MKAZI wa kijiji cha Kisalala, Kata ya Laela wilayani
Sumbawanga katika mkoa wa Rukwa, Lydia Shazi (29) amejifungua watoto watatu
wote wa kiume kwa siku tofauti na hospitali mbili tofauti.
Akizungumza na HABARI LEO hospitalini hapo jana mama huyo
ambaye sasa amekuwa na idadi ya watoto saba alieleza kuwa mtoto wake wa kwanza
alijifungulia katika Kituo cha Afya kilichopo mji mdogo wa Laela wilayani
Sumbawanga uliopo umbali wa kilometa 97 kutoka mjini Sumbawanga.
Aliongeza kueleza kuwa mtoto huyo alizaliwa Mei 6 mwaka
huu katika zahanati hiyo akiwa na uzito wa kilo 2 na gramu 200.
“Wakunga na wauguzi katika kituo cha afya cha Laela
walifahamu kuwa nitajifungua mapacha hivyo baada ya kubaini kuwa nina upungufu
wa damu mwilini waliamua kunikimbikiza katika Hospitali ya Mkoa wa Rukwa mjini
Sumbawanga kwa uchunguzi na matibabu,” anaeleza.
Aliongeza kuwa alifika hospitalini hapo Mei 6, mwaka huu
ambapo alilazwa ambapo baada ya siku mbili tangu nijifungue mwanangu wa kwanza
nilihisi uchungu na nikajifungua mtoto wa pili na watatu Mei 8 , mwaka huu.
“Mtoto wa pili alizaliwa akiwa na uzito wa kilo mbili
kamili wakati wa tatu alikuwa na kilo 2 na gramu 600… hawa wawili
nilijifungulia hapa hospitali ya mkoa Mei 8, mwaka huu wakati wa kwanza
alizaliwa katika kituo cha afya Laela Mei 6, mwaka huu… namshukuru Mungu
wanangu wote ni wazima wenye afya njema isitoshe nilijifungua salama tena kwa
njia ya kawaida,” alibainisha mzazi huyo.
Akizungumza na gazeti hili hospitalini hapo ambapo mzazi
huyo anaendelea kupatiwa matibabu kutokana na kubainika kitabibu kuwa ana
upungufu wa damu, ameiomba Serikali na jamii imsaidie chakula na mavazi kwa
ajili ya watoto hao kwa kuwa uwezo wake wa kipato kuwahudumia ni mdogo.
“Namshukuru Mungu nimeweza kujifungua salama …licha ya
watoto hawa watatu niliojifungua hospitalini hapa, bado nina watoto wengine
wanne nyumbani …hali ya kipato mie na mume wangu si nzuri hata kidogo …hivyo
naiomba Serikali na jamii inisaidie katika malezi na makuzi ya watoto hawa
watatu,” alisisitiza.
Mama huyo alikiri alikuwa akifahamu kuwa angejifungua
pacha, lakini hakudhani wangekuwa watoto watatu, “maandalizi yangu kabla ya
kujifungua yalikuwa hafifu sana naomba mwenye nguo, mafuta ya kupaka watoto
wanisaidie,” alieleza kwa hisia.
Akizungumza na gazeti hili hospitalini hapo, mkunga na
muuguzi wa zamu katika wodi ya wazazi hospitalini hapo, Cremensia Kagoma
alithibitisha kuwa hali ya kiafya ya mama huyo inazidi kuimarika mara baada ya
kupatiwa matibabu ikiwa ni pamoja na kuongezewa damu.
Kwa mujibu wa muuguzi huyo wa zamu, alieleza kuwa mzazi
huyo alifika hospitalini hapo hali yake ikiwa duni sana hivyo iliwalazimu
wahudumu wa afya hospitalini hapo kuchanga kiasi cha Sh 70,000 ambazo
zimetumika kuwanunulia watoto hao nguo nzito ili kuwakinga na baridi.
No comments:
Post a Comment