Thursday, June 5, 2014

my article for newspaper: bustani za kwenye vyungu

Mwongozo wa bustani za maua za kwenye vyungu
Hata kama una eneo dogo kiasi gani lakini unapenda bustani za maua, unaweza ukatimiza tamanio lako hilo kwa kutengeneza bustani za maua za kwenye vyungu.
Au pengine labda una eneo la kutosha kuwa na bustani ya ardhini lakini bado kuna yale maeneo kama ukutani, ndani ya nyumba au kwenye varanda ambapo ungependa kuwa na maua, basi suluhisho ni bustani za kwenye vyungu.

Bustani hizi zinakuwezesha kutengeneza bustani maalum kwa ajili ya eneo lolote. Unaweza kuotesha humo maua yako ya upendeleo ambayo usingependa kuotesha kwenye eneo kubwa la bustani ya ardhini kwani labda yatamezwa na mimea mingine iliyopo kwenye bustani husika. Mtunza bustani wa bustani za kwenye vyungu kikomo chake ni ubunifu wake pekee, anasema landscaper Aisha Idd.

Kwenye makala hii bi Aisha atatufunza jinsi ya kuchagua vyombo vya kuoteshea, uwekaji wa mbolea, udongo na umwagiliaji wa bustani zako bila kusahau maua yanayofaa kuotesha kwenye vyungu na mengine mengi!
Baadhi ya vyombo vinavyoweza kutumika kwenye bustani za kwenye vyungu ni vyungu vidogo vya kuning’iniza na vile vikubwa vya kuweka chini pamoja na maboksi ya mbao.                                                                                                                                       

Aisha anatupa mwongozo wa namna ya kuchagua vyungu kwa ajili ya bustani yako hiyo. Anasema epuka vyungu vyenye midomo myembamba. Pia vyungu vya plastiki nyembamba sana vinaweza kuharibiwa na jua na vitafanya ua lililoko ndani kukaukiwa na maji mara kwa mara. Kama utachagua vyungu vya udongo fahamu kuwa udongo unapitisha maji hivyo kiasi cha mji kitakuwa kinapotea kupitia kuta za chungu. Vyungu vya seramiki na saruji ndio vizuri zaidi kwenye kuhifadhi maji ila vinatakiwa kuwa na matundu kadhaa.                                                                                                                                    

Maboksi ya mbao huenda yakaoza, mbao nyekundu na za aina ya cedar huwa haziozi na zinaweza kutumika bila tatizo. Maboksi ya mbao zilizowekwa dawa ya kuzuia kuoza au kuliwa na wadudu si mazuri kwani kemikali zlizopo kwenye dawa hizo huwa zinaweza kuunguza maua. Uzuri wa mabokisi ya mbao ya kuoteshea maua ni kuwa yanaweza kutengenezwa kwa umbo na ukubwa utakaofiti eneo linalohitajika kuwekwa.

Vyungu viwe na ukubwa wa wastani kwani vikiwa vidogo sana vitazuia mizizi ya mmea kutambaa vizuri na pia huwa vinakauka maji mapema sana. Ukubwa na idadi ya mimea inayooteshwa itatokana na ukubwa wa chungu kitakachotumika. Maua yenye mizizi inayoenda chini inahitaji vyungu virefu. Hakikisha kuwa vyungu vyako vinapitisha maji vizuri na tandika magazeti chini ili kuzuia udongo usiwe unakimbia chungu wakati wa kukimwagilia. Sasa utajiuliza hayo magazeti si yataloa? Ni kweli ila hata kama yakiloa yatatengeneza kizuizi chini kwani hama tujuavyo ni kuwa karatasi haiozi. Kwa upande wa vyungu vidogo vya kuning’iniza hakikisha ya kuwa hutundiki kwenye ukuta wenye jua la moja kwa moja kwani vitakuwa vinakaukiwa maji mara kwa mara.

Hakikisha kuwa chombo chako cha kuoteshea bustani za kwenye vyungu kinapitisha maji mapema lakini kinahifadhi unyevu wa kutosha kuweka mizizi katika hali ya maji. Mboji inafanya udongo mzuri sana wa kwenye vyungu. Ila ni muhimu kujua hitaji la mmea kwani usijezidisha udongo wenye mbolea kali, na pia mbolea nyingine kama ya kuku ina tindikali sana kwahivyo inahitaji maji kwa wingi pindi unapoiweka. Kadri utakavyokuwa unamwagilia mmea wako ndivyo utkavyokuwa unaweka mbolea kwani huwa maji yanaondoa baadhi ya vimeng’enyo. Pia kuna mbolea za dukani za maji maji ambazo waweza tumia kwa kupata maelezo ya kitaalam toka kwa wauzaji.

Umwagiliaji wa bustani yako ya kwenye vyungu ufanyike pale mmea unapohitaji maji kwa maana ya ikiwa dalili za hali ya kunyong’onyea zitaanza kujitokeza. Baadhi ya mimea inaweza kuvumilia na inahitaji ukame kiasi kwamba ukiimwagilia mara kwa mara unaisababishia kuwa na unyevu wakati wote kwa maana hiyo itakufa. Ielewe mimea uliyo nayo, anasema Aisha. Kuna mimea mingine ya kwenye vyungu kwa mfano, kama iko ndani ya nyumba inaweza kumwagiliwa vikombe viwili tu kwa juma zima. Kumwagilia kuwe ni hitaji na sio jambo la kila wakati na kanuni kuu ya kujua kuwa mmea unahitaji maji ni kujaribu udongo wake. Kama inchi moja au zaidi ya udongo ni mkavu basi mwagilia.

Kwenye mazingira ya uwazi, mimea ya kwenye vyungu inapoteza maji mapema. Wakati wa kiangazi bustani zilizowekwa kwenye mazingira haya huenda zikahitaji kumwagiliwa kila siku.   Sasa basi, ni muhimu kufahamu kuwa sio kila maua au mmea unafaa kuoteshwa kwenye vyungu. Mimea inayokubalika zaidi kwa bustani hizi ni ile yenye mizizi michache na mifupi. Pindi uendapo kwenye bustani za wauza maua zilizojaa maeneo mengi kando kando ya barabara kuu watakufahamisha.                             

Umaarufu wa bustani za kwenye vyungu umetisha.

Mimea kwenye vyungu inaonekana kila mahali, kutoka kwenye makazi ya watu hadi maofisini, mahotelini, kwenye ma mall na hata barabarani. Udongo mbaya au hakuna eneo la kuweka bustani sio kisingizio tena cha kutokuweza kufurahia kijiraha cha kuwa na bustani!

Makala hii imeandaliwa na Vivi Machange ambaye ana mapenzi makubwa juu ya muonekano wa makazi. Kwa maoni au maswali tuma kwenda 0755 200023 au viviobed@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment