Thursday, June 12, 2014

my article for newspaper: jinsi ya kutunza na kusafisha godoro

Kila mmoja anapenda usingizi wake, na tunategemea godoro kutupatia mahali safi na nyororo pa kulala. Ni nini kinafanyika pale godoro lako linapokuwa chafu? Ni kwa namna gani unazuia mavumbi na wadudu kuweka makao kwenye godoro lako na kukubughudhi na usingizi wako? Ni ratiba gani ya matunzo na usafi godoro inahitaji?

Kama inavyofahamika kwamba binadamu anatumia theluthi moja ya maisha yake akiwa amelaza mwili mlalo na tena wengi wetu juu ya godoro, basi ungetegemea kwamba kusafisha godoro ingekuwa ni orodha namba moja kati ya vitu vinavyopewa kipaumbele kwenye orodha ya kusafisha, lakini utashangaa wala siyo. Ni mara chache tunafikiria juu ya kusafisha godoro.

Tatizo ni kuwa, unaondoa shuka zote, unabakiwa na godoro ambalo limeshionewa foronya ambayo huwezi kuivua sio – kama vile kuna zipu unayoweza tu ukafungua kirahisi ukavua foronya na kwenda kuifua – hapana, ukweli wa masikitiko ni kuwa – wakati tunatoa shuka zote, tunakuwa kama tumeziba macho kwa uchafu mwingine wowote uliopo juu ya godoro lenyewe.

Godoro linaweza kuhifadhi uchafu wa vimiminika, madoa, vumbi na mbaya zaidi hata wadudu kama chawa na kunguni  – kwahivyo kuwa na godoro safi ni muhimu kwa sababu kadhaa zaidi ya kufahamu kuwa mwili ambao umevalishwa nusu unalilalia kukiwa na shuka pekee iliyotenganisha mwili huo na godoro.

Kusafisha godoro kwa mashine ya kunyonya vumbi ni muhimu kwa ajili ya kuondoa vumbi, seli za ngozi zilizokufa na uchafu mwingine unaotua kwenye godoro lako na ambao unajilimbikiza kadri muda unavyokwenda. Fikiria kusafisha godoro kwa namna hii kwa walau mara mbili kwa mwaka. Sasa kumbuka kuwa kwa vile mashine hii ya kusafishia kwa upepo ina vichwa kadhaa, utapaswa kutumia kile kichwa cha kusafishia viti na sio kile cha kawaida cha kusafishia zulia kwa huwa kinazoa kila aina ya uchafu kwa hivyo usingependa kukipitisha hicho kwenye godoro lako. Wakati wa kusafisha godoro ni vyema kusafisha pia mvunguni.

Vile vile kila baada ya miezi sita iwe ni wakati wa kugeuza godoro lako juu kwenda chini na miguuni kwenda kichwani. Fikiria kwa mfano mwenzi wako na wewe mna zaidi ya kilo mia, kwa hivyo kwa kugeuza na kuzungusha godoro inamaanisha kuwa mnaongeza uhai wake na kuleta uwiano wa uchakavu . Kulingana na ukubwa wa godoro, hii kwa kirahisi kabisa inaweza kuwa kazi ya watu wawili.

Madoa kama ya mapatapishi, jasho, damu, mkojo na vimiminika vingine toka mwilini huwa kuna wakati vinatua kwenye godoro. Kama ilivyo ada kwa doa lolote, ni vyema kulichangamkia liondoke mapema kabla halijakomaa zaidi. Madoa ya vimiminika yanatakiwa kwanza yafutwe kwa maji baridi, na kitambaa chenye unyevu. Na baadaye unyevu wa ziada unakaushwa na kitambaa kikavu. Kumbuka kufuta kwa kukandamiza badala ya kuzungusha mduara ili kuondoa uwezekano wa kuchana kitambaa cha godoro. Madoa haya ya viminika toka mwilini asili yake ni protini kwa hivyo tumia maji ya baridi pekee wakati wa kuondoa madoa haya.

Funika godoro lako kwa foronya ya kuvulika ili kulinda maeneo ya godoro. Chagua foronya ambayo inaosheka kirahisi ambayo ni rahisi kuvalisha na kuvua kwenye godoro lako. Foronya nyingine zimebuniwa maalum kwa kazi ya kuzuia kushika vumbi kwa hivyo kukupunguzia kazi ya kunyonya godoro vumbi mara kwa mara.

Kama maeneo ya godoro yamepatwa na tope au udongo ondoa kwa shampoo ya kusafishia sofa na mazulia. Safisha tu lile eneo lililochafuka kwa kutumia sponji. Suuza eneo hilo kwa sponji jingine la maji ya moto na kandamiza eneo hilo kwa kitambaa kikavu ili kunyonya unyevu. Unaweza kuruhusu eneo hilo kukauka kwa kuwasha feni au hata kutoa godoro nje kwenye jua kali. Usiruhusu maji kuzama sana ndani kwenye kiini cha godoro kwani maji na godoro sio marafiki.

Endapo godoro litakuwa makazi ya wadudu kama chawa na kunguni jambo hili si dogo eti wadudu hawa waondolewe tu na watu hapo nyumbani ambao sio wataalam wa kazi hii. Changamka mapema na mwite mtaalam. Watakusafishia na kupuliza dawa godoro lako chumba, na hata maeneo mengine ya makazi yako ambayo yatakuwa yamedhurika na wadudu hawa. Kama umefikiwa na wadudu hawa unataka waondoke na wataalam wanajua jinsi ya kufanya kazi yao.

Hongera kwa kuwa na dogoro safi ambalo litadumu muda mrefu!


Makala hii imeandaliwa na Vivi Machange ambaye ana mapenzi makubwa juu ya muonekano wa makazi. Kwa maoni au maswali tuma kwenda 0755 200023 au christines.daughter@yahoo.com

No comments:

Post a Comment