Utepe
wa kitambaa cha meza (table runner)
ni kitambaa chembamba kinachotandazwa katikati ya meza. Ni njia rahisi na ya haraka
ya kubadilisha muonekano wa meza yoyote ile. Vitambaa hivi vinapatikana kwa
ukubwa, rangi na malighafi za aina mbalimbali. Wakati unaweza kufuata kanuni
katika kutumia utepe wa mezani lakini pia unaweza kuwa mbunifu mwenyewe na
kuutupia kwa jinsi unayoona inakupendeza.
Upana
wa utepe unatakiwa uwe theluthi ya upana wa meza. Kwa maana hiyo unavyotupiwa
pale kati ya meza unabakiwa na pande mbili za meza zenye upana karibia sawa na
wa utepe. Na hii ni kama unatupia kwa kuendana na urefu wa meza. Endapo itakuwa
unatupia kwa upana, utahitaji tepe zaidi ya moja na upana unaweza kupungua.
Tepe
nyingi zimeshashonwa tayari na zinakuja kwa upana wa inchi 10, 12, 13, 14 na 15
na kwa urefu wa inchi 54 hadi 108. Kwahivyo kabla ya kununua unapaswa kufahamu
ukubwa wa meza unayotaka kuuwekea.
Kumbuka
kuwa hakuna kanuni hasa za kutumia utepe wa mezani, usiogope kama upana au
urefu hautakuwa jinsi inavyosemwa hapa, kinachotakiwa ni wewe ujue unachotaka, ukipende
na ujue jinsi ya kuupamba. Haya mambo ya vipimo yanahusu zaidi kwa upambaji wa
matukio rasmi kama harusi na warsha.
Na
hata kama vipimo hivi havitaendana na meza yako, maadam umeshajua mbinu ni
kiasi cha kutengenezesha kwa fundi (au hata ukashona mweneywe) kwa kitambaa
unachopenda kiwe ni batiki, kitenge na kadhalika.
Tepe
za mezani zinaweza kutumika kwa njia mbalimbali na kwa meza yoyote japo kiasili
zilitumika kwenye meza za chumba cha chakula, hata hivyo unaweza kuwa mbunifu
na kuzitumia kwenye meza yoyote iwe ni ile meza ndefu, ya kahawa, ya pembeni
mwa sofa, ya kwenye varanda au ya bustanini. Zinawezekana kwa meza ya umbo
lolote liwe pembe nne, duara na yai.
Njia
iliyozoeleka zaidi ya kutumia utepe wa mezani ni kwa kuuweka katikati ya meza
ukiwa unakimbia kwa urefu. Hii inasadia kuweka pambo la kati na hata mabakuli
ya vyakula kwenye mstari wakati wa kula. Huu utepe pia kinasaidia kufanya meza
isikwaruzwe na vyombo au mapambo mengine, na kukinga polishi yake isiharibiwe
na joto la vyakula.
Unaweza
pia ukatumia tepe fupi na nyembaba zilizowekwa kwa upana wa meza. Hizi za hivi
zaidi ya kutumika kama mapambo ya meza pia zinaweza kutumika kama mkeka wa meza
wakati wa kula kuwekea sahani.
Vimikeka
vidogo (mats) vya meza vya kuwekea sahani vinaweza kutumika pamoja na utepe kwa
rangi zinazofanana. Na kwa maana hivyo hutakuwa na haja tena ya kutandika
kitambaa cha meza.
Kama
vinatumika pamoja utepe wa mezani usifanane na kitamba cha meza, unatakiwa kuwa
na rangi tofauti ili uonekane usimame peke yake.
Unaweza
pia kutumia utepe wa mezani kwenye fenicha nyingine. Tumia tepe kulinda fenicha
zilizotengenezwa kwa glasi,utumie wakati unapotaka kuweka kitu juu ya meza
ambacho unadhani kitakwaruza meza.
Ni
vyema kuangalia ulaini wa kitambaa cha utepe kama utaendana na ulaini wa meza
yako. Kwa mfano, kama meza yako ina kioo au imepakwa polishi ina maana inateleza,
haifai kuweka utepe wa hariri (silk), satini ama polista. Tepe za namna hii zitafaa kwa zile meza
zisizokuwa na finishing ya kuteleza.
Utepe
za mezani uoane na mapambo yako mengine ya hapo chumbani.
Tepe
za mezani zinaweza kupatikana popote wanapouza vitambaa vya meza.
Tepe
za mezani ni njia bora zaidi ya kupamba meza kwa kuiongezea rangi na muonekano.
Zinapendeza pale zinapotumiwa na mapambo mengine mezani kama vile vesi ya maua
au bakuli la matunda.
Makala hii imeandaliwa
na Vivi ambaye ana mapenzi na muonekano wa nyumba. Kwa maoni ama maswali
tembelea www.vivimachange.blogspot.com
No comments:
Post a Comment