Mazingira
ya nyumbani kwako yasaidie kufanikisha maazimio yako ya mwaka mpya
Ni wakati mwingine tena wa mwaka ambao wengi wetu
wanapenda kufanya mabadiliko kwenye maisha yao. Je umeshafikiria mabadiliko ya
mwaka mpya kwa ajili ya kiota chako? Japo mabadiliko haya yanajulikana na wengi
zaidi kama maazimio, kwa kutia msisitizo zaidi makala hii itayaita malengo.
Malengo yanatamkwa kwa kusisitiza wakati uliopo ni nini tamanio lako (kwa mfano
kuamua kubadili mpangilio wa fenicha za sebuleni kwako ili kuwezesha kunogesha
zaidi mazungumzo) wakati maazimio yanatamka ni nini ungependa huko mbeleni ya
kuwa unaenda kufanya nini wakati ujao.
Mara nyingi malengo (au maazimio) ya mwaka mpya
yanatupiliwa mbali hata kama nguvu za kutosha ziliwekwa ili kuhakikisha yanafanikiwa.
Moja ya sababu za malengo kutofanikiwa ni mazingira ya nyumbani kwako kutosaidia
kuwezesha mafanikio ya malengo hayo. Kama unataka kufanya mabadiliko ndani ya
maisha yako bila kuhusisha mazingira yako kufanikiwa ni hatihati. Kwa maana ya
kwamba kama unaweka malengo yako ya mwaka 2013 kwa ajili ya makazi yako na
ukayaacha mazingira yalivyo, ni ngumu sana kubadili chochote. Hata matangazo
kwa mfano ya kujikinga na maambukizi ya VVU yanaonyesha uhusiano kati ya
maambukizi na mazingira fulani ambayo yanachochea maambukizi hayo.
Kanuni ya malengo kuwa na uhusiano na mazingira inahusika
karibia katika kila kitu. Kama unataka mwaka ujao uwe tofauti basi unatakiwa
kuweka mazingira ya kuwezesha malengo yako.
Je mazingira yako yanakusaidia kupata kile unachokihitaji?
Kwenye mazingira ya nyumbani kwako vitu ambavyo havijakaa mahali pake au
vimekaa mahali ambapo havifanyi kazi yake au havitumiki tena vinakukwamisha
kutimiza malengo yako hapo nyumbani. Tembelea kwenye makabati ya nguo na vyombo
angalia kwa umakini kuona ni vitu gani vya kuhifadhi, vya kugawa ama vya
kutupa. Fanya hivyo kwa nia ya kupata nafasi ya kile tu kitakachosaidia
kufanikisha malengo yako.
Pengine lengo lako la mwaka mpya ni kutokula hovyo
kwa nia ya kupungua uzito. Je mara zote unaingia nyumbani kwa kupitia mlango wa
nyuma ambapo unaingilia moja kwa moja jikoni? Kumbuka kanuni kuwa unachokiona
mwanzo kinagusa zaidi akili yako, kwa hiyo kama mara ungiapo ndani unakutana na
jokufu, chakula na kadhalika utapata hamu ya kula hapo hapo. Tumia mlango wa
mbele ambapo utaona kitu tofauti mara uingiapo ndani - kitu ambacho
hakitakufikirisha kula.
Mahusiano mengi yanaweza kuboreshwa kwa mapambo ya
nyumbani hasa katika swala la kuwasiliana. Je chumba cha kulala cha wakuu wa
familia ni mahali patakatifu kwa wawili? Hakikisha vitu kama taa, vimeza, na
viti kwenye chumba hicho viko viwili viwili.
Au lengo lako mwakani ni kuwa na wageni wengi zaidi
nyumbani? Hakikisha basi mlango wa mbele unaonekana na kuna njia ya wazi ya
kuingilia. Taa zinazomulika njia ya kuelekea mlango huo ziwe zinafanya kazi.
Pitia mlango wa mbele kama mgeni mtarajiwa uone kama kila kitu kiko sawa. Je
njia hiyo inakaribisha? Na sebule yako je nayo inavutia kwa ajili ya wageni
wako wengi ambao unapenda kuwaalika nyumbani mwakani?
Kwa wale ambao azimio lao kuu la mwaka 2013 ni
kupamba nyumba zao hakikisha unachagua rangi kwa umakini, fikiria mpangilio wa
fenicha je zinawatendea haki watumiaji wa chumba husika. Angalia vitu ambavyo
inabidi uvifanyie kazi ili kuboresha muonekano wa makazi yako. Kama kwa mfano
sakafu ya sebule yako ni ya marumaru na unachoka kusugua na kudeki kila siku na
unakiri kuwa ni ngumu kuifanya iwe safi; basi weka zulia kubwa ambapo
utapitisha mashine ya kunyonya mchanga mara mbili au tatu kwa wiki.
Ikiwa unaazimia kutojaza vyombo vichafu kwenye karo
basi mwaka ujao lenga kuosha chombo mara baada ya kukitumia. Na hata hakikisha
wanafamilia wengine pia wanafanya hivyo.
Huenda kijani kinakubariki lakini huna eneo kubwa ya
kuweza kuwa na bustani za ardhini. Otesha basi bustani za kwenye vyungu walau
ukifungua pazia la chumba cha kulala kunapopambazuka ukutane na kijani. Azimia
kupamba ndani mwako kwa maua freshi japo mara moja kwa mwezi.
Kweli, baadhi ya mabadiliko ya nyumbani kwako
unaweza kuhitaji kutafuta msaada, lakini kuna mabadiliko mengi sana ambayo
hayahitaji gharama lakini yanahitaji muda na nguvu ( na pengine
kautaalamu) kwahiyo kwa 2013 kwa nini
usiazimie kupamba mwenyewe? Unaonaje? Ni azimio moja zuri kwa ajili ya makazi
yako ambalo unaweza kutekeleza. Fanya usafi mkubwa ndani ya nyumba yako mara
moja kwa mwezi ( weka tarehe kwenye kalenda yako na isismamie). Shikrikisha na wanafamilia
wengine pia.
Hii inaweza isikubalike kwa baadhi ya watu ila ni
mawazo binafsi kuwa azimia kila anayeingia ndani avue viatu mlangoni. Viatu vya
wanawake vilivyo na visigino vya ncha kali mara nyingine vinakwaruza sakafu za
marumaru na mbao na kuacha alama na vile vya wanaume baadhi vina soli
zinazoacha rangi sakafuni na hivyo kufanya sakafu ionekane zee kuliko kawaida.
Mwaka ujao lenga kuweka nyumba yako nadhifu kila
mara kama vile unategemea mgeni wa heshima!
Makala
hii imeandaliwa na Vivi O. Machange. Kwa maoni niandikie viviobed@yahoo.co.uk au kwa simu 0755 2000 23
No comments:
Post a Comment