Thursday, November 20, 2014

my article for newspaper: jinsi ya kupamba bedroom

Jinsi ya kupamba chumba cha kulala

Kwa nyumba nyingi chumba cha kulala ni chumba binafsi zaidi. Ni chumba pia ambacho kina vitu vingi zaidi binafsi. Kinaweza kuwa kama kiota cha mahaba au mahali patakatifu pa kulala na kupumzika. Pia kinaweza kuwa chumba cha kuchangamka na kutuliza kwa watoto, kwa jinsi wanavyokuwa wakigundua kuwa wanamiliki chumba chao wenyewe.
Kupenda kufurahisha marafiki, majirani na wageni; wenye nyumba wengi wanamalizia nguvu zao kupamba vile vyumba vya kuonekana na hadhara ndani ya nyumba. Umefika wakati wa kuwa mchoyo na kuelekeza nguvu zako kwenye chumba cha kulala. Juu ya yote ni kuwa kabla ya kuoga kujiaandaa kutoka ni lazima kwanza utokee kitandani.
Kwanza kabisa anza na kitanda kwa ajii kitovu cha chumba chochote cha kulala ni kitanda. Ni wazi kuwa kitu cha kwanza cha kuzingatia kwenye kitanda itakuwa ni godoro, lakini usisahau ubao wa kichwani. Ni ngumu kudharau umuhimu wa sababu za kisaikolojia katika kupata usingizi mwororo. Hisia na hata muonekano wa kitanda chako wakati unapoingia humo inaweza kuelezea ni namna gani unavyojisikia wakati unapotoka humo.
Kwa upande wa sakafu chaguo zuri zaidi kwa ajili ya chumba cha kulala ni zulia na mara zote imekuwa hivyo. Hamna kitu kizuri kama kuamka na kuweka miguu yako kwenye sakafu ambayo inaelekea kuwa na hisia kama za kitandani kwa kupata joto lile lile mithili ya la kitandani. Wengine hupenda kuweka sakafu za marumaru na mbao lakini eneo la pembeni mwa kitanda wengi wanapenda kuweka zulia.
Wazo la mwanga katika chumba cha kulala kwa baadhi linadharauliwa. Taa zisizokuwa na maridadi na balbu za juu ya kichwa tu zimeanza kupoteza mvuto kwenye chumba cha kulala cha kisasa. Taa za vivuli za kuweka juu ya vimeza vya kando mwa kitanda na za ukutani za maridadi ndio zinaendana na wakati kwa chumba cha kulala, kwa ajili ya mwanga wa chumba hiki kwa matumizi ya wakati wowote iwe ni mchana, jioni au usiku. Taa ndogo zinaweza kuwekwa kwa ajili ya kutumia muda maalum ambapo hutaki kuwasha taa zote kwa mfano wakati wa kusoma au kushikisha kifungo.

Kwa vyumba vidogo vya kulala mara nyingi vinafaidika na uwepo na makabati ya nguo, madroo na shelfu kwa kusaidia kuhifadhi na kuweka mpangilio. Baadhi ya vitu vidogo dogo na nguo vinapoukuwa vimewekwa kwenye sehemu hizi za kuhifadhia, chumba kinaonekana nadhifu.

Mara nyingi rangi za mwanga  zinashauriwa zaidi kwenye chumba cha kulala kwa ajili zinaleta hisia ya mapumziko. Rangi za vitambaa vya malazi viendane na rangi nyingine hapo chumbani na hata zile za samani. Shuka za rangi na maua ya kuvutia zinunuliwe ili kuongeza uzuri wa chumba.
Komfota lenye rangi nzito litaendana na samani au ubao wa kichwani wa mbao. Hii pia ni kweli kwa mapazia.

Wakati huo huo kumbuka kuweka samani zenye ukubwa na wingi wa kuendana na ukubwa wa chumba. Kabla hujanunua samani hizo ni vyema kwanza kufahamu mpangilio wa sakafu na ukubwa uliopo.

Kutengeneza bajeti ni muhimu kwa mradi wowote wa maboresho ya nyumbani. Kujipa wastani wa gharama inayohitajika itakusaidia kuamua ni nini kinachoweza kufanyika na kipi si kipaumbele. Baadhi ya shughuli kwenye mradi huu unaweza kufanya mwenyewe, kwa baadhi itakubidi utafute mtaalam. Kama kipaumbele chako ni ukuta kwa mfano, basi unaweza kutafuta mtalam wa rangi akapaka, ilihali ukitandika zulia mwenyewe. Vyovyote utakavyoamua, ni wakati wa kufanya chumba chako kuwa chako tena.

Kupamba chumba cha kulala ni shughuli mojawapo ya maboresho ya nyumbani ambayo inaweza kuhuisha tena afya yako na mahali unapoishi.


Makala hii imeandaliwa na Vivi Machange ambaye ana mapenzi makubwa juu ya muonekano wa makazi na pia ni mjasiriamali wa usafi wa magari, mazulia na nguo. Kwa maoni au maswali tuma kwenda 0755 200023 au christines.daughter@yahoo.com

No comments:

Post a Comment