Zingatia haya
kabla ya kununua fenicha za nje ya nyumba
Fenicha
za nje ya nyumba pia zinajulikana kama fenicha za kwenye bustani au varanda. Aina hii ya fenicha huwa imetengenezwa kwa
malighafi inayozuia maji kupenya, kwa kuwa ni kwa ajili ya matumizi ya nje.
Fenicha za nje ya nyumba zimekuwa
zikitumika toka enzi za himaya ya Roma.
Fenicha
za nje ya nyumba ni muhimu kwa mikutano
wakati unapokuwa na kikundi cha watu kwa ajili ya siku maalum kama vile siku ya
kuzaliwa na kadhalika. Hakuna kinachofurahisha zaidi kama kuwa na kiusingizi
kwenye upepo mwanana wa kwenye varanda au bustani. Kuwa na chakula cha usiku na
mwenzi wako wakati nyota ziking’aa angani inakuwa ni mahaba zaidi ya ndani ya
nyumba.
Ila
kuna jambo linalofanya aina hii ya fenicha kuwa tofauti na zile za ndani;
malighafi ya fenicha za nje ya nyumba ni lazima iwe imara kwa sababu fenicha zitapambana
na mvua kubwa, jua kali, upepo na baridi kali. Je hali ya hewa ya unapoishi ni
joto na ukame, au unaishi karibia na pwani? Mvua ni za mara kwa mara? Haya yote
ni maswali muhimu ya kupatikana majibu kabla ya kununua fenicha za nje ya
nyumba. Hapa ni sababu, hali ya joto na ukame inafanya mbao kupasuka. Upepo
mkali unaweza kufanya fenicha za aluminiam zipeperushwe.
Ndio
maana ni muhimu sana kuhakikisha kuwa fenicha unazotumia kwenye mazingira ya
nje ya nyumba ni sahihi kwa matumizi hayo.
Kwa
malighafi, fenicha nyingi za kutumia nje ya nyumba zimetengenezwa kwa plastiki,
mbao aluminiam na chuma cha pua. Amua ni malighafi ya aina gani unataka kwa
ajili ya fenicha zako za nje. Vitu vitatu ambavyo vitakusaidia kuamua ni hali
ya hewa, utunzaji na muonekano.
Baadhi ya
malighafi kama vile aluminiam hazihitaji utunzaji wa kina. Chuma cha pua
kinaweza kudumu kwa muda mrefu sana na kinamudu joto na unyevu. Hapa
ni muhimu kufahamu kuwa fenicha za nje za mbao sio imara kama nyingine, kwa
hivyo inatakiwa kuziweka dawa mara kwa mara, anasema mseremala Rajab Hamis.
Fenicha za nje ya nyumba
zinakusaidia kuongeza ukubwa wa makazi yako, unapata eneo zaidi la kupumzika
hasa wakati ule ambao jua sio kali sana au mvua sio nyingi. Kwa hivyo fenicha
hizi zinakamilisha ahadi ya mapumziko, burudani na raha kwa ujumla. Uchaguzi wa
fenicha za nje unazingatia hatua zilezile za kununua fenicha za ndani. Japo
kunahitajika umakini wa ziada kwa ajili ya tofauti kati ya fenicha hizi mbili.
Fikiria ni eneo kiasi gani ulilonalo
na lina umbo la namna gani. Je ni varanda ndefu na nyembamba au ni fupi pana? Tumia
eneo na umbo la varanda au bustani yako kufahamu ukubwa wa fenicha zako za nje.
Hakikisha unaacha nafasi ya kutosha kati ya fenicha zako ili uweze kupishana
kirahisi. Tumia utaratibu ule ule wa kupanga fenicha za ndani. Kwa eneo dogo
meza za ukubwa wa kwenye mgahawa na stuli zitafaa zaidi kwani zitachukua nafasi
ndogo.
Ni wapi
utakapoweka fenicha zako za nje, je kwenye bustani yako kuna eneo la kukaa
ambalo lina paa? Na pia je fenicha zako zitakaa juu ya sakafu laini ya udongo
na majani au zitakaa juu ya sakafu ngumu? Hii itakusaidia kuchagua malighafi ambayo
itaoana na mazingira yako.
Hakikisha
kuwa ukikalia fenicha zako unapumzika vyema. Hata kama viti haviji na mito unaweza
kutengenezesha mito yako mwenyewe na uwe unaihifadhi ndani majira ambayo
hutumii fenicha za nje. Jaribu fenicha za nje kabla ya
kununua na hata kuzilaza kwa jinsi ambayo ungetaka viwe kama vitanda vya
mchana.
Yote hayo yakiwa yameshasemwa bajeti
yako ndio itaamua ni nini unachoweza kununua. Siwezi nikasisitiza ni kwa namna
gani ni muhimu kununua fenicha imara zaidi unazoweza kumudu. Kama uchumi
unagomba, bado kuna namna unayoweza kupata fenicha za nje zilizo imara kwa hela
uliyonayo. Unaweza kupata fenicha za nje nzuri na imara kwa bei nafuu kabisa
kwa kununua zile zilizotumika. Fenicha zinazouzwa kwenye minada ya wafanyakazi
wa kimataifa wanaomaliza muda wao na hivyo kurejea kwao, ukizifanyia maboresho
kidogo na kuzisafisha zinaonekana kama mpya, na huwa hizi zinakuwa na ubora
unaokubalika. Unaweza pia kufikiria kubadilisha mito na makusheni kwa ajili ya
kuhuisha fenicha za nje za zamani.
Makala hii
imeandaliwa na Vivi Machange ambaye ni mjasiriamali upande wa usafi wa nguo, mazulia na magari;
pia ana mapenzi makubwa ya muonekano wa nyumba. Kwa maoni au maswali tuma
kwenda 0755 200023 au christines.daughter@yahoo.com
No comments:
Post a Comment