Hatua
za kupitia ili kufanikisha kupamba nyumba yako
Wazo la kuanza kupamba ndani ya nyumba ni la
kusisimua au kuogopesha kutegemea na uzoefu, bajeti, ladha na pia muda wako.
Kabla ya kuanza kupamba chumba kwanza kihakiki. Na
njia nzuri ya kuhakiki chumba ni kuondoa kila kitu. Ukishaondoa samani, pazia
na sanaa za ukutani basi unaiona sehemu kwa uwazi zaidi. Chunguza paa, ukuta
madirisha na eneo lenye mbao. Je kuna kitu kinahitaji marekebisho? Mara
nyingi bafuni na jikoni ndio kunakuwa na hitaji la marekebisho makubwa.
Vipengele hivi vitatu vya paa, ukuta na sakafu ni kitovu cha muonekano wa
chumba. Hakikisha unafanya marekebisho
yote yanayohitajika kabla ya kuanza kupamba.
Kama hujawahi kupamba kabisa, unaweza kujihisi kuwa
hujui ni vipi au ni wapi pa kuanzia. Kama kupamba ni kofia ya zamani kwako,
unaweza usijue ni wapi pa kumalizia. Lakini baada ya yote kusemwa na kufanyika,
unataka muonekano mpya na unataka kuanza kazi ya kutafuta muonekano huo.
Kuna swali dogo sana juu ya ni kitu gani ufanye mwisho,
lakini kuna vitu lukuki vya kuanzia. Kwa kuwa kupaka rangi kama nyumba
ilishapakwa rangi kabla basi inakuwa sio kazi kubwa na rangi zipo za aina
nyingi, unatakiwa kusubiri kununua rangi hadi uwe na vitu vingine vyote.
Lakini ni nini ufanye kwanza? Je ununue fenicha za
kujaza chumba au ununue hicho kizulia kinachokuvutia? Je umeshachagua kitambaa
cha kifahari utakachokitumia? Ni kweli kuwa unaweza kuanzia popote unapotaka na
kuunganisha yote pamoja kwenye mpango mmoja.
Ila kiukweli inasaidia kama unaanza kwa mpango, vitu kinachokuhamasisha
na mandhari ya rangi.
Tafuta vyanzo vya hamasa yako na anza kuufanyia kazi
mradi wako huo wa kupamba. Utafurahi kuwa ulichukua muda kupanga.
Weka mpango wako kwenye karatasi. Ni kama tu
mchanganuo wa biashara ni lazima uweke maono yako kwenye maandishi. Weka kwenye
maandishi na tekeleza. Pambanua staili yako halafu chagua mpango wa rangi kwa
mandhari yako. Je unachagua mapambo ya kizamani, ya kitamaduni au mapambo ya
kisasa. Chukua muda kupambanua vipengele
vya staili inavyopenda na fanya mpango wa kuvileta nyumbani kwako.
Anza na ulichonacho. Sio kila mtu (kwa kweli ni watu
wachache sana) wanaoweza kuanzia ziro, chumba kitupu na kuanza kupamba. Wengi
wetu tayari tuna fenicha kadhaa au nyumba ina sakafu ya marumaru au vitu fulani
fulani kwenye ujezi ambavyo usingependa kuvitupilia mbali kwenye upambaji wako.
Kama kuna vitu unavipenda vizingatie na kuvifanya maalum. Kama kuna vitu
usivyopenda lakini huwezi kuvibadili, tafuta njia za kuvififisha kwenye eneo
lako jipya ulilopamba.
Kama una vitu vya kupambia, hivi vinaweza kuwa
kianzio cha mpango wako wa kupamba. Kwa kuzingatia mpangilio wa rangi na
mandhari ya kupambia unaweza kupambanua mwanzo wa mradi wako huo wa kupamba.
Labda ulichonacho cha kuanzia ni sanaa za ukutani,
mara nyingi sanaa unayochagua itasema ni nini unapenda. Kwa mfano kama unapenda
picha za rangi nyeusi na nyeupe huenda ikakubidi upambe ndani mwako kwa mtindo
wa kisasa zaidi.
Kuna rangi unayopendelea zaidi? Kama una rangi
unayopendelea itumie ikuongoze kwa mpangilio wa rangi za mapambo yako ya ndani.
Itumie kwenye vitupio vyako. Chagua vitambaa vyenye rangi na michoro hiyo
unayopendelea. Tumia rangi zilizopo kwenye vitambaa hivyo kupambanua rangi
utakazotumia kwenye ukuta, kwenye fenicha na kwenye vitupio vingine utakavyochagua kama vile taa za vivuli na
kadhalika.
Au anza na kizulia. Kwa rangi na michoro ya kitupio cha kizulia
unaweza kuweka vipengele vingine rahisi kwa kuzingatia kizulia badala ya
vitambaa au rangi za kuta
Kufumba na kufumbua unaanza kuona ndoto yako
ikikamilika, nyumba iliyovishwa rangi na sanaa zilizopangwa zikapangika.
Makala
hii imeandaliwa na Vivi O. Machange. Kwa maoni niandikie barua pepe viviobed@yahoo.co.uk au kwa simu 0755 2000 23