Wednesday, December 14, 2016

Unaponunua mti wa bandia wa Krismasi zingatia haya

Kwa miaka kadhaa sasa baadhi ya Watanzania wamekuwa na utamaduni wa kupamba nyumba zao kwa kutumia miti bandia ya krismasi kipindi cha msimu wa sikukuu hiyo. Miti hii imepata umaarufu kwa kasi kwani inasaidia kupunguza usumbufu na pia unaweza kuhifadhi baada ya sikukuu na kutumia tena mwaka inayofuata.

Kutokana na kuwepo kwa
miti mbalimbali ya bandia ya krismasi inayouzwa, inaweza kukuwia changamoto kupata ulio sahihi. Kwa kuzingatia yafuatayo itakurahisishia mchakato huo.

Kwanza kabisa fahamu ukubwa wa mti unaohitaji. Na hii itakusaidia pale ambapo unajua kabisa kuwa ni wapi unauweka iwe ni kwenye ujia, kona ya chumba au katikati. Ndipo unafahamu ni eneo kiasi gani unalohitaji kufunika. Unafahamu upana na urefu, usinunue mti mrefu kiasi kwamba utagusana na dari.

Nunua mti wenye ubora wa juu. Moja ya faida ya mti wa krismasi wa bandia ni kwamba ni uwekezaji wa miaka mingi. Kufahamu kiwango cha ubora angalia majani yake. Mti wenye majani yaliyofunga hata kuficha shina ni bora kuliko ule ulio wazi. Halafu pia miti ya bandia ya krismasi yenye ubora wa hali ya juu huwa ina stendi za chuma. Kama lengo lako ni mti bora, epuka ile yenye stendi za plastiki.

Stendi imara inakuhakikishia mti kutoinama au kutojikunja upande mmoja, hata pale mapambo inayobeba yanapokuwa ni mazito. Baadhi ya miti ambayo ubora ni wa hali ya juu zaidi, stendi zake za chuma zinakuwa zimeongezewa mipira ili kulinda sakafu.

Ingawa miti ya bandia ya krismasi inaweza kuwa na mchanganyiko wa maumbo mawili ya majani yake, haijalishi ni upi utanunua ila cha kuzingatia ni kununua ambao ngalao wenye muonekano wa mti hai. Kwa mfano ipo miti ambayo rangi zinapishana kuendana na eneo la mti kama ni shina, majani yaliyokomaa na yale machanga. Kwa mfano tawi au shina linaweza kuwa na kijani kinachoelekea kwenye rangi ya udongo wakati majani yaliyokomaa yakiwa na kijani kizito huku yale mabichi yakiwa na kijani mpauko. Hii yote ni kujaribu kuongopea jicho kwamba mti ni hai.

Nunua mti ambao utakubaliana na ulivyopanga kuupamba. Hakikisha matawi ni imara kuweza kubeba mapambo unayotaka kuuwekea.


Fahamu rangi unayotaka kabla hujanunua. Waliokulia kwenye nyumba ambazo zina kawaida ya kupamba kwa mti wa krismasi wanajikuta wakidhani kwamba mti wa krismasi sahihi ni ule wanaoufahanmu toka utotoni. Mingi ya miti hiyo ya zamani ilikuwa rangi ya kijani tu, ila kwa miaka ya sasa tumeona miti ikija kwa rangi nyeupe, silva kama barafu na kadhalika. Usifungwe na fikra za kuwa mti wa krismasi lazima uwe wa kijani. Nunua mti ambao utakutengeneza kumbukumbu nzuri na muhimu kwako na familia yako.

No comments:

Post a Comment