu. Bluu hiyo inapotumika madirishani na kwenye vitupio kama vile mito ya
makochi, zulia na mapambo mengine inafanya ujirani mzuri wa rangi kati ya
maeneo hayo mawili.
Pia
kama sofa ni la rangi za jamii ya bluu, pendezesha sebule kwa zulia la rangi ya
kijivu. Au njia nyingine ni ya kuwa na
pazia za krimu unazozioanisha na kiti au sofa zilizotenenezwa kwa kitambaa cha
maua au michoro yenye rangi ya bluu iliyokolea, yaani bluu nzito kwenye rangi
za familia ya bluu.
Bluu
na krimu laini ni njia ya ajabu ya kutuliza chumba hasa sebule. Muunganiko huu
unaendana na fenicha za rangi nyepesi kama vile zilizopaushwa na jua. Kwenye
fenicha hizo weka mapambo madogodogo na vitupio vyenye bluu ya kukolea na ile
ya kuwaka.
Kwa
ukutani unaweza kutumia bluu pia ila uzingatie kuwa bluu nzito inafaa pale
ambapo sebule ni kubwa na inapokea mwanga mwingi wa jua, kinyume cha hapo bluu
hii itasababisha giza. Ikiwa unataka kuongeza mwanga sebuleni tumia bluu
nyepesi pamoja na njano.
Kuna
njia nyingi mno za kuweza kupendezesha sebule kwa bluu. Kikomo ni ubunifu wako!
No comments:
Post a Comment