Eneo la kufulia liwe
na muonekano na vifaa hivi.
Ni mara ngapi kwa juma ambazo unafua nguo? Familia ya watu wanne
kwa mfano, inaweza kuwa inafua kati ya mara 3-4 kwa juma. Kwa maana hiyo ni
vyema kuwa na chumba ama eneo maalum la kufulia nguo ambalo lina vitu muhimu
vinavyotakikana kuwepo ili kufanikisha kwa haraka na kwa urahisi mchakato mzima
wa kuondoa nguo kutoka kwenye uchafu hadi kuiweka katika hali ya kufaa kuvaliwa
tena.
Asilimia kubwa ya kaya katika nchi zinazoendelea hakuna
mahali au chumba maalum cha kufulia na badala yake hasa maeneo ya mijini mahali
pa kufulia ni juu ya shimo la maji taka! Hii sio sawa kwa mfuaji kwani muda
wote anaokuwa anafua pale anavuta hewa chafu inayotoka shimoni humo hivyo
kuhatarisha afya. Kwa wenzetu walioendelea na baadhi ya familia katika nchi
zinazoendelea, kwenye makazi yao wana chumba au eneo maalum la kufulia
linalokidhi viwango vya vifaa na mahitaji. Si sawa kuwa na eneo tu la nje
karibia na chanzo cha maji kwa ajili ya kufulia kwani kuna vitu muhimu ambavyo
vinafanikisha zoezi la kufua na kwa kweli huwezi kuvihifadhi nje tu kwenye eneo
hilo.
Eneo ama chumba cha kufulia kitafaa zaidi kikiwa kiko maeneo
ya uani. Ili kuwa na eneo sahihi la kufulia ambalo utaokoa muda na nguvu zako
na kukufanya uvutiwe na kazi hiyo fikiria shughuli zitakazofanyika hapo:
kuchambua nguo, kufua, kukausha, kunyoosha, kutundika na kukunja. Weka
mpangilio wa kuwezesha vifaa vyako viendane na mtiririko huo. Wala hutakiwi kuwa
na eneo kuubwa kwa kazi hii, dogo liwavyo, eneo hili litawezesha nguo zitoke
kwenye sinki iwapo unafua kwa mikono au kwenye mashine kwenda kukaushwa/kuanikwa,
na kupelekwa meza ama kaunta ya kunyooshea na kukunjwa ama kutundikwa kuendana
na hitaji la kila nguo.
Nchi yetu imejaaliwa kuwa kwenye ukanda wa jua la kutosha
ambapo hatuna haja ya kuwa na mashine za kukaushia nguo. Rasilimali ya jua tuliyonayo
inatutosha hatuhitaji kukausha kwa mashine za umeme. Kinachotakiwa tu ni kuwa
na kamba za kukaushia karibia na mahali pako hapo pa kufulia.
Ni lazima kuwa na mahali pa kutundikia nguo zinazonyooshwa
ambazo hazitakunjwa. Fimbo za kutundia mahali pa kufulia zinahusu. Fimbo hizi ziwe
mbali kidogo na ukuta ili nguo zilizokwisha nyooshwa zisiuguse. Fimbo hizi ni
za kutundika nguo kwa muda tu wakati wa kunyoosha kabla hasijasambazwa katika
makabati ya nguo husika. Zile nguo zinazokunjwa baada ya kunyooshwa nazo
zinahitajika mahali pa kuhifadhia kwa muda katika chumba cha kufulia kabla
hazijasambazwa kwenye droo zinazohusika. Kwa maana hiyo pamoja na fimbo ya
kutundikia, pia unahitaji kuwa na shelfu. Huu mpangilio ni kwa ajili ya
kurahisisha mchakato wa kuondoa nguo kwenye kutoweza kuvalika kutokana na
uchafu hadi kuiwezesha kuvalika tena; kwa hiyo ni kwa kaya yoyote na wala
usidhanie ni maisha ya watu wa daraja fulani tu.
Gawa sakafu ya eneo
lako la kufulia katika maeneo mawili. Lile la maji maji kwa mfano kwenye sinki
na lile kavu kwa mfano pale pa kunyooshea. Utajikuta hili eneo kavu halipati
maji kabisa na waweza kupamba hata kwa kizulia. Kama una mashine ya kufulia
weka upande sawa na wa sinki ili hata imuwie rahisi fundi bomba endapo kutakuwa
na tatizo lolote kwani bomba zote zitakuwa eneo moja na kufanya zile shughuli
za maji maji kuwa pamoja. Tenga la nguo chafu liwe jirani kwa ajili ya urahisi
wa kubeba na kuweka kwenye mashine au kwenye sinki.
Eneo la kamba za kukaushia lisiwe mbali na panaponyooshewa
ili iwe rahisi kuanua nguo na kupeleka moja kwa moja kwenye kaunta ya
kunyooshea. Ili kutumia eneo dogo mara nyingi baadhi ya wenye nyumba wanapenda
kujenga kaunta ya kunyooshea juu ya mashine ya kufulia. Inakuwa ni busara
kutumia eneo hili la juu ya mashine badala ya kuliacha bure na badala yake kwenda
kuweka kimeza cha kunyooshea kwingine. Na kwa bahati nzuri mashine za kufulia
kwa ajili ya majumbani zina urefu chini kidogo ya meza ya kunyooshea kwa hivyo
hakuna ubaya kujengea hii kaunta ya kunyooshea juu yake. Pia kaunta iliyojengwa
kwa zege kwa ajili ya kunyooshea ni imara na inadumu maisha kulinganisha na
meza.
Kuweka vifaa katika mpangilio kunarahisisha mambo. Kusanya
sabuni na dawa zako zote za kufuli katika shelfu mojawapo ili kila kitu kiwe
kwenye ncha ya vidole vyako pale unapokihitaji. Hakikisha baadhi ya madawa na
blichi zinakuwa eneo la juu ambalo watoto wadogo hawawezi kufikia, kama vipi
weka loki kabisa.
Mahali pako pa kufulia pawe na mwanga wa kutosha. Mwanga
mwingi wa asili ni mzuri zaidi hasa wakati wa kufua kwa mkono na kunyoosha. Mwanga
pia unakuonyesha ndani ya mashine kukuridhisha kuwa hakuna nguo iliyosahaulika.
Sakafu inayofaa
bafuni na jikoni inafaa pia eneo la kufulia. Sakafu ya marumaru ni rahisi kusafisha,
haipitishi maji na ikitokea kumwagika haiharibiwi na blichi.
Kufua haitakiwi kuwa kazi ya kuchukiza. Weka mpangilio huu
mahali pako pa kufulia na kamwe
hutachukia mchakato mzima wa kufua na kunyoosha nguo.
Makala hii imeandaliwa
na Vivi O. Machange. Vivi ni mjasiriamali upande wa usafi wa magari, nguo na
mazulia; pia ana mapenzi makubwa ya mitindo na mapambo ya nyumbani. Kwa maoni
au maswali tuma kwenda 0755 200023 au viviobed@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment