Jinsi
ya kununua kitanda kitakachokufaa
Katika maisha haya ya kuchoka sana, kitanda cha
kukupa starehe ndio kila mmoja wetu anahitaji. Baada ya kazi nyingi mno na
uchovu, sote tunataka usiku wa mapumziko na starehe. Kitanda cha namna hii
hakikupi tu hamasa ya kuanza siku ya kesho yake bali pia kinakupa nguvu ya
kupambana na mabaya ya maisha. Inawezekana hukuwahi kufikiria hivi kabla,
lakini ni lazima ukubali kuwa kitanda ni moja kati ya vitu muhimu zaidi kwenye
maisha yetu. Hii ndio maana kabla ya kununua kitanda unatakiwa kuwa na uhakika
wa unachohitaji kutokana na kitanda hicho.
Starehe, uimara na mtindo ni vitu vya kuzingatia katika kujipatia
kitanda kitakachokufaa. Fuatana nami katika makala hii ujionee jinsi ya
kujipatia kitanda sahihi kwako.
Inawezekana umeshaona aina kadhaa za vitanda kwa nyumbani
kwa majirani zako au kwa rafiki, fikiria kwa undani kama kuna mtindo ambao
umekugusa. Ni vyema kununua kile ambacho moyo wako umekuwa ukitamani. Baadhi ya watu wanapendelea vitanda vya mbao
na wengine wanakuwa na furaha wakiwa na vitanda vya chuma.
Mara zote cheki ni aina gani ya godoro litakalofaa kwa
kitanda unachotaka kununua kwa kuwa mengine yanaendana na muundo wa kitanda wakati yapo ya kufiti
kwenye kitanda chochote. Pia hakikisha saizi ya godoro lako litatosha kwenye
msingi wa kitanda husika.
Ni kawaida kwa mtu kuwa na ufahamu binafsi wakati
anajaribu kitanda kwenye duka la muuzaji, na wanunuzi wengi huwa wanajaribu
kitanda kwa kukilalia mara moja na kuamka. Lakini ili uwe na uhakika kuwa
kitanda na godoro ni sahihi kwako, unatakiwa ulale kwa pozi mbalimbali kwenye
kila kitanda kama unavyolala usiku kwa
muda wa si chini ya dakika tano.
Kama umechagua kitanda cha aina fulani, hakikisha unacheki kabisa
hali yake ya starehe. Kama kitanda hakikupi starehe hutakaa ukitumie kwa
furaha. Haina maana kununua kitanda hicho ambacho hakitakuwa na matumizi kwako
hapo baadaye kwa sababu tu eti umependa mtindo na muundo wake. Tafuta kingine
ambacho kitakupa starehe unayoitaka. Kwa mfano, ni kuwa unatakiwa kuchagua
kitanda ambacho kina urefu wa inchi 4-6 zaidi ya urefu wa mtu mrefu zaidi atakayelalia
kitanda hicho.
Uimara wa kitanda husika ni kigezo muhimu.Ni ukweli
kuwa unawekeza hela nyingi kwenye kitanda, sasa ina maana gani kununua ambacho
ni dhaifu na kitavunjika siku za karibuni. Kwahiyo ni vyema ukawekeza hela zako
hizo kwa kitanda imara ambacho kitadumu miaka nenda rudi kwani kitanda sio kitu
cha kununua kila mara.
Zaidi ya yote swali muhimu la kujiuliza ni kuwa ni
kitanda cha ukubwa gani kitatosha chumba chako kwa nafasi iliyopo. Kama kitanda
hiki ni kwa ajili yako na mwenzi wako ni vyema mkakubaliana wote wawili kabla
ya kufanya maamuzi ya ununuzi. Ni lazima mfikirie pia kama kunaweza kuwa na
kitanda kitakachofaa zaidi ya hicho mnachotaka kununua. Kama eneo ni dogo ni
vyema mkafikiria kununua kitanda chenye sehemu ya kuhifadhia. Kitanda cha
kuhifadhia hakina tofauti kubwa na hivi vya kawaida vilivyozoeleka na wengi
bali tu ni kuwa kina sehemu ya kuhifadhia mithili ya droo chini ya godoro na
vingine vina shelfu zilizojengewa kwenye ubao wa kichwani hivyo kuondoa haja ya
kuweka vimeza vya kando.
Mwisho kabisa kama una matatizo ya mgongo aina ya
kitanda unachohitaji nayo inahusu. Kama
kuna aina yeyote ya kitanda itakayokusaidia kwa hali yako hiyo basi nunua. Kama
mtu ni mlemavu au mgonjwa na anatafuta
kitanda cha kumsaidia katika hali yake hiyo ni wazo zuri. Kitanda ni kati ya
vitu vya manunuzi ya hela kubwa yanayofanywa kwa matumizi ya nyumbani. Sio tu
kinawezesha kupata usingizi mnono bali kinahusika pia na afya ya mgongo wako.
Maumivu ya mgongo yanaweza kufanya maisha ya watu kuwa ya taabu, bali kuwa na kitanda sahihi
kwa mgongo wako italeta tofauti kubwa.
Manunuzi ya kitanda imara ni ya pesa nyingi, kwa
hivyo fikiria kwa kina juu ya nini unachotaka kabla ya kufanya uamuzi.
Unapendelea mbao, chuma, ngozi ama kitambaa? Hakikisha unalinganisha na kushindanisha
mauzo ya vitanda mbalimbali kabla ya kufanya
uamuzi wa mwisho.
Makala
hii imeandaliwa na Vivi O. Machange. Kwa maoni niandikie barua pepe viviobed@yahoo.co.uk au kwa simu 0755
200023
Vivi asante kwa elimu nzuri ya mambo haya, mara nyingi tunapuuzia vitu hivi.Endelea kutuelimisha mama!!.Vale
ReplyDelete