JESHI la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, limesema
watu 12 wamethibitika kupoteza maisha jijini humo kutokana na athari za
mafuriko ya mvua zinazoendelea kunyesha.
Taarifa iliyotolewa Dar es Salaam
jana na Kamanda wa
Kanda hiyo, Kamishna Suleiman Kova, ilisema idadi hiyo ni ongezeko la watu
wanne kutokana na taarifa ya awali iliyotolewa na jeshi hilo juu ya vifo vya
watu wanane.
Alisema Mei 9, mwaka huu, saa 12 asubuhi katika Bonde la
Mto Mkwajuni, Mtaa wa Makuti, Magomeni, wilayani Kinondoni, ulipatikana mwili
wa mwanamke anayekadiriwa kuwa na umri kati ya miaka 40-45, ambaye hakufahamika
jina lake wala
makazi, akiwa amevaa nguo aina ya dera rangi ya njano.
Aliongeza kuwa, mwili wake umehifadhiwa katika Hospitali
ya Muhimbili kwa utambuzi ambapo mtu mwingine Valerian Eradius (13), mwanafunzi
wa kidato cha kwanza, Sekondari ya Kigogo, mkazi wa Mburahati kwa Shebe,
alifariki dunia Mei 10 baada ya kuangukiwa na ukuta.
"Mei 8, mwaka huu, maeneo ya Mbezi Beach
Kilongamiwa, Tarafa ya Kawe, wilayani Kinondoni, mtu mmoja Gervas Shayo (28),
mkazi wa Mbezi Juu alikufa maji na mwili wa marehemu umehifadhiwa Hospitali ya
Mwananyamala.
"Mtu mwingine anayekadiriwa kuwa na umri kati ya
miaka (35-38) ambaye jina, umri wala makazi yake hayajajulikana, ameopolewa
katika tope leo (jana), maeneo ya Magomeni Suna katika Bonde la Mto Msimbazi
akiwa amefariki, mwili wake upo Hospitali ya Muhimbili," alisema.
Kamishna Kova aliongeza kuwa, uzoefu unaonyesha jinsi
maji yanavyoendelea kupungua, madhara yanaendelea kuonekana; hivyo aliwataka
wananchi kutoa taarifa mapema ili hatua zichukuliwe mara moja pamoja na kuiondoa miili ya watu
waliokufa kutokana na athari za mvua hizo.
MAJIRA
No comments:
Post a Comment