Umuhimu wa kujali
ubora wakati wa kununua marumaru za bafuni
Bila
shaka kila mmoja anataka apate bidhaa au huduma kwa thamani ya hela aliyotoa
wakati wa ujenzi wa nyumba yake, lakini chaguo la marumaru za bafuni inahitaji
kuwa makini zaidi ya hilo. Katika makala hii nitakuwa na Mhandisi David ambaye
atatujuza umuhimu wa kuzingatia ubora zaidi ya gharama wakati wa kununua
marumaru za bafuni.
Unaweza
kuwa umepata marumaru za bei nafuu, lakini zisizokuwa na kiwango. Marumaru za
aina hii zitakugharimu kwa kiasi kikubwa muda wote utakaokuwa unaishi kwenye
nyumba yako hiyo.
Linapokuja
swala la marumaru za bafuni, malighafi, rangi, uimara, mtelezo, na usimikaji ni
mambo muhimu zaidi ya kuzingatia, anasema David. Hakikisha kuwa unapata ushauri
kwa fundi mwenye uwezo kabla ya kufikia kufanya uamuzi.
Marumaru
za bafuni zipo za kuanzia maumbo madogo zenye nyongeza ya border za aina na michoro mbalimbali. Wajenzi wanatafuta marumaru
za maumbo tofauti tofauti kutoka umbo la
pembe nne lililozoeleka hadi malighafi nyingine kama mawe ya asili na vioo. Wanapenda
pia mabafu yao yawe na muonekano wa kazi
za sanaa zaidi, anasema David. Ila marumaru za bafuni zinafanya kazi kubwa,
zinatakiwa kufanya mvuke usisambae vyumba vingine na kulinda kuta zisiharibiwe
na ukungu na hali ya umajimaji. Zinatakiwa zizibwe vyema na grout maeneo ya miungio na ziwe na
usalama kutembea juu yake zinapowkuwa zimeloa, anasema mhandishi.
Pamoja
na mawe ya asili, marumaru bado zitabaki kuwa chaguo maarufu zaidi kwa ajili ya
kuta na sakafu za bafuni. Marumaru ngumu zina rangi sawa kwenye unene wake
wote, ingawa zina gharama zaidi, na hapa ndipo mnunuzi anapopaswa kuwa makini.
Ujue kutofautisha kama unanunua marumaru zilizopakwa rangi kwa juu tu, na hizi
ni zile nyepesi na bei yake iko chini. Aina hii ni kuwa baada ya muda si mrefu
rangi inatoka kutokana na kukanyagwa mara kwa mara, kwa kuwa rangi imepakwa
kwenye eneo la juu la marumaru kwa unene kiasi tu na sio unene wote. Hizi
zilizopakwa rangi inakuwa eneo la juu tu mfano barafu kwenye mlima au kwenye
keki! Hizi za aina hii zinafaa zaidi kwa mapambo pengine kutengenezea ua la
ukutani lakini sio kwa kuhimili shurba za sakafu ya bafuni. Marumaru ambazo zina rangi hiyo hiyo hadi ndani kwenye
kiini na unene wote wa marumaru ni imara zaidi kwa matumizi ya sakafu ya bafuni.
Kwa
hivyo muhimu zaidi ni kutumia marumaru hizi ngumu zenye rangi sawa kila mahali
kwa ajili ya sakafu na kuchagua za bei rahisi zinazoendana na zile ngumu kwa
ajili ya ukuta, anasema David. Usimikaji wa marumaru ni kazi ya sanaa kwahivyo
inahitaji fundi mwenye uwezo nayo.
Zaidi
ya kuweka marumaru bafuni unaweza kuweka pia jiwe la asili kama vile marble lakini iliyo ngumu. Ubora wa jiwe
na usimikaji wake ni muhimu sana. Uwekaji wa jiwe la asili ni wa kitaalam.
Kunaweza kuwa na shida ya kufitisha slabu kubwa ya jiwe hilo kwenye maeneo ya
kutolea maji machafu na kuingiza maji safi, na muhimu zaidi ya yote sio kila jiwe la asili
linafaa kwenye mazingira ya mvuke na majimaji ya bafuni, anasema mhandisi. Mawe
mengine ya asili yananyonya maji na mwishowe kuwa na mipasuko.
Marumaru zitaongeza
thamaini ya nyumba yako, kwahivyo kuwa tayari kutumia muda na pesa. Kwa bafu la
kisasa na muonekno wa kifahari chagua marumaru zenye rangi za mwanga kama vile
nyeupe ukutani huku ukiweka miisho na mpangilio fulani wenye mvuto kwa baadhi ya maeneo ya ukuta.
Haijalishi
ni mtindo gani wa marumaru utakaochagua kwa ajili ya bafu lako, zingatia ubora
na usimikaji wa kitaalam kabla ya kufanya maamuzi yoyote. Dondoo muhimu kuliko
zote, kabla hujaanza kutengeneza bafu lako angalia thamani ya nyumba yako. Ubora
wa bafu uendane na thamani ya nyumba. Kwa kuzingatia hilo utafanya uamuzi
sahihi kwa kushirikisha wataalam watakaokufanya usijutie maamuzi yako hapo
baadaye.
Makala hii
imeandaliwa na Vivi Machange ambaye ana mapenzi makubwa juu ya muonekano wa
makazi na pia ni mjasiriamali wa usafi wa magari, mazulia na nguo. Kwa maoni au
maswali tuma kwenda 0755 200023 au christines.daughter@yahoo.com
No comments:
Post a Comment