Kupamba nyumba yako
ni zaidi ya kuchagua rangi za kuta na aina ya fenicha — unatakiwa pia
uchague rangi sahihi ya zulia.
Kuchagua rangi sahihi
za mazulia kwa ajili ya nyumba yako sio uamuzi mdogo, mazulia ambayo utakaa
nayo kwa miaka. Kwa ajili kuweka mazulia ni moja ya mapambo ya ndani
yanayogharimu zaidi kimuda na kipesa. Kwa mfano si busara kutandika zulia la
ukuta kwa ukuta ambalo unategemea kuondoa chini ya miaka mitatu. Kwanza si kazi
ya kitoto kuanza kutoa vitu ndani kwa ajili ya kutanzika zulia la aina hii, na
pili huwa zulia hili ni kubwa kwa hivyo pia ni gharama. Nimefanya mahojiana na
Bi Aisha Idd ambaye anauza mazulia ya nyumbani kutaka kujua mambo ya kuzingatia
kwa upande wa rangi wakati wa kununua mazulia ya nyumbani.
Bi Aisha anasema
michoro na rangi za mazulia zinabadilika kila wakati kwa hivyo kwa ajili
mazulia ni gharama, unatakiwa kuchagua yale ya rangi ambazo zitaoana na
muonekano wa sasa ama mipango ya baadaye kama ipo juu ya nyumba yako. “Kwa
kawaida rangi za mapambo ya sakafu huwa zinakuwa nyuma mwaka 1-2 kulinganisha
na zile rangi za mitindo ya nguo, anasema Bi Aisha” Hii ina maana kwamba rangi
maarufu zaidi kwenye maduka ya nguo za wanawake, zitaanza kuonekana kwenye sakafu
za nyumba miaka kadhaa mbele. Upo hapo!
Kwa mazulia ya
nyumbani ambazo zinaonekana zimepitwa na wakati kwa sasa ni rangi za dhahabu,
kijani, silva, damu ya mzee na rangi ya udongo. Rangi zisizokolea au kwa maneno
mengine rangi za mwanga kama vile bluu, khaki, kijivu na rangi ya maziwa
zinaonekana kuwa maarufu zaidi kwa sasa. Hata hivyo hakuna rangi ambayo
inashika kasi kwa sasa kama kijivu na khaki na wala haijalishi mabadiliko ya
mara kwa mara ya rangi hizi. Aisha anasema labda ni kutokana na kuwa kuna jinsi
nyingi ya kuoanisha rangi hizi mbili na vizulia vya kutupia.
Sasa basi wakati wa
kuchagua mazulia kwa ajili ya sakafu za nyumba yako zingatia mambo kadha wa
kadha. Bahati nzuri ni kuwa vizulia vile vya kutupia baadhi ya maeneo vinakuja
kwa bei, michoro na rangi lukuki ambapo ushindwe wewe tu. Kwa kweli sio ngumu
kupata ukubwa na rangi unazotaka kwa uwezo ulio nao. Siku zote kumbuka kuwa
uchaguzi wako wa mazulia ya nyubani kwa kila chumba ni msingi wa ladha yako.
Baadhi
ya dondoo zifuatatzo zitakusaidia kuchagua rangi sahihi ya mazulia ya kwenye vyumba
vya nyumba yako. Kwa kuwa zulia huwa ni la kudumu na kuweka la rangi fulani ni uamuzi wa gharama kufanya, hapa ni dondoo
chache za kukusaidia katika uamuzi huo mgumu.
Kwanza kabisa fahamu kuwa zulia ni moyo wa
nyumba yako. Linatoa utambulisho wako hasa lile la sebuleni. Kwa vile mnachukua
muda mwingi sebuleni kama familia, fikiria rangi ambayo inaenda kukubaliana na
mfumo wa maisha yenu. Je sebule yako ni rasmi au ni ya kujimwaya mwaya?
Kuamua ni mazulia ya rangi ipi ununue, fahamu ni kwa kiasi gani yatakanyagwa.
Zulia linavyozidi kukanyagwa ndivyo kuna uwezekano wa kuchafuka kwa maana ya
kumwagikiwa vimiminika vilivyobebwa na wapitaji, madoa na majasho ya miguu. Mazulia
ya rangi za mwanga kwa mfano khaki na kijivu huonyesha uchafu kirahisi lakini
yanaweza kusafishika kwa dawa za kuondoa madoa kwenye mazulia ila kama mazulia
yenyewe sio imara basi yataanza kuonyesha alama za uchakavu kwenye maeneo hayo
ukiliinganisha na mazulia ya rangi za giza. Kama una wanyama wa ndani au sakafu
ya nje ya nyumba isiyo ngumu ni rahisi mazulia yako kuchafuka kuliko yule
anayeishi kwenye nyumba yenye mazingira ya nje yaliyowekwa sakafu ngumu.
Familia nyingi haziweki zulia jikoni.
Fikiria matumizi ya eneo ambapo zulia litawekwa kabla ya kuamua rangi. Je
unataka zulia lilete mwanga ama lipunguze mwanga chumba ambacho kina mwanga
mkali zaidi? Nyekundu ni sahihi kwa vyumbani, sebuleni na kwenye ujia kwani haionyeshi
madoa kwa hasira kama rangi za mwanga. Ila kwa vyumba ambavyo vina kiasi
kikubwa cha mwanga wa jua fikiria juu ya zulia kuchuja, tatizo ambalo
linaonyesha sana kwenye zulia za rangi za giza.
Kuchagua rangi kunahusika sana na vitu
mbalimbali anbavyo vinahusika kwenye zulia hilo. Chagua rangi za giza kama kuna
watoto wadogo ili kuficha yale madoa yasiyoepukika. Kama una wanyama wa ndani
fikiria vitu kama tope wanaloweza kuingiza. Hata kama huhusiki na hivyo vyote
basi fikiria hata sherehe na wale wageni ambao kwa vyovyote vile hawatainama
kuvua viatu vyao!
Chagua rangi ya zulia itakayoendana na haiba na mazingira ya nyumbani
kwako. Kwa mfano, kuna familia ambazo kuna sebule rasmi kwa ajili ya wageni tu na
kuna nyingine ya familia. Hii rasmi
huenda kwa kawaida huwa na muonekano wa rangi za kifahari na rangi za mazulia yake
huwa ni moja kwa mfano zulia la sakafu yote ya sebule rasmi yaweza kuwa ya rangi
ya maziwa. Sasa kabla ya kuamua rangi ya zulia jiulize je unapenda kutembea
kwenye chumba ambacho zulia lake lote ni la rangi moja tena ya mwanga?
Rangi za zulia utakazochagua zinahusiana vip na rangi za kuta na mapambo
mengine hapo chumbani? Kila chumba kinahitaji sehemu moja ambayo ni kitovu.
Zulia lako linaweza kuwa ndio kitovu, hautaki zulia lishindane na mapambo yako
mengine kwa ajili chumba kinaweza kuonekana vurugu vurugu.
Shirikisha
wanafamilia na chukua kura! Kwa ajili wote mnaenda kutumia mazulia haya,
inaweza kuwa vyema kujua ni rangi zipi familia yako inaona zitafaa zaidi chumba
fulani. Lete sampo nyumbani mshauriane pamoja. Huenda ukagundua rangi ambayo haukuwa
umeiwaza mwanzo.
No comments:
Post a Comment