Walimu wa Shule ya Msingi Mwatulole mkoani Geita, hawana
meza wala viti hali inayowalazimu kukalia madaftari ya wanafunzi kwa
kuyatandika kwenye magogo.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti
juzi baada ya kukutwa
wamekalia madaftari, walimu hao walisema ukosefu wa samani shuleni hapo
unawaathiri katika ufundishaji.
“Wakati mwingine tunasahihisha madaftari, huku
tumesimama,” alisema Mwalimu Mathias Matiginya na kuongeza:
“Unakuta mwalimu ana vipindi vinne kwa siku, lakini
anaishia kufundisha viwili kutokana na kusimama muda mrefu, anachoka haraka.”
Pia, alisema shule hiyo ina walimu wengi na haina ofisi,
viti wala meza, hivyo walimu wanatumia darasa kama ofisi.
Mwalimu mkuu wa shule hiyo, Catherine Mgisu alisema suala
hilo limefikishwa kwa uongozi wa halmashauri na kamati ya shule.
Alisema kamati hiyo inafanya jitihada za kuhamasisha
wazazi kusaidia maendeleo ya shule ikiwamo upatikanaji wa viti na meza za
walimu.
“Hii shule ina changamoto nyingi siyo ukosefu wa vitu
hivyo tu, bali ina wanafunzi wengi, uhaba wa madarasa na madawati pamoja na
utoro wa wanafunzi,” alisema Mwalimu Mgisu.
Katika hatua nyingine; Mwalimu wa Taaluma, Salma Rajab
alisema anakerwa na wingi wa wanafunzi.
Alisema kutokana na hali hiyo kipindi cha mitihani mbanano huwa mkubwa hali
inayowanyima fursa ya kusimamia vizuri.
“Walimu tunapata shida hasa wanafunzi wanapofanya
mitihani, tunashindwa kupata uhalisia wa matokeo yao. Huwa hatulitawali darasa
kutokana na msongamano, hivyo tunakaa nje,” alisema Mwalimu Rajab. Mwalimu
Debora Lucas alisema darasa moja linachukua zaidi ya wanafunzi 3,000.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Geita, Magarita Nakainga
alisema alipokea taarifa ya changamoto hizo na kwamba suala hilo
linashughulikiwa ili kuhakikisha shule inakuwa na hali nzuri.
“Ni aibu kwa shule za mjini kuwa hivyo, hivi sasa
tunaweka mikakati ya kukarabati na kuboresha miundombinu tunakusanya mapato ili
tuanze kazi hiyo,” alisema.
MWANANCHI
No comments:
Post a Comment