Kusafisha
madirisha na milango ya kioo nyumbani ni moja ya kazi ambayo inawezekana unaipa
wasafishaji wa nje waifanye kwa kuhofia kuwa ni ngumu. Japo kiukweli haipaswi kuwa
kazi ngumu, kama unajua mbinu na hatua sahihi za kupitia ili kufanikisha kwa
urahisi. Zifuatazo ni hatua za kupitia ili kufanikisha kusafisha maeneo yenye
vioo yang’ae kabisa.
·
Pangu muda wa kusafisha
Safisha muda ambao jua halipigi moja
kwa moja kwenye kioo.
Jua kali linakausha dirisha mapema
mara unapoanza kuliloanisha kabla ya
kulisuuza ambapo inaacha ukungu wa dawa ya
kusafishia au matone ya maji na hivyo kukulazimu kurudia tena zoezi hilo. Ili
kuepuka hali hiyo, safisha asubuhi na mapema kabla jua halijawa kali au subiri
hadi siku yenye mawingu.
·
Andaa vitendea kazi
Vimiminika vya kusafishia vyaweza
kuwa vya aina mbili, ya kwanza ikiwa ni ile dawa maalum iliyotengenezwa kwa
lengo la kusafishia vioo na aina ya pili ikiwa ni kutumia maji. Endapo unatumia
maji yachanganye na kiasi kidogo cha vinega kwa uwiano wa kipimo kimoja cha vinega
kwa vipimo kumi vya maji. Vifaa vingine ni sponji, kitambaa kikavu cha pamba au
magazeti, brashi ndogo laini na ngazi ndogo endapo madirisha yako umbali mkubwa
toka ardhini.
·
Safisha
kuanzia juu kushuka chini
Ikiwa
kweli unataka usafishe eneo lenye kioo litakate na kung’aa, basi safisha
kuanzia juu kushuka chini. Kufanya hivyo kutakuhakikishia kuwa hakuna uchafu
utakaodondokea kwenye sehemu ambayo umeshasafisha tayari.
Kama eneo la kioo unalotaka kusafisha
ni chafu sana kwa mfano kuna vumbi jingi au utando wa buibui, inakupasa kutumia
kitambaa kikavu kuondoa uchafu huo kwanza. Kwenye kona kuna kawaida ya uchafu
kuzama kwahivyo tumia brashi laini kuuondoa.
·
Loanisha kioo
Kwa kutumia sponji lenye maji loanisha
kioo huku ukiepuka kuweka maji mengi kiasi cha kuchuruzikia kwenye fremu ya
mlango au dirisha la kioo unalosafisha. Suuza na kausha kioo kwa kutumia
kitambaa kikavu halafu mwishoni ng’arisha kwa kufuta na kipande cha gazeti.
Endapo unatumia dawa za kusafishia
kioo basi inakupasa kuipulizia kidogo kidogo moja kwa moja kwenye kioo huku
ukifuta haraka haraka kabla haijakaukia. Tumia gazeti au kitambaa cha pamba
ambacho hakitoi nyuzinyuzi.
Pia ni vyema kufahamu kuwa baadhi ya
dawa za kusafishia vioo zinaharibu mbao. Kuwa makini kama fremu ya eneo la kioo
unalosafisha imetengenezwa kwa mbao, puliza dawa kidogo kidogo na epuka
kuigusisha na fremu.
·
Safisha fremu na kona kwa kitambaa
tofauti
Haijalishi ni ngumu kiasi gani
unaweza kuondoa uchafu kwenye eneo la kioo, lile la kona na fremu ndio linabeba
uchafu mwingi zaidi kama huna vifaa sahihi. Safisha maeneo haya kwa kutumia kitambaa
au fulana zee ya pamba, inanyonya uchafu wote na kuacha fremu safi.
Madirisha ya kioo inapaswa yawe
yanasafishwa kwa kina angalau mara moja kila mwezi au walau kila baada ya miezi
miwili.
No comments:
Post a Comment