Mambo
ya kuzingatia kabla ya kununua kaunta za jiko
Kaunta za jiko zinahusika mno katika
muonekano wa chumba hicho, lakini pia ni kwa umuhimu mkubwa wa kuwa na sehemu
ya kufanyia kazi. Kaunta nzuri zinatakiwa ziwe imara, kuweza kuhimili matumizi
ya kila siku, kumwagikiwa na vitu na kuhimili mgusano na vyombo vya kupikia vyenye
moto kuwekwa juu yake.
Ukiondoa sakafu, kaunta ya jiko ni
sehemu inayotumika zaidi ndani ya nyumba. Ni sehemu tunayoandalia chakula,
tunayoweka funguo, barua na bili zilizoingia nyumbani na hata wakati mwingine
tunaweka hapo magazeti. Hatuwezi kukataa umuhimu wake hasa kwa matumizi. Hata
hivyo kwa ajili ni kitovu basi, muonekano wa kishirika na vifaa vingine hapo jikoni
kama makabati, jokofu, jiko na sakafu unahusu. Lakini ni kaunta zako za jikoni
ndio zinakuwa kipaumbele kwa ajili ni eneo ambalo macho yanaelekea moja kwa
moja.
Kabla ya kununua kaunta za jiko
hatua ya kwanza ni kufanya utafiti. Kuna aina lukuki sokoni kwa maana ya
mitindo na vifaa vilivyotengenezea, kwa hiyo chukua muda wako kuchunguza aina
mbalimbali. Kila aina inawakilisha faida na hasara, kwa hivyo sio vyema
kukurupuka.
Kama ni swala la umaridadi au
uimara, utunzaji au gharama, kila vifaa vilivyotengenezea kaunta vina faida na
hasara zake. Nunua kaunta inayokubaliana na mahitaji yako kwa maana ya staili
na matumizi.
Kujifunza jinsi ya kununua kaunta ya jiko ni mchakato muhimu pale unapojenga au
kurekebisha chumba cha jiko. Kaunta sahihi itakubaliana na bajeti yako , mtindo
wako wa maisha na muonekano wa mapambo yako ya ndani.
Zifuatazo ni baadhi ya aina za vifaa
vinavyotengenezea kaunta za jiko kama zinavyoelezewa na mtaalamu wa maboresho
ya nyumbani Bwana Deo Minja. Na anaelezea faida na hasara ya kila aina.
Marble ni jiwe muhimu
la asili linalotumika kwa wingi kutengenezea kaunta za jiko. Jiwe hili kiasili lina
michoro mbalimbali inayolipa jiko kiwango na hisia za asili. Hata siku moja
kaunta ya aina hii haikuangushi jikoni. Utunzaji wake na usafishaji ni rahisi
ila unashauriwa kutokata vyakula kwa kisu juu ya marble moja kwa moja kwani inaweza kukwaruzika hivyo kuharibu
muonekano. Kaunta hizi ni laini, rahisi kusafishika na haipitishi maji wala
joto. Ukitembelea kwenye kila nyumba zenye majiko la kisasa, nyingi zitakuwa na
kauta za jiko za aina ya marble.
Jiwe lingine maarufu kwa ajili ya kutengenezea kauta
za jiko ni granite. Jiwe hili
linafanya jiko lionekane la kifahari na huwa linakuja kwa rangi zaidi ya 3000,
anasema Minja. Linadumu maisha ni ni la pili kwa ugumu baada ya almasi. Changamoto
yake kubwa ni kuwa ni gharama kubwa
Kaunta
za jiko za marumaru ni imara na rahisi kusafishika. Marumaru kwa kawaida
inaongeza uhai wa mahali. Pia sio gharama na kuna aina na rangi mbalimbali kwa
nyumba za kawaida. Changamoto yake ni kuwa kwa vile zile marumaru ni kipande
vidogodogo vinavyounganishwa pamoja, basi wakati mwingine kaunta inakosa levo
na pia ni rahisi kuwa na mipasuko na ile grout
inayowekwa katikati ya mistari huwa inashika uchafu kirahisi mno
Kaunta
nyingine za jiko ni zile za kujaladia kwa mfano formica. Ziumetengenezwa kwa vifaa vya plastiki vyenye sehemu ya
juu laini ambayo inakuwa rahsi
kusafisha. Faida yake ni kwamba ni bei rahisi na zipo za rangi mbalimbali.
Hasara yake ni kuwa mikwaruzo na mipasuko hairekebishiki.
Kaunta za mbao zinaleta muonekano mzuri na zipo za
mitindo na rangi mabalimbali. Mbao ngumu kama vile mkongo na mninga ndio
zinazotumiaka zaidi kwa ajili ya kaunta. Ni rahisi kusafisha na changamoto yake
ni kuwa zinahitajika kufanyiwa maboresho ya mara kwa mara. Ubaya wa kaunta za
mbao ni kuwa zinaharibiwa na maji na baada ya muda zinashika madoa.
Kaunta za chuma kisichoshika kutu kwa jiko lako
nacho ni chaguo zuri. Zinahimili joto na ni imara. Na kwa sababu zinajengewa
kwa matakwa yako inawezekana pasionekane viungio vyovyote kwenye kaunta yako. Zinafaa
kuwekea sufuria za moto na ni rahisi kusafishika. Changamoto yake ni kuwa zina
kelele, zinaweza kubonyea na huwezi kukatia juu yake.
Kama
una chumba cha jiko chenye umbo lisilo
la kawaida hasa kona, zege inaweza kuwa chaguo zuri kwa ajili ya kaunta za jiko
lako. Faida zake ni kwamba zinahimili joto na mikwaruzo. Na hazihitaji utunzaji
kivile, zinaweza kuwekwa rangi na urembo wa aina mbalimbali ila changamoto yake
ni kuwa kama tunavyojua zege ni saruji
kwa hivyo nyufa zinaweza kutokea na ule muonekano wa zege chumba kinaonekana
kama cha kiwandani zaidi.
Baada ya kujua aina zote hizi za vifaa vya
kutengenezea kaunta za jiko kama tulivyoelezwa na Bwana Minja kifuatacho ni kuangalia
bajeti yako. Bajeti ndio kikwazo namba moja kwenye kuchagua kaunta za jiko. Kwa
mfano kaunta za granite na marble zinaweza kuwa gharama mara 3
zaidi ya zile za kujaladia.
Jambo la pili la kuzingatia kabla ya kunua vifaa
vyako vya kujengea kaunta za jiko ni umaridadi. Kaunta zote zinatakiwa zitimize
lengo la msingi ambalo ni kuweza kuwa na eneo la kufanyia kazi wakati wa
kuandaa chakula, hata hivyo kuna upande wa umaridadi. Kama huna uhakika wa
muonekano wa kaunta unayotaka basi angalia maeneo mengine ya jiko kama vile makabati
ili kuweza kuleta uwiano na kaunta.
Jambo la tatu na kubwa kuliko ni kuamua sasa kununua
kifaa cha aina hii ili kutengenezea kaunta za jiko lako. Gharama, uimara na
muonekano unatofautiana kwa kila aina ya vifaa vya kutengnezea kaunta.
Haijalishi
ni aina gani ya kaunta ya jiko utakayoamua kuweka nyumbani kwako, mara zote
hakikisha kuwa unapitia kwa mtaalam. Inatatiza, inakula muda, na kama nia yako
kuu ni kufanya eneo hili lionekane maridadi wakati huo huo likitumika, unataka
kuwa na uhakika wa usimikaji sahihi.
Makala hii imeandaliwa na Vivi O.
Machange. Vivi ni mjasiriamali upande wa usafi wa nguo, mazulia na magari;
pia ana mapenzi makubwa juu ya muonekano wa nyumba. Kwa maoni au maswali tuma
kwenda 0755 200023 au viviobed@yahoo.co.uk