Lile sakata la Askofu Benson Bagonza wa
Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Karagwe mkoani
Kagera kudaiwa kuzaa watoto wawili na muumini wake, Peace Sylvester limeendelea
kuchukua sura mpya kufuatia mwanamke huyo kumtaka askofu wakapime D.N.A.
Mbali na madai hayo, naye baba mzazi wa Peace, mzee
Sylvester Katoto (72) ameibukia jijini hapa na kumtaka askofu huyo kujitokeza
hadharani na kuikana damu yake hiyo mbele yake.Akizungumza hivi karibuni na
gazeti hili jijini hapa, mzee Katoto alisema ameamua kufika Arusha akitokea
Karagwe kumsaidia binti yake huyo na kuongeza kwamba amesikitishwa sana kwa
taarifa kuwa Askofu Bagonza amewatelekeza watoto wake.
“Nimeamua kuyasema haya ili jamii ijue. Bagonza aliwahi
kuja kwangu (Karagwe) baada ya Peace kujifungua mtoto wake wa kike na kunieleza
kuwa, yeye ndiye mhusika wa mtoto huyo
na aliniomba nimtunzie siri kutokana na wadhifa alionao kikanisa.
“Ninachotaka Bagonza ajitokeze ana kwa ana na ayakane
hayo maneno aliyoniambia, pia nataka aikane damu ya hawa watoto hapa
hadharani,’’ alisema.Mzee huyo aliongeza kusema kwamba, yeye na watoto wake
watatu wa kiume waliamua kufunga safari mpaka Arusha kukanusha barua
iliyoandikwa na mtoto wake (jina tunalo) ikisema kwamba, ukoo umemtenga Peace
kufuatia sakata lake na askofu huyo kurindima kwenye vyombo vya habari.
“Tutakwenda Ustawi wa Jamii kupeleka malalamiko yetu ili
waone uwezekano wa kumwita askofu. Nimejaribu kumpigia simu na kumtumia ujumbe
wa maneno (SMS) lakini hajanijibu hadi sasa.“Lengo letu ni kuhakikisha Peace
anapata haki yake na si vinginevyo, pia namtaka askofu kuacha kuwatumia watu
wengine katika suala hili ila ajitokeze ili azungumze na mimi,’’ alisema mzee
Katoto.
Katika hatua nyingine, Peace ambaye ndiye mlalamikaji
alimtaka mtu aliyenukuliwa na gazeti moja la kila wiki (si la Global Publishers
ambayo ni makini) akidai watoto hao ni wake, ajitokeze hadharani na awe tayari
kwenda kupima kipimo cha vinasaba (D.N.A) ili kubaini ukweli.
“Pia namtaka Askofu Bagonza twende wote tukapime kipimo
hicho kitakachothibitisha kuwa watoto hawa baba yao ni yupi na nasisitiza
askofu ajitokeze hadharani aikane damu yake kama anaweza,” alisema Peace.Peace
alikwenda mbele zaidi kwa kusema kuwa, wiki iliyopita askofu mmoja wa kanisa
hilo mkoani Kagera (jina tunalo) alimfuata Arusha kwa ajili ya kushughulikia suala hilo.
Alisema askofu huyo alimwambia asiendelee tena
kulitangaza jambo hilo kwani linashughulikiwa hatua ambayo Peace alisema hadi
sasa hajapata mwafaka badala yake ameona kwenye gazeti moja la wiki kuwa
aliyezaa na Peace ni mwanaume mwingine ambaye alidai hamfahamu na kudai kwamba
amepandikizwa ili kuiaminisha jamii.
Peace kwa sasa
anajipanga kulifikisha suala hilo Ustawi wa Jamii na Kituo cha Sheria na
Haki za Binadamu kwa ajili ya msaada zaidi na ameiomba jamii na taasisi
zinazotetea haki ya mwanamke zijitokeze kumsaidia ili haki ipatikane.
Alimlaumu kaka yake mmoja kwa kitendo chake cha kumvamia
na kumpiga baba yake na ndugu zake hapo nyumbani kwake baada ya kukataa
ushawishi wake kuhusu kuegemea upande wa askofu.
Gazeti hili lilimtafuta Askofu Bagonza kwa njia ya simu
ambapo alipokea na baada ya mwandishi kijitambulisha alikata simu na
alipopigiwa tena alipokea mtu aliyejitambulisha kuwa ni dereva wake ambaye
alisema askofu alikuwa bize.
Katika Gazeti la Ijumaa Wikienda (ndugu na hili), toleo
la 407, Aprili 20-26, 2015, ukurasa wake wa mbele kulikuwa na habari yenye
kichwa; AIBU…ASKOFU KKKT APIGA MIMBA MBILI NJE YA NDOA.
Katika habari hiyo, Peace alimlalamikia askofu huyo kwa
kumzalisha watoto wawili, Piana (6) na Bariki (3) lakini amewatelekeza.Alisema
kufuatia hali hiyo, alimfungulia askofu mashitaka katika Kituo Kikuu cha Polisi
cha Arusha na kunukuliwa katika jalada lenye kumbukumbu Na. AR/RB/5290/2015 KUTELEKEZA FAMILIA.
GPL
No comments:
Post a Comment