Friday, May 15, 2015

Njia kuu tatu za kusafisha zulia lako

Zulia safi ni muhimu kwa muonekano wa nyumba na kwa afya ya watu wanaoishi humo. Zulia chafu na lenye madoa linaweza kuleta ukakasi kulitazama na kusababisha mazingira yasiyokuwa na amani, na wakati huo huo kusababisha mzio na magonjwa ya mfumo wa hewa. Kuna njia kuu tatu za kusafisha zulia kutegemea na kiwango cha uchafu.
Njia ya kwanza ni kusafisha zulia kwa kutumia mashine ya upepo. Hii ndio njia ya kitaalam inayopendekewa zaidi. Ingawa baadhi kwa kutokujua au hali ya uchumi wanasafisha zulia kwa kufagia ambapo husababisha kusambaza vumbi ndani badala ya lengo la awali la kusafisha. Na makala hii itaongelea njia hizi kuu tatu za kusafisha zulia kwa nia ya kuondoa vumbi, madoa, tope na unyevu.

Tukianza na njia ya kwanza ambayo ni kusafisha kwa mashine ya upepo ni kwamba zulia linatakiwa kunyonywa vumbi na chembechembe kwa kutumia mashine hii walau mara moja kwa juma na mara zaidi kwa zile sehemu zinazopitiwa mara kwa mara. Kusafisha zulia kwa njia hii kunasaidia kuongeza uhai wake kwa kuondoa zile chembechembe ambazo zingeweza kuharibu nyuzi za zulia. Kuwa makini wakati wa kusafisha kwa njia hii hasa pale ambapo nyuzi za zulia hilo ni nene, kwa ajili takataka nyingi zinazama chini hivyo waweza kupitisha mashine mara moja na kurudiarudia ili kutoa taka za chini kabisa.

Wakati wa kusafisha zingatia yale maeneo ambayo watu wanakaa na kuchezesha miguu yao kwani yanakuwa na uchafu mwingi. Njia ya kusafisha zulia kwa mashine inatakiwa zulia liwe kavu kila mahali. Hii ni kwakuwa endapo sehemu itakuwa ina unyevu, vumbi lililopo kwenye mfuko wa mashine likikutana na maji linafanya tope na hivyo kuifanya mota ifanye kazi kubwa ya kupuliza zaidi ya inavyotakiwa na huenda ukaishababishia kufa mapema.

Njia ya pili ya kusafisha zulia ni kwa kutumia vimiminika ambavyo ni maji kidogo na dawa za kusafishia. Kama tulivyoona kuwa chembechembe na vumbi vinasafishwa kwa njia ya mashine je madoa inakuwaje? Chembechembe ni uchafu mmoja—madoa ni mwingine. Uchafu hizi mbili zinatokea japo kwa kila zulia na ni ngumu kuondoa. Kanuni namba moja ya kuepusha madoa kwenye zulia lako ni kuyasafisha papo kwa hapo mara yanapotokea. Kama ukilidaka doa likiwa halijakaukia kuna uwezekano wa kuliondoa kabisa. Taratibu safisha kwanza kwa maji kidogo ya sabuni na kitambaa au brashi laini sana ili usong’oe nyuzi pale ambapo doa limetokea kabla ya kutumia dawa yoyote ya kusafishia zulia ili kuweza kuondoa kiasi kikubwa cha uchafu huo. Baada ya hapo ndio tumia dawa kumalizia alama iliyobaki ili pawe sawa na kwingine. Na kabla ya kutumia dawa yoyote ya kusafishaia zulia, jaribu eneo dogo kuhakikisha kwamba haipaushi rangi.

Baada ya hapo kama eneo ni kubwa litakua limebaki na unyevu. Unachotakiwa kufanya ni kuchukua taulo jeupe kavu na kufuta sehemu ile ukikandamiza kwa nia ya kunyonya maji. Kama unaona kuwa unyevu ni mwingi unaweka kuweka hilo taulo nyeupe la bafuni kavu juu yake na kuliwekea kitu kizito ili likakandamiza au hata kuwambia mtoto arukeruke juu ya taulo. Litasaidia kunyonya maji kwa kiasi kikubwa ambapo baada ya kuliondoa kama mzunguko wa hewa ndani ni mzuri baada ya muda patakuwa pamekauka.

Tukienda kwenye njia ya tatu ni ya kusafisha zulia kwa kina. Kuna wakati kwenye uhai wa zulia, kusafisha kwa mashine ya vumbi au dawa za madoa hakuwezi kuhuisha tena muonekano wa zulia lako. Zulia linalotakiwa kufanyiwa usafi huu wa kina linakuwa na ishara nne ambazo ni: hali ya kuwa na mnato na rangi ya asili kupotea, maeneo yanayokuwa yamebakiwa na rangi ya asili ni kama vile mvunguni mwa kitanda na meza. Dalili nyingine ni zulia kujenga alama kwenye eneo la miguu ya viti na meza na pia kuhisi fukuto la vumbi pale unapoingia chumbani.

Kama zulia lako lina dalili yoyote kati ya hizi , basi ni wakati wa kulisafisha kwa kina. Ikiwa huna muda, nguvu na vitendea kazi vya kufanya kazi hiyo, ni wakati wa kuliondoa, kulibeba na kulipeleka kwa wataalam wa kusafisha mazulia. Na hapa ndio pale tunapoona maeneo mengi ya kusafishia magari kukiwa na mazulia yanayosafishwa ambapo husafishwa kwa maji ya msukumo mkubwa, kusuguliwa na dawa za kusafishia na baadaye kuanikwa hadi likauke kabisa bila kubaki na harufu yoyote.

Matatatizo maalumu ya zulia ni kama vile kuungua, doa kubwa, kusagika eneo linalopitwa sana na kupauka rangi. Suluhisho la matatizo haya ni kuficha eneo lenye tatizo chini ya kochi, kitanda ama meza, na pia unaweza kuweka kizulia cha kutupia eneo lile.


Makala hii imeandikwa na Vivi na kwa maoni au maswali tembelea www.vivimachange.blogspot.com

No comments:

Post a Comment