Boresha muonekano wa ndani ya nyumba kwa kuweka vioo vya
mapambo.
Vioo vina kitu kwakweli ambacho ni maalum ndani yake.
Vinakusaidia kukujulisha unaonekanaje na pia kukuwezesha kujiweka jinsi ambayo
unataka uonekane. Zaidi ya haya maandalizi binafsi na kujiridhisha na muonekano
wako kabla hujatoka, vioo vinasaidia pia kwenye kupamba ndani na hivyo kufanya
muonekano wa nyumba kuwa maridadi na nadhifu zaidi kwa kila mgeni
anayekutembelea.
Kama
kuna pambo la ndani ambalo wenye nyumba hatakiwi kulikosa, basi ni kioo.
Havitumiki tu kujiangalia unapoingia, bali vina mahadhi yake kwenye kuongeza
staili ya chumba au muonekano wa kupagawisha kwa kumfanya mgeni kuduwaa. Sababu
nyingine kuu hapa ni kuwa vioo vinaweza kuwa
na bajeti rafiki. Ni kweli kuwa kuna vioo ambavyo ni lazima viwepo
nyumbani kwa matumizi kuwa watu wanahitaji ili kuhakikisha kuwa wanaonekana
jinsi wanavyotaka kuonekana, lakini leo kwenye makala hii tunaongelea vioo kama
mapambo ambavyo unaweka kwenye ukuta wa nyumba yako ili kuongeza staili na
ukubwa.
Utagundua
kuwa leo, sokoni kuna aina nyingi na tofauti za miundo na aina za vioo.
Watengenezeaji wa vioo vya mapambo wanakuja juu kwa kuongeza ubunifu hasa wa
fremu wanazofungia vioo hivi. Unaweza kuvipata vioo hivi vikiwa kwenye fremu ya
kila malighafi unayohitaji kwa mandhari unaotaka kutengeneza.
Fremu nayo ni kigezo muhimu cha kioo kuwa kifaa cha mapambo. Unaweza
kuagiza kioo kwa umbo unalotaka kwa mfano unaweza kuwa na kioo kwenye ukuta wa
sebule ambacho kinatoa sura kwenye taswira nne kwa jinsi ambayo ukijitazama
unaona uso nne zinazofanana.. Haijalishi staili unayotaka au bajeti uliyonayo,
kuna uhakika wa kupata kioo ambacho ni sahihi kwa mradi wako.
Sababu
ya kuweka vioo hivi ndani ya nyumba ni ukweli rahisi kuwa unataka kutumia ile hali
ya kujiona ndani ya kioo kwa faida ya kimapambo. Baadhi wananunua vioo na
kuvitundika kama sanaa nyingine za ukutani, kwa maana ya kuwa wanakitundika
katikati ya picha na fremu nyingine, au wanakiweka kwenye ukuta ambao hauna
kitu kingine ambacho kingefaa hapo. Hata hivyo unaweza kutumia vioo vya mapambo
kuakisi mwanga na vifaa. Kwa mfano unaweza kuwa na ujia (corridor) ambao una
mlango upande mmoja lakini mwingine hauna. Pambo lako hapo linaweza kuwa mmea
wa kijani (uwe hai au mfu) pale kwenye ukuta usiokuwa na mlango pamoja na kioo.
Kioo kitauakisi ujia kwa kuukuza uonekane mpana na mrefu. Kupamba kwa vioo kunafanya eneo dogo lionekane kubwa na
mbinu hii inatumika na wataalam wengi wa ubunifu wa ndani nyumba.
Kupamba kwa vioo kunaongeza mwanga
wa chumba. Chumba kilichopakwa rangi ya giza kinaweza kuonekana kidogo,
kuongeza vioo kwenye kuta zake kutaboresha mwanga. Njia sahihi zaidi ya kuongeza
mwanga wa jua bila kuongeza taa ni kufunga vioo vitazamane na madirisha. Vioo
vinadaka mwanga wa jua toka dirishani na kuusambaza chumba kizima. Hii inaweza
kuwa njia mojawapo pia ya kubana matumizi badala ya kuwasha taa mchana.
Kupamba kwa vioo vya mapambo hakuhitaji mtaalam. Mtu akiwa na vifaa vya toolbox anaweza kufunga vioo ukutani na kutengeneza chumba chenye muonekano mzuri kwa gharama nafuu.
Chagua vioo vyenye maumbo ya kuvutia,
pembe nne ni nzuri ila vioo vyenye maumbo yasiyozoeleka vinafanya umaridadi
zaidi. Tafiti aina na maumbo mbalimbali ya vioo kabla hujamua ni vipi unataka.
Ili kukifanya chumba kisicho na
uwiano kionekane kuwa nao, funga vioo vya mapambo ukutani. Vioo hivi viwekwe
kuakisi vitu fulani kwenye chumba ili kufanya ionekane kama vitu hivi viko
katika kila upande wa chumba, kwahivyo pale unapoingia uone kama chumba kina
uwiano na ni kikubwa.
Baadhi ya wenye nyumba wanatamani
waboreshe muonekano wa ndani wa nyumba zao. Marekebisho yana gharama kubwa,
hata hivyo wewe mwenye nyumba usizime tamanio lako. Unaweza kunyanyua uso wa
ndani ya nyumba yako kwa kutumia vioo vya mapambo badala ya marekebisho
makubwa.. Mradi huu mdogo wa kunyanyua uso kwa kutumia vioo unaweza kukupa
matokeo usiyotarajia. Kupamba kwa vioo ni moja kati ya njia nyepesi na rahisi
za kuboresha muonekano wa ndani ya nyumba.
Makala hii
imeandaliwa na Vivi Machange ambaye ni mjasiriamali upande wa usafi wa nguo, mazulia na magari;
pia ana mapenzi makubwa ya muonekano wa nyumba. Kwa maoni au maswali tuma
kwenda 0755 200023 au christines.daughter@yahoo.com
No comments:
Post a Comment