Tuesday, October 4, 2016

Njia kuu 4 za kuaminika ili kuongeza nafasi kwenye chumba cha kulala

Inawezekana umepanga nyumba yenye chumba kidogo cha kulala. Na kama tujuavyo nyumba nyingi za kupanga hazina ile mifumo ya kukuwezesha kupangilia vitu vyako kama vile makabati ya nguo na kadhalika. Hata hivyo unaweza kuishi vizuri mno kwenye chumba hicho kidogo endapo utafahamu jinsi ya kukiweka katika muonekano sahihi.

Kuna mbinu nyingi ya kukipanga chumba cha
kulala kikaonekana kuwa na nafasi kubwa endapo ndicho unachojaribu kwa sasa. Nimebahatika kutembelea nyumba nyingi  na kwa kadri ninavyojua kuna njia kuu nne muhimu zinazoweza kukupa matokeo mazuri ya kuwa na nafasi ya kutosha ndani ya chumba kidogo cha kulala bila chumba hicho kuonekana kuwa na mrundikano.

Njia ya kwanza ni kuweka kitanda karibia na ukuta halafu unakamata fursa ya huo ukuta wa kichwani mwa kitanda. Ni ukuta ambao unakaa tu bila kazi yoyote na unafaa kuwekea shelfu au kabati (endapo utaweka na milango) kwa ajili ya kuhifadhia baadhi ya vitu kwani sio sehemu ambayo wala unapita kwamba shelfu zitakukera. Hakikisha kuwa vitu vya kuhifadhi kwenye shelfu hizi ni vile ambavyo hata kwa bahati mbaya vikikudondokea ukiwa umelala havitakuumiza, kwa mfano nguo, shuka na taulo.

Njia ya pili ni kwa kuwa na stendi rahisi kwa ajili ya kutundikia pochi, tai, mikanda, skafu na vingine vingi vinavyowezekana kutundikwa kwa mtindo huu. Stendi hii huwa ina uwezo wa kusimamishwa kwenye kona na kutundikwa  vitu vingi sana na huku ikichukua eneo dogo tu. Na kwa upande wa nguo za kutundika jipatie stendi nyingine kwa kazi hiyo. Maana zile za kukunja tayari una shelfu za kichwani mwa kitanda.

Ukipiga mahesabu ya haraka utakuwa umebakiwa na vitu kama masanduku na viatu ambavyo pengine huna pa kuvihifadhi. Ukisema uongeze raki ya viatu inaweza kusababisha muonekano wa mrundikano kwani tayari kuna stendi ya nguo na ya pochi. Habari njema ni kwamba kuna mvungu wa kitanda ambapo pako tu wazi. Tumia mvungu kupanga viatu na kule kwa mbali kabisa hifadhi masanduku na boksi za vitu usivyotumia mara kwa mara. Kama utakuwa umefikiria toka mwanzo unaweza kuagiza kitanda chenye miguu mirefu ili kufanikisha zaidi ongezeko la nafasi mvunguni.


Kwa ufupi ni kwamba unavyokuwa na maeneo mengi ya kuhifadhi vitu ndivyo nafasi ya chumba inavyoonekana kubwa. Tumia eneo la nyuma ya mlango kutundika mfuko (mithili ya ile ya viatu) wenye vyumba vingi vidogodogo kwa ajili ya kuwekea vitu kama vile chanuo vipodozi na vibanio huku kioo cha kujitazama ukiwa umekichimbia ukutani kwahivyo unajikuta wala huna haja ya dressing table itakayokumaliazia nafasi bure.

No comments:

Post a Comment