Thursday, August 2, 2012

My Article for Newspaper: Mitindo; Wanawake Dhidi ya Wanaume


Mitindo; wanawake dhidi ya wanaume


Mara nyingi wanawake wanakuwa macho na mitindo zaidi ya wanaume – wakitafuta mitindo iliyopo na ambayo itawapendeza. Mwanamke atanunua majarida ya mitindo, kwenda kwenye mitandao kuangalia mitindo ya nyakati na ni nini wanamitindo wanaonyesha kwenye maonyesho mbalimbali ya mavazi. Hata hivyo, wanaume wengi hawako hivyo, wao wanavaa kile tu wanachojisikia watakuwa huru. Kwa nini kuna tofauti ya mtizamo wa mitindo kati ya wanawake na wanaume; na je jinsia ya kiume kweli inajali kama mwanamke anavaa kuendana na wakati ama laa?

Msisitizo wa uzuri wa mwanamke unaongezeka kila kukicha. Jinsia ya kike inaonekana kupendelea na kuthamini zaidi kuvaa kuendana na mtindo uliopo. Katika ulimwengu wa mablog na mitandao mingine ya kijamii wanawake wamekuwa wakiweka picha zenye kuonyesha mitindo yao wakiwa wametoklezea bomba (na wanaume nao wanaelekea hukohuko). Kutokana na kuwa macho juu na mitindo wanawake mara nyingi kuwa na hela na muda wa kufanya manunuzi ya haraka na mwishomwisho kwa ajili ya viwalo vya mtoko wa jioni na shoga zake sio kitu cha kushangaza. Wanaume kwa upande mwingine wamekuwa wakionekna kama hawana ubunifu sana wa kujua wanavaa nini. Hata hivyo hisia hizi zinaonekana kuyeyuka kadri siku zinavyosoga kwani wengi wameonekna wakiwa madukani wakicheki ni raba gani zitakazoendana na kaptula zao za jinzi.

Kupata toleo jipya la gauni linaloshika kiuno ni njia ya urembo kwa wanawake karne hii. Tasnia ya mitindo nayo imejikita zaidi kwa wanawake – majarida mengi yanatoa dondoo na miongozo ya mitindo ya kike, kwa mfano ni wapi pa kununua magauni ya maksi wakati huo huo majarida haya hayatoi mwongozo huu kwa wanaume.

Pamoja na kuwa muonekano wa mwanamke umekuwa sehemu kubwa ya mitindo ya kike historia inaonyesha kuwa tangu kale mwanamke kuvaa kuendana na wakati kumemfanya ajisikie yuko juu na wa kisasa zaidi. Kupitia mitindo mwanamke anaongeza kujiamini kwake wakati kwa wanaume ni tofauti. Wanaume wao wanaongeza kujiamini kwao kwa njia nyingine ambazo sio mitindo ambazo zinaweza zikaeleza kwa nini wanaume wanavutiwa sana na mazoezi ya kuongeza misuli na ukakamavu kinyume na kuwa macho juu kujua ni mitindo gani ya nguo za usiku za kiangazi imeingia kwenye maonyesho na madukani.

Burudani kwa sehemu kubwa imechangia wanawake kuvutiwa na mitindo.  Bila kuwa na mvuto kwenye sanaa ya mitindo tasnia hii isingekuwepo. Kwa wengine ni njia ya maisha, kazi zinapatikana kutokana na mitindo. Wakati kufuatilia mitindo ni kwa wanawake ni kama labda mpira wa miguu wa wanaume – kitu wanachopendela na ni burudani kwao.

Wakati kuna wanaume pia wanaopenda kufuatilia mambo ya mitindo, wanawake wanajijali zaidi muonekano wao na ni nini wanavaa. Hata hivyo ulimwegu unabadilika kila siku na karne zijazo huenda wanaume wakawapiku wanawake kwenye kufuatilia mambo ya mitindo.

Mwanamke anapenda upekee na staili za kivyakevyake zaidi ya mwanaume alivyo. Hebu fikiria kisa hiki: Mwanamke anaingia kwenye mkusanyiko na kukuta wanawake wengine wawili wamevaa gauni kama lake. Kwa mwanamke yeyote yule atashangaa hee imekuwaje! Na kama mwanamke huyo ni mtu maarufu kama walio na wasaidizi binafsi wa kuwapangia nguo za kuvaa basi hata huyo msaidizi huenda akafukuzwa kazi kuwa alimchaguliaje gauni kama sare ya shule. Sasa tuangalie kisa hikihiki kwa upande wa wanaume.  Mwanaume ameingia kwenye sherehe na kukuta wanaume wengine wawili au watatu wamevaa suti kama yake.  Wanaume wengi watachukulia hii kama chanya. Fikra kama: “inaonekana kama nimevaa sahihi kwa ajili ya tukio hili” au “ niko mahali sahihi” mawazo haya yatakuja akilini mwa wanaume walio wengi.  

Kwa kuwa wanawake wengi wanapenda staili za peke yao zaidi ya wanaume walivyo wabunifu wengi wa mavazi wameweka nguvu zaidi kwenye mavazi ya kike. Pia ukisoma historia za wabunifu wengi maarufu walianza kubuni mavazi ya wanawake kabla ya kubuni ya wanaume.

Mwanamke usimkasirikie patna wako kuwa haulambi, wanaume wanapenda kuvaa wajisikie huru na kwao haijalishi sana kama ni mtindo uliopo ama laa.
Makala hii imeandaliwa na Vivi O. Machange 0755 200023

No comments:

Post a Comment