Thursday, January 2, 2014

My article for newspaper: malengo ya mwaka mpya



Ni wakati mwingine tena wa mwaka ambao wengi wetu wanapenda kufanya mabadiliko kwenye maisha yao. Je umeshafikiria mabadiliko ya mwaka mpya kwa ajili ya kiota chako? Japo mabadiliko haya yanajulikana na wengi zaidi kama maazimio, kwa kutia msisitizo zaidi makala hii itayaita malengo. Malengo yanatamkwa kwa kusisitiza wakati uliopo ni nini tamanio lako (kwa mfano kuamua kubadili mpangilio wa fenicha za sebuleni kwako ili kuwezesha kunogesha zaidi mazungumzo) wakati maazimio yanatamka ni nini ungependa huko mbeleni ya kuwa unaenda kufanya nini wakati ujao.
Mara nyingi malengo (au maazimio) ya mwaka mpya yanatupiliwa mbali hata kama nguvu za kutosha ziliwekwa ili kuhakikisha yanafanikiwa. Moja ya sababu za malengo kutofanikiwa ni mazingira ya nyumbani kwako kutosaidia kuwezesha mafanikio ya malengo hayo. Kama unataka kufanya mabadiliko ndani ya maisha yako bila kuhusisha mazingira yako kufanikiwa ni mbinde. Kwa maana ya kwamba kama unaweka malengo yako ya mwaka 2014 kwa ajili ya makazi yako na ukayaacha mazingira yalivyo, ni ngumu sana kubadili chochote. Hata matangazo kwa mfano ya kujikinga na maambukizi ya VVU yanaonyesha uhusiano kati ya maambukizi na mazingira fulani ambayo yanachochea maambukizi hayo.
Kanuni ya malengo kuwa na uhusiano na mazingira inahusika karibia katika kila kitu. Kama unataka mwaka huu uwe tofauti basi unatakiwa kuweka mazingira ya kuwezesha malengo yako.
Je mazingira yako yanakusaidia kupata kile unachokihitaji? Kwenye mazingira ya nyumbani kwako vitu ambavyo havijakaa mahali pake au vimekaa mahali ambapo havifanyi kazi yake au havitumiki tena vinakukwamisha kutimiza malengo yako hapo nyumbani. Tembelea kwenye makabati ya nguo na vyombo angalia kwa umakini kuona ni vitu gani vya kuhifadhi, vya kugawa ama vya kutupa. Fanya hivyo kwa nia ya kupata nafasi ya kile tu kitakachosaidia kufanikisha malengo yako.
Pengine lengo lako la mwaka mpya ni kutokula hovyo kwa nia ya kupungua uzito. Je mara zote unaingia nyumbani kwa kupitia mlango wa nyuma ambapo unaingilia moja kwa moja jikoni? Kumbuka kanuni kuwa unachokiona mwanzo kinagusa zaidi akili yako, kwa hiyo kama mara ungiapo ndani unakutana na jokufu, chakula na kadhalika utapata hamu ya kula hapo hapo. Tumia mlango wa mbele ambapo utaona kitu tofauti mara uingiapo ndani - kitu ambacho hakitakufikirisha kula.
Mahusiano mengi yanaweza kuboreshwa kwa mapambo ya nyumbani hasa katika swala la kuwasiliana. Je chumba cha kulala cha wakuu wa familia ni mahali patakatifu kwa wawili? Hakikisha vitu kama taa, vimeza, na viti kwenye chumba hicho viko viwili viwili.
Au lengo lako mwaka huu ni kuwa na wageni wengi zaidi nyumbani? Hakikisha basi mlango wa mbele unaonekana na kuna njia ya wazi ya kuingilia. Taa zinazomulika njia ya kuelekea mlango huo ziwe zinafanya kazi. Pitia mlango wa mbele kama mgeni mtarajiwa uone kama kila kitu kiko sawa. Je njia hiyo inakaribisha? Na sebule yako je nayo inavutia kwa ajili ya wageni wako wengi ambao unapenda kuwaalika nyumbani mwaka huu?
Kwa wale ambao azimio lao kuu la mwaka 2014 ni kupamba nyumba zao hakikisha unachagua rangi kwa umakini, fikiria mpangilio wa fenicha je zinawatendea haki watumiaji wa chumba husika. Angalia vitu ambavyo inabidi uvifanyie kazi ili kuboresha muonekano wa makazi yako. Kama kwa mfano sakafu ya sebule yako ni ya marumaru na unachoka kusugua na kusafisha kila siku na unakiri kuwa ni ngumu kuifanya iwe safi; basi weka zulia kubwa ambapo utasafisha kwa mashine ya upepo mara mbili au tatu kwa wiki.
Ikiwa unaazimia kutojaza vyombo vichafu kwenye karo basi mwaka ujao lenga kuosha chombo mara baada ya kukitumia. Na hata hakikisha wanafamilia wengine pia wanafanya hivyo.
Huenda kijani kinakubariki lakini huna eneo kubwa ya kuweza kuwa na bustani za ardhini. Otesha basi bustani za kwenye vyungu walau ukifungua pazia la chumba cha kulala kunapopambazuka ukutane na kijani. Azimia kupamba ndani mwako kwa maua freshi japo mara moja kwa mwezi.
Kweli, baadhi ya mabadiliko ya nyumbani kwako unaweza kuhitaji kutafuta msaada, lakini kuna mabadiliko mengi sana ambayo hayahitaji gharama lakini yanahitaji muda na nguvu ( na pengine kautaalamu)  kwahiyo kwa 2014 kwa nini usiazimie kupamba mwenyewe? Unaonaje? Ni azimio moja zuri kwa ajili ya makazi yako ambalo unaweza kutekeleza. Fanya usafi mkubwa ndani ya nyumba yako mara moja kwa mwezi ( weka tarehe kwenye kalenda yako na isismamie). Mwanamke unatakiwa upende usafi na usiwe mvivu. Shirikisha na wanafamilia wengine pia.
Hii inaweza isikubalike kwa baadhi ya watu ila ni mawazo binafsi kuwa azimia kila anayeingia ndani avue viatu mlangoni. Viatu vya wanawake vilivyo na visigino vya ncha kali mara nyingine vinakwaruza sakafu za marumaru na mbao na kuacha alama na vile vya wanaume baadhi vina soli zinazoacha rangi sakafuni na hivyo kufanya sakafu ionekane zee kuliko kawaida.
Mwaka huu lenga kuweka nyumba yako nadhifu kila mara kama vile unategemea mgeni wa heshima!
Makala hii imeandaliwa na Vivi O. Machange. Vivi ni mjasiriamali upande wa usafi wa magari, nguo na mazulia; pia ana mapenzi makubwa ya mitindo na mapambo ya nyumbani. Kwa maoni au maswali tuma kwenda 0755 200023 au viviobed@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment