Mwanamke
anavyovutia akivaa mkanda kuendana na umbile lake
Mikanda sio rafiki wa kila mtu. Mkanda unaweza kuwa
kitupio cha mitindo chenye changamoto kuvaa hasa kama huna umbile kama la wanamitindo.
Kiukweli mkanda unaweza kuwa kinyume chako kwa kuonyesha yale maeneo ya mwili
ambayo ungependa kuficha kama utachagua saizi, aina au kuvaa mahali pasipo
sahihi.
Mikanda ya wanawake ipo iliyotengenezwa kwa ngozi, vitambaa, vito na
kadhalika. Ipo ya rangi moja au yenye malighafi nyingine kama nyuzi, vito,
mawe, bakoli na nyingine nyingi. Mikanda iliyozoeleka sana ni ya ngozi na
vitambaa, chagua mkanda ambao sio tu unaendana na vazi lako, bali pia
unaonyesha vyema umbo lako la kike. Kwa mfano mkanda mpana unapendeza kwa
mwanamke mwenye umbo namba nane
kwa
kutenganisha vyema kiuno hivyo kuleta mvuto kiunoni. Mkanda huo ukivaliwa
sehemu nyembamba kuliko yote ya kiwiliwili – sehemu ya asili ya kiuno ambapo ni
pale penye kitovu unasisitiza umbo halisi la kike na pia unamfanya mvaaji
kuonekana slimu.
Kiasili mikanda ya wanawake ilivaliwa kwenye nyonga tuu ila karne hii inavaliwa
popote kwenye kiwiliwili chake. Ipo inayovaliwa chini tu ya matiti, ipo
inayovaliwa sehemu ya asili ya kiuno na ipo inayovaliwa chini ya kiuno karibia
kabisa na makalio.
Inalipa kujaribu mikanda mbalimabali sehemu mbalimbali za kiwiliwili kuona
matokeo tofauti tofauti. Pia zingatia aina na ukubwa wa bakoli kwa kuwa
zinaweza kukuonyesha kiwiliwili kipana au chembamba. Usijali, kwa majaribio
kadhaa utapata picha ya mkanda wa kukutoa bomba.
Kama
baada ya kujifungua umebaki na tumbo kubwa wala usione aibu kuvaa mkanda.
Mkanda uliovaliwa vyema kiunoni utanyonga tumbo na kukupa umbo namba nane.
Mkanda mpana wenye rangi zilizokolea unaovaliwa
kwenye eneo asili la kiuno ( yaani pale kwenye kitovu) unakufanya uonekane
tumbo slimu. Usinyonge sana ili nyama zisigawanyike
labda tu kama umevaa blauzi pana ambayo haitaonyesha mikunjo ya nyama.
Ukiwa umefungwa vyema mkanda wa kuzunguka nyonga ndio njia iliyozoeleka
zaidi ya kuvaa mkanda na ambayo haipitwi na wakati. Vaa mkanda mwembamba au mpana
nyongani na suruali au sketi ya mtindo wa katibu muhtasi au gauni la shifti au
juu ya blauzi yenye vifungo. Ukivaa mkanda wa kwenye nyonga jitahidi kupunguza
vitupio vingine na pia usivae na hereni au bangili za plastiki kwa ajili
unawezekana kuonekana kama wa mwaka 47..
Jitahidi kuoanisha rangi kwa mfano, kama unavaa suruali pensi nyeupe na
shati jeusi unaweza ukafikiria mkanda mweupe vile vile.
Kama mkanda utavaliwa karibia na makalio badala ya kwenye nyonga itasaidia
kuondoa macho ya mtazamaji kwenye tumbo na kuelekezea kwenye mkanda. Pia kama
una tumbo kubwa njia nyingine ni kuvaa mkanda chini tu ya matiti kuliko kiunoni
kabisa. Mikanda inayovaliwa eneo hili la kiwiliwili inatakiwa kuwa myembamba na
bila madoido. Vaa mkanda chini ya matiti pale tu nguo yako ikiwa ina vile
vishikizo vya mkanda kwa ajili kama tujuavyo bila hivi vishikizo mkanda utang’ang’ania
kushuka chini. Ila jua kuwa uvaaji huu wa mkanda utakufanya uonekane na kifua
kikubwa.
Kama una kiwiliwili kifupi unatakiwa kuvaa mkanda
kwa jinsi ambayo kitaonekana ni kirefu. Chagua mkanda wa rangi ya jamii moja na
nguo uliyovaa kwa ajili mkanda ukiwa na rangi tofauti kabisa na vazi utaleta
mgawanyiko hivyo kufanya kiwiliwili kizidi kuonekana kifupi kwa kuonekana
kimekatika nusu mbili. Kuvaa mkanda wa jamii moja na vazi ni njia pia ya
kuonekana slimu hasa maeneo ya tumboni.
Kama
una bahati ya kuwa na kiwiliwili cha umbo namba nane au umbo la tofali mkanda
mpana ukivaliwa nyongani utakutoa bomba. Mkanda wa kiunoni utakufaa zaidi wewe
mwenye umbile hili kulikoni ule wa chini ya matiti au wa kwenye makalio.
Miili midogo inapendeza na mikanda myembamba wakati wale wenye miili kikubwa
wang’ang’anie mikanda mipana. Mikanda myembamba sana kwa miili mikubwa inaweza kuongeza
ukubwa wa mwili wa mvaaji kimuonekano wakati ile minene na mipana kiasi italeta
uwiano wa muonekano.
Uwe uwavyo mkanda kwa mwanamke ni sawa na polishi kwenye mbao huongeza mvuto
kwa kila vazi. Kila leo mikanda inavaliwa kiubunifu zaidi kiasi kwamba unaweza
kuazima mmojawapo hata kwenye kabati la nguo la patna wako.
Makala
hii imeandaliwa na Vivi O. Machange 0755 2000 23