Saturday, December 3, 2016

Namna ya kuboresha hali ya hewa ndani ya nyumba

Ulishafikwa na tatizo la kuingia nyumbani na mara kichwa kinaanza kukuuma kwa hewa nzito iliyopo? Au labda umegundua harufu ambayo huifurahii ndani ya nyumba yako na haielekei kuisha? Hizi zote ni dalili za haja ya kuboresha hali ya hewa ya ndani ya nyumba.

Watoto na watu wenye mzio wanaweza kuhisi mabadiliko ya hewa ndani ya
nyumba hata yawe madogo kiasi gani. Ila pia matokeo ya hewa nzito ndani ya nyumba yanaweza kuwasababishia wanafamilia matatizo ya kiafya miaka mingi ijayo endapo tatizo hilo halitafutiwi suluhisho mapema.

Inawezekana mwanzoni likaonekana ni jambo gumu la kufanya, ila cha kushangaza ni kuwa kuboresha hali ya hewa ya ndani ni rahisi sana. Unachotakiwa ni kuzingatia tu mambo machache, na unaweza kuwa na nyumba huru na harufu na isiyokuwa na vichafua hali ya hewa.

Uboreshaji wa uingizaji njia za kuingiza hewa ndani ni namna kuu  ya kuongeza ubora wa hewa ya ndani. Wakati hewa inapoanza kuwa nzito na hakuna uingizaji wa iliyo safi hapo ndipo na vichafua hewa ndani ya nyumba vinapoanza kujijenga. Na changamoto kubwa ya nyumba zetu za kisasa ni kuwa zimezibwa kila mahali na ni kawaida kukuta milango na madirisha yamefungwa kwa muda mrefu kuliko yanavyofunguliwa. Njia rahisi ya kuondoa tatizo hili ni kufungua madirisha kila siku na pia kuwasha feni.

Jambo lingine ni kuzingatia usafi wa jumla, kwamba sakafu ziwe safi  na zisafishwe kila inapobidi. Kwa kuruhusu taka, nguo chafu, vumbi na uchafu mwingine kujijenga unakaribisha uwezekano wa kuharibu hali ya hewa ndani ya nyumba. Usiruhusu vyombo vichafu vijazane kwa muda mrefu bila kusafishwa, na pia usihifadhi nguo chafu zinazonuka majasho kwa muda mrefu bila kufuliwa. Futa vumbi kila wakati.

Kama una vifaa vya kisasa vihusianavyo na maboresho ya hewa ya ndani kama vile viyoyozi hakikisha kuwa vinafanyiwa usafi wa mara kwa mara ili chujio zake zisibebe vumbi na kushiriki kulisambaza. Pia feni zisafishwe. Bila kusahau kutumia marashi za kupuliza ndani ya nyumba pale inapobidi.

Epuka vichafuzi vya hewa ya ndani kama kweli umepania kuboresha hali ya hewa ndani ya nyumba yako. Kitu cha kwanza cha kufanya ni kuepuka kinachoharibu hali hiyo ya hewa.  Kwa mfano kuna fenicha na gundi zinazotoa harufu kipindi chote, madawa, manukato yatumikayo kwenye dawa za kusafishia. Na pia kuna harufu zinaingizwa ndani ya nyumba kupitia fenicha mpya, magodoro, mazulia au hata rangi ya ukutani.


Uvutaji wa sigara ndani upigwe marufuku kabisa kwani ndio kichafuzi namba moja cha hewa. Inaweza kuwa maumivu kama mvutaji ni mwenye nyumba lakini hakuna jinsi itabidi iwe hivyo. 

No comments:

Post a Comment