Jinsi
ya kuwa na mpangilio na kuondoa mlundikano wa vitu katika nyumba yako
Unapohitaji kitu na ukakifuata mahali kinapotakiwa
kiwe usipokikuta hapo unaweza kujisikia hasira, kuchanganyikiwa na hata kama ni
katika uzalishaji ukapungua. Hutakiwi
kuwa mtaalamu wa mpangilio wa vitu ili kuweza kuwa na mipangilio mizuri zaidi
mwaka huu. Haijalishi ni mpangilio kwenye kabati lako la nguo, chumba cha
kulala, meza yako ya ofsini au hata kwenye akaunti yako ya barua pepe.
Utajisikia vizuri utakapoweza kuchambua na kuweka vitu kwenye mpangilio.
Wengi wetu tunashawishiwa na vitu, matukio na watu
ambao tuko karibu nao kwa hiyo inaleta mantiki kabisa kuanza kuweka mpangilio
na kuondoa mlundikano kwenye chumba chako cha kulala. Ondoa vitu vyote ambavyo
kwakweli havihusiki kwenye chumba hiki kwa mfano vifaa vya mazoezi, vitu vya
ofisini na kadhalika. Usisahau kuondoa mlundikano mvunguni.
Weka mpangilio kwenye kabati lako la nguo. Hatua ya kwanza ni kuondoa kila kitu. Hapo
ndio utakapoweza kuona una nini. Vitu kwenye kabati lako hili vitakuwa kwenye
makundi manne: vya kubaki, vya kugawa, vya kutupa (takataka) na vya kuhamishia
eneo lingine yaani vile ambavyo havitakiwi kuwa kwenye kabati la nguo. Andaa
maboksi na raki za viatu, na usisahau mifuko ya plastiki kwa ajili ya kuwekea
vitu vya kugawa. Kuwa mkweli, je ni kweli kuwa unahitaji na kupenda kila kitu?
Kama nguo, kiatu ama kitupio hujakiona, hujakihitaji au hujakivaa ndani ya mwaka mmoja basi kitupilie mbali.
Kila nguo iliyoko kwenye kabati lako la nguo jiulize
maswali matatu: Je inakutosha? Ulishaivaa miezi 12 iliyopita? Ina thamani ya
kuifanya iwe kwenye kabati lako la nguo? Kama majibu ni hapana basi iweke
kwenye fungu la kugawa.
Endelea na mchakato huo huo kwenye nguo na viatu vya
mwenzi na watoto wako. Utakapomaliza zoezi hili utajikuta una mzigo mkubwa wa
vitu vya kugawa na hata taka nyingi.
Vile vile kwenye ofisi yako iwe ni ofisi ya nyumbani
au ya mahali pa kazi basi kama msemo wa safari inaanza kwa hatua moja tenga saa
moja ya saa yako ya kazi kwa kupitia nyaraka moja moja. Amua ni ipi ya
kutupa, ni ipi ya kumwagiza mfanyakazi
wa chini yako aifanyie kazi, ni ipi ya masjala na mwisho ni ipi ya wewe
kuifanyia kazi mara moja. Jiwekee utaratibu wa kumeneji nyaraka zako. Kama unadhani
hailipi kutumia muda wako fulani kuweka vitu kwenye mpangilio basi wacha uone
ni vipi vitu vilivyolundikana vinaweza kukuvuruga katika maisha yako ya kila
siku.
Kwenye droo za kabati lako la sebuleni. Je
kumejaa daftari za zamani na vitabu vya jinsi ya kuendesha biashara vya nyakati
ukisoma elimu ya juu na risiti za bili zilizolipwa miaka mingi iliyopita? Au pengine
droo hizo zimejaa midoli na vigari vya watoto wako ambao sasa wako kidato cha
pili? Ikiwa ni hivyo basi akili ni lazima ivurugike. Vitu visivyo kwenye
mpangilio na uhitaji wa wakati husika vinakunyonya nguvu taratibu. Na hata
kutafuta kitu kwenye mlundikano ni mbaya zaidi.
Ingia jikoni, hali ya jiko lako ndio hali ya afya
yako. Kwahiyo ihurumie afya yako kwa kusafisha na kuweka mpangilio kwenye jiko
lako! Safisha kwenye jokofu, punguza viporo vilivyoshamiri huko. Safisha jiko
lenyewe, masufuria na vikaangio. Safisha kwenye madroo yote na ondoa chupa zote
zisizohitajika.
Kama kawaida mlango wa mbele ni kivutio cha nyumba
na ni eneo unaloanzia kupata nguvu unapoingia nyumbani. Zipe fahamu zako unafuu
kwa kuweka mazingira ya mlango wa mbele kwenye mpangilio ili kuondoa msongo wa
mawazo. Ondoa vitu kwenye mlango huo ambavyo kwakweli havitakiwi pale kwa mfano
doo la uchafu, vyungu vya maua vyenye nyufa na kadhalika. Lete muonekano wa
umaridadi kwenye eneo hili la mbele ya nyumba.
Tafuta njia ya kushughulika na barua na bili
zinazokuja nyumbani ili zisisambae kila mahali. Droo dogo kwenye kabati lako la
nguo linaweza kuwa suluhisho la kuhifadhi barua zako kama hamna nafasi eneo
lingine.
Sababu ya watu wengi kutopenda kuweka vitu katika
mpangilio na kuondoa vile visivyotumika sio ni kwa vile inahitaji nguvu na
muda. Sababu ya ukweli ni kuwa mchakato mzima una hisia kama vile ni tiba, na
ni zoezi linalohitaji stamina. Ila habari njema ni kuwa mara ufanyapo zoezi
hili na kuweka mkakati na miundombinu ya kuwezesha vitu kutolundikana tena basi
maisha yanakuwa rahisi kwako kwani utazungukwa na mazingira freshi na safi.
Zingatia kuweka mpangilio, kuondoa mlundikano ili
kufanya maeneo mbalimbali ya nyumbani kama yalivyoainishwa hapo juu kuwa
nadhifu kwa kuwa yameunganika na ustawi wako hapo nyumbani. Watafiti wa
kisayansi walishagundua kitambo kuwa
mlundikano wa vitu humsababishia binadamu kutozingatia mambo na pia kuwa na
uwezo mdogo wa kuchanganua mambo.
Makala
hii imeandikwa na Vivi O. Machange. Kwa maoni niandikie viviobed@yahoo.co.uk au kwa simu 0755 2000 23
No comments:
Post a Comment