Jinsi
ya kupamba nyumba yako kwa kutumia vioo
Kwa uchache kila binadamu anapenda vioo. Huenda
unajiuliza kama kuna sehemu nyumbani kwako ambayo hupaswi kuweka kioo. Kupata
jibu la swali hili kwanza jiulize ni nini kinachooonekana kwenye kioo hicho. Ni kitu ambacho unakipenda
zaidi? Kama una kioo kinachotazamana na kabati lenye mrundikano wa vitabu basi
ukiangalia kwenye kioo hicho unaona makabati mawili yenye mrundikano wa vitabu!
Na vile vile kioo kinachotazamana na picha nzuri kitakuonyesha picha mbili nzuri.
Vioo vinaweza kufanya mwanga wa nje uje ndani na
kuleta mng’ao ndani ya nyumba. Weka kioo kitazamane na dirisha na mara moja
mahali panafunguka. Kioo pia kinaweza kusaidia kufanya sehemu nyembamba
kuonekana pana. Weka kioo kwa jinsi ambayo kitanasa mwanga wa asili kutokea
dirishani; kwa hiyo mwanga utadunda kurudi chumbani. Hii ni dondoo muhimu kwa mapambo ya ndani kwa vyumba vyenye mwanga
hafifu.
Sehemu
mojawapo ya kuepuka vioo ni chumba cha chakula. Sijui yeyote ambaye angependa
kujiangalia kwenye kioo wakati anakula. Mazingira ya nyumbani yawe
yanafanikisha malengo yako. Chochote kinachokufanya usijisikie vizuri
hakisaidii kufanikisha malengo hayo.
Swala la vioo kwenye chumba cha kulala ni la mtu
binafsi. Ingawa vioo ni muhimu kwenye
chuma hiki ila sio vitazamane na kitanda. Ukubwa na mahali pa kuweka ni vitu
muhimu vya kuzingatia. Ukuta uliotundikwa kioo kwenye chumba cha kulala mara
nyingine unaweza kuondoa mazingira ya hisia kuwa chumba cha kulala ni kama
mahali patakatifu. Ni nani anapenda kujiona sehemu kubwa ya mwili wake? Jaribu
kufunika vioo vikubwa usiku ili kuleta usingizi mwororo.
Watoto ni wadadisi wa mazingira yao. Mara nyingi
wanaogopeshwa na vivuli wanavyoona kwenye vioo usiku. Watoto wengi wanaogopa kuwa
kwenye vyumba vyao hasa usiku kwa ajili ya vioo. Mara chache kufunika vioo
vyote usiku inasaidia, vinginevyo ni vyema kuondoa vioo kwenye kuta za vyumba
vya watoto na kuvitundika kwa ndani ya milango ya makabati ya nguo.
Vioo bafuni ni kawaida sana na vina kazi kwa hivyo
watu wengi wala hawafikirii kama ni mapambo ya ndani. Hata hivyo vioo vinaweza
kuongeza mapambo ya chumba chochote. Vioo vikubwa vinaweza kuwa vizito zaidi;
vitundikwe kwa uangalifu.
Kuweka ama kutoweka kioo kitazamane na mlango wa
mbele ni swali ambalo watu wengi wanajiuliza. Baadhi wanafikiri kuwa kioo
kwenye ukuta unaotazamana na mlango wa mbele kinawachanganya wageni
wanaokutembelea njia ya kuelekea; kwa hivyo watu hawa hupendelea kutundika
picha kubwa na kuweka kioo upande mwingine wa ukuta ila sio kitazamane na mlango
wa mbele. Kama utapenda kuweka kioo zingatia urefu wa yeyote aliyeko ndani ya
nyumba yako na pia mgeni wako.
Cheki kuona kuwa vioo vyote ndani ya nyumba yako
vimetundikwa katika urefu sahihi. Kioo kitundikwe kwa jinsi ambayo kichwa cha
kila mtu ndani ya nyumba kitaonekana. (Watoto wadogo wanaweza kuwa na vioo kwenye
vyumba vyao vya kucheza ambavyo vimetundikwa kwa urefu sahihi kuendana na wao.)
Sio afya na hujisikii vizuri ukijiangalia kwenye kioo na kuona sehemu ya kichwa
chako imekatika ama kichwa chote hakionekani kabisa. Watu wengi pia wanatundika
vipaneli vya vioo vilivyoko kwenye fremu moja ambapo inakuwa ngumu kujiona
kivuli kilichokamilika badala yake unajiona vipande vipande. Kama vile isivyo
poa kujiona sehemu ya kichwa ikiwa imekatwa vile vile haipendezi kujiona
vipande vipande. Kama una fremu ya vioo vya namna hii basi itundike itazamane
na dirisha ambapo italeta hisia ya kuwa kama nayo ni dirisha la ukweli.
Kioo chenye ufa au kipande maeneo ya kati
kinachokosekana kitakupa hisia ya wewe kuwa na ufa au chochote unachokiona
kwenye kioo hicho. Unaweza kupenda kioo cha sanaa fulani lakini kama kivuli
unachokiona hakionekani vizuri basi
hicho hakifai.
Tundika mfululizo wa vioo vitatu ama vitano vyenye
urefu sawa, vyembamba kufanya ukuta mfupi kuonekana mrefu. Mfululizo huu
unatengeneza mtindo wa kuvutia kwa kuonyesha sehemu tu ya chumba badala ya
picha nzima. Kwa mtindo huu chagua ukuta ambao haupokei mwanga wa jua wa moja
kwa moja ili kuepuka chumba kung’aa sana.
Yote kwa yote nia inachukua sehemu kubwa katika
kupamba kwa vioo. Fikiria kabla ya kutundika kioo. Kwa nini unakitundika hapo?
Ni nini kinaenda kuakisi. Kama vikiwekwa kwa mwamko na nia, vioo vinaweza kuwa
mapambo mazuri sana ya nyumba yako.
Makala hii imeandaliwa na Vivi O. Machange. Kwa
maoni niandikie viviobed@yahoo.co.uk au kwa simu 0755 200023
No comments:
Post a Comment