Friday, September 4, 2015

Vitu unavyoweza kuweka kwenye kabati la vyombo, zaidi ya vyombo

Tuseme una kabati lako la vyombo ambalo lina vipande viwili – kipande cha juu kikiwa na milango ya kioo na cha chini kikiwa na milango ilisiyoonyesha kilichomo ndani kwa mfano milango ya mbao au malighafi nyingine. Kwa kawaida sehemu ya chini ya kabati haina mvuto ila hii ya juu ndio inavutia.
Kwa pamoja sehemu hizi mbili zinajitosheleza na kuleta muonekano wa kabati moja kubwa lililokamilika, refu linalokaribia kugusa dari.

Wengi mtakubaliana na mimi kuwa mnatumia sehemu ya chini kwa vyombo vyote lakini hii ya juu mnaitumia kuweka vile vyombo vyenye mvuto.
Ukitumia kabati hili kama ilivyokusudiwa, linaleta mvuto wa kipekee kwenye chumba cha chakula au sebuleni. 

Sasa changamoto ni kuwa wapo ambao hawajui ni vitu gani zaidi ya vyombo ambavyo wanaweza kuweka kwenye kabati lao hilo! Hivyo basi zifuatazo ni dondoo za kukufahamisha vitu zaidi ya vyombo unavyoweza kuweka kwenye kabati la vyombo na kuliwezesha livutie zaidi:

Kutegemea na ni wapi umeweka kabati, unaweza kulitumia kuweka vitu vya ziada kama vitabu, majarida au vitambaa vya mezani na vitaulo vya jikoni.

Unaweza kuweka chochote ambacho unakipenda na pia kitapendeza machoni mwa wengine kama vile fremu za picha za familia na inasemekana zile picha za rangi nyeupe na nyeusi ndio zinafaa zaidi,  mikanda ya video na mziki. Kuwa mbunifu!

Glasi, sahani, vyungu na birika za mapambo tu na sio kwa ajili tu kutumika.

Unaweza kutandika kitambaa cha mapambo juu ya kabati. Naamini msomaji wangu kama wewe ni mtu wa zamani unakumbuka nyakati ambao wengi walikuwa wanatandika vitambaa vya kijani vilivyodariziwa juu ya makabati ya vyombo. Vivyohivyo leo hii unaweza kuwa na kitambaa cha rangi au michoro unayoipenda na ukakitandika juu ya kabati la vyombo.

Unaweza kuweka vishikio vya mishumaa na mishumaa.
Unaweza pia kuweka vitu vya msimu wa sikukuu.

Kwahiyo una sehemu mbili za kuweka vitu zaidi ya vyombo kwenye kabati lako la vyombo. Juu ya kabati na ndani kwenye milando ya kioo, zitumie ipasavyo kuleta umaridadi.

No comments:

Post a Comment