Thursday, August 1, 2013

My article for newspaper: vizulia vya bafuni



Pendezesha bufuni kwako kwa kuweka vizulia

Ni wachache wetu wanatumia muda wao wa thamani kuweka mazingira yenye kuleta mvuto na burudiko bafuni. Unaweza kuweka vizulia vya bafuni  kwa matumizi na pia kama mapambo kuongeza ufahari wa muonekano wa bafu zako. Bafu nyingi zina sakafu za marumaru ambayo inaonekana maridadi sana lakini inaweza kuwa baridi kwa vidole vya miguu mitupu. Vizulia vya bafuni zaidi ya kuwa mapambo ni burudani kwa miguu yako.

Vizulia vya bafuni vinaweza kusaidia sakafu ya bafu kuwa na hisia ya joto na mvuto kwa watu waliopo ndani ya nyumba. Vizulia vingi vya bafuni  havitelezi  na vinatumiwa sana bafuni kuruhusu watoto na wazee kujikinga na sakafu ya baridi.

Vizulia vya bafuni ni njia rahisi kuliko zote za kuleta muonekano maridadi bafuni. Wala hutakiwi kupaka rangi upya au kuweka marumaru mpya ili kuleta muonekano mpya bafuni. Wewe weka tu vizulia sahihi na vitupio kadhaa na kila mtu atadhani kuwa umejenga upya bafu zako.
Unaweza kupata vizulia lukuki ambavyo vitakufaa kwa matumizi ya bafuni. Ila kwa kawaida huwa vizulia vya bafuni vinakuja kwa seti yake lakini hii haikuzuii kuwa mbunifu kwa kuweka vizulia bafuni kwa ladha yako.  

 Huna haja ya kung’ang’ania vizulia vya umbo la yai na duara ambavyo vimezoeleka na wengi kuwa ndivyo vya bafuni.
Wakati wa kuchagua vizulia vya bafuni ni muhimu kuzingatia kuwa bafuni ni muhimu kama vilivyo vyumba vingine vilivyo ndani ya nyumba yako. Kwa hiyo chukua muda kufikia maamuzi juu ya ni muonekano gani unataka kuujenga bafuni. Kwahivyo moja kwa moja utachagua vizulia sahihi kwa kuhuisha mapambo yako ya bafuni.

Seti za vizulia vya bafuni ni gharama nafuu kwa mtu wa maisha ya kati na kuna aina mbalimbali kwa mhusika kuchagua. Kama wakati wa kuchagua sakafu ya kuweka kwenye nyumba unavyohitaji iwe imara, vilevile kabla ya kununua vizulia vya bafuni hakikisha kuwa vinadumu,  vinaweza kustahimili mazingira ya bafuni, ni rafiki kwa watoto, vinaonekanaje na unavihisije ukiwa na umevikanyaga kwa miguu mitupu.
Sakafu ya bafuni huwa inapata matone ya maji ambapo inaweza kusababisha utelezi. Vizulia vya bafuni vinakupa kituo cha kusimama kwa kujiamini kuwa hutaanguka pale unapotoka kwenye sinki au bomba la mvua la kuongea.

Vizulia vya bafuni vinatakiwa viwe vinavyosafishika kirahisi . Havitakiwi kuwa na unyevu nyevu unaotokana na maji ya moto ya bafuni. Vile vizulia vyenye mpira kwa chini ni sahihi kuzuia uozo na kuvujisha maji. Hata hivyo jua kuwa vizulia vitatakiwa kuanikwa mara kwa mara kufanya tatizo la unyevu na uozo lisiwepo.
Vizulia vya bafuni mara nyingi vinawekwa yale maeneo yanayoweza kuloa maji kirahisi. Maeneo hayo hasa ni kama pale kwenye eneo la kuogea  na la kunawia mikono. Pia vinaweza kuwekwa kama tandiko la mlango wa bafuni. Ukubwa wa bafu ndio utaamua kama uweke kizulia kikubwa au vingi vidogodogo.

Ingawa kulikuwa na hasara kadhaa za kuweka vizulia bafuni, watengeneza mazulia wamechukua hatua madhubuti dhidi ya malalamiko makuu kuhusu zulia za bafuni – unyevu, ukungu na madoa. Ni rahisi kubadilisha zulia kuliko kubadilisha sakafu iliyooza.

Baadhi ya njia za kawaida ambazo vizulia vinaweza kukutana na unyevu bafuni ni pamoja na bakteria wanaojazana kwenye lile eneo la kuzunguka sinki la choo. Bakteria wanaokuwa kwenye mkojo kwa bahati mbaya wanaweza kusambaa kwenye zulia. Safisha vizulia mara kwa mara kuondoa ukungu na bakteria wanaoweza kuwepo. Hakikisha mara zote vizulia ni vikavu iwezekanavyo. Pia kuna vifaa mbalimbali vinavyoweza kusaidia kuzuia maji yasipite kwenye pazia la bafuni na kurukia kwenye kizulia.

Ingawa kizulia chochote kinaweza kutandikwa kwenye sakafu ya  bafuni, ambavyo vinatumika sana ni vile vizulia vya bafuni vyenye mpira kwa chini. Faida ya zulia za bafuni ni kuwa zinafanya bafu lionekane maridadi na lenye mvuto. Ni vilaini kuliko marumaru kwa hivyo watu wengi wanaburudika kuvikanyaga na miguu mitupu.  Ajali za kuteleza bafuni zinapungua.  Ni rahisi kuteleza kwenye sakafu ngumu ya bafauni kama vile marumaru kuliko kwenye zulia.

Kumbuka mapambo mengine hapo bafuni. Fikiria mwanga wa taa na rangi ya sakafu na vifaa vingine vya usafi vilivyopo hapo bafuni. Vizulia vya rangi za kung’aa  vinafaa kwenye bafu za watoto na vinaleta mvuto sana sakafuni.  Kwahivyo kama unataka macho yaelekee kwenye vitu vingine kama kioo cha ukutani weka vizulia vya bafuni visivyokuwa na rangi kali. Staili na mandhari mbalimbali zinaweza kupatikana mitandaoni au kwenye majarida ya mapambo ya ndani.

Kwa hivyo kama unataka kuweka muonekano mpya wa bafu lako vizulia ni chaguo sahihi na gharama nafuu zaidi. Vizulia sahihi vya bafuni vitafanya bafuni kuwe sehemu ya burudani kwa watoto. Ulishapata ugeni wa watoto nyumbani na wakawa hawaishi kuomba kwenye bafuni? Ni kwa kuwa kunavutia! Hebu fikiria umeweka vizulia vyenye katuni za spiderman, pazia la bafuni na miswaki inayooana, hutakaa ugombane tena na watoto wako wadogo kuhusu kupiga mswaki na kuoga. Vizulia visiwekwe kwenye bafu za jumuiya!

Makala hii imeandaliwa na Vivi O. Machange. Vivi anajishughulisha na usafi wa mazulia na nguo aina zote; pia ana mapenzi makubwa ya mitindo na mapambo ya nyumbani. Kwa maoni au maswali tuma kwenda viviobed@yahoo.co.uk au 0755 200023

No comments:

Post a Comment