TANZANIA inaongoza kwa kuwa na wakimbizi wengi barani Afrika ambapo
inakadiriwa kwa sasa wapo 70,000 ikifuatiwa na Rwanda yenye wakimbizi 26,000.
Aidha,
Jimbo la Kivu Kusini katika Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Kongo ni la tatu likiwa na wakimbizi 9,000.
Inakadiriwa kuwa zaidi ya wakimbizi 105,000 walikimbia
nchini Burundi na kwenda kutafuta hifadhi nchi jirani kutokana na mgogoro wa
kisiasa unaoendelea nchini humo.
Hayo yalibainishwa na Mkuu wa Shirika la Kimataifa la
Uhamiaji (IOM) nchini Tanzania, Damien Thuriaux.
Alisema, IOM kwa kushirikiana na Serikali za mikoa nchini
pamoja na Umoja wa Mataifa wamefanikiwa
kuwaokoa wakimbizi wapatao 50,000 toka nchini Burundi waliokuwa katika kijiji
kidogo cha Kagunga mpakani mwa Tanzania na Burundi.
Alisema, wakimbizi hao walikuwa wakichukuliwa katika
kijiji hicho kwa usafiri wa mashua upande wa Tanzania, Ziwa Tanganyika ambapo
mashua mbili zilikuwa zikibeba wakimbizi 600 kila siku na kusafiri umbali wa
kilomita 60 kutoka Kagunga hadi Kigoma.
Sehemu ambayo wakimbizi 1,500 hukimbia kila siku kutoka
Burundi kutokana na ghasia za kisiasa zinazoendelea.
Alisema, baadhi ya wakimbizi wamekuwa wakitembea umbali
wa kilomita 170 na kufika kambi ya wakimbizi ya Nyarugusu ambapo IOM na
washirika wake wamekuwa wakitoa misaada ya usafiri wa mabasi na malori.
Alisema, katika zoezi hilo wameweza kusaidiwa na serikali
ya Tanzania.
"Mchakato unaoendelea sasa ni kuendelea kutoa
misaada ya kibinadamu kwa wakimbizi hao, kwa kuwa sasa kuna msongamano mkubwa
wa wakimbizi katika Kijiji cha Kagunga, ambapo wakimbizi wanasubiri usafiri wa
mashua ili waweze kutoka na kuingia nchini Tanzania," alisema.
Alisema, watu 1,500 kuhamishwa kila siku kwa kutumia
mashua ni idadi kubwa ambayo inaweza kuchukua zaidi ya mwezi mzima kuwaokoa
wakimbizi hao.
MAJIRA
PICHA: RFI
No comments:
Post a Comment