Milango
katika nyumba nyingi mara nyingi haifikiriwi kufanyiwa usafi. Ni ile ya vyumba
vya kulala, ya makabati ya nguo, ya mabafu, wa jikoni na wa stoo. Labda ni
kwasababu haipati uchafu kwa wingi na kwa muda mfupi kama maeneo mengine ya
ndani. Hata hivyo inapaswa kusafishwa kila baada ya kipindi fulani. Ikiwa ni
pamoja na eneo lenye kitasa linapaswa kusafishwa na
kutakatishwa kwa dawa ya
kuua vijidudu kwani kinashikwa na mikono mingi na kila mkono unatofautiana na
mwingine kwa kiwango cha usafi. Zifuatazo ni dondoo za namna ya kusafisha
milango ya ndani ya mbao, ambapo tunaugawa mlango kwenye maeneo matatu ambayo
ni fremu, mlango wenyewe na kitasa.
Anza
na kufuta vumbi la juu maeneo yote matatu ya mlango kabla ya kutumia aina
yoyote ya kimiminika cha kusafishia. Kurukia moja kwa moja kusafisha kwa
kimiminika kutasababisha kusambaza vumbi kwa kutengeneza tope hivyo kuongeza
ukubwa wa kazi. Vile vile kuufuta mlango ili kuondoa vumbi na chembechembe za
juu za uchafu kwanza, inasaidia kuepuka kuusababishia mikwaruzo na uharibifu.
Baada
ya kufuta vumbi, anza kwa kusafisha kuanzia juu kushuka chini fremu iliyozunguka
mlango wote. Tumia kitambaa au sponji lililoloa maji matupu ili kuondoa ngazi
ya mwanzo ya udongo. Kama fremu hiyo haitakua chafu kivile, maji matupu
yanaweza kuondoa uchafu wote. Laa endapo
inahitaji usafi wa kina, tumia maji ya uvuguvugu na sabuni. Ipo milango ambayo
inakaa muda mrefu sana bila kusafishwa kiasi kwamba eneo la bawaba linakuwa limeshaanza
kuvujisha vilainishi vyake au hata vilainishi hivyo vimeshakauka na kusababisha
mlango kupiga kelele pale unapofunguliwa au kufungwa. Baada ya kusafisha eneo hili la mlango la
fremu, tumia kitambaa safi na laini kuikausha
ibaki kavu. Kuendana na hali iliyopo unaweza kuhitajika kupaka upya kilainishi
kwenye bawaba.
Umeshamaliza
kusafisha fremu, sasa unahamia kwenye mlango wenyewe. Kwa ajili unakuwa
umeshafuta vumbi unapitia tena hatua hizihizi kama za kusafisha fremu, huku
ukikumbuka kusafisha hadi eneo la ubavuni linaloshikana na fremu. Ni lile ambalo huwezi
kuliona mlango ukiwa umefungwa, ingawa linaweza kubeba uchafu mwingi sana.
Ng’arisha
mlango wako kwa kutumia ving’arishi vya fenicha za mbao vinavyouzwa madukani.
Malizia
kwa kusafisha eneo la tatu la mlango ambalo ni kitasa, kwa kutumia kitambaa
chenye unyevu kiasi huku ukiweka umakini wa malighafi iliyotengenezea kitasa
hicho. Kwa mfano kama kitasa ni cha brasi unaweza kununua bidhaa maalum
zilizotengenezwa kwa ajili ya kusafishia brasi. Mwisho kausha kitasa na kama
una dawa ya kuua vijidudu kipake au kipulizie.
Muhimu
unaposafisha mlango wa mbao kuepuka kutumia kemikali ambazo hazijaidhinishwa
kwa matumizi ya kwenye mbao kwani unaweza kuharibu finishing ya mlango.
Kwa usafi wa majumbani na ofsini waone Cleanex Group simu namba 0713 064 064
No comments:
Post a Comment