Tuesday, February 26, 2013

My article for newspaper: Hatua za kupamba







Hatua za kupitia ili kufanikisha kupamba nyumba yako

Wazo la kuanza kupamba ndani ya nyumba ni la kusisimua au kuogopesha kutegemea na uzoefu, bajeti, ladha na pia muda wako.

Kabla ya kuanza kupamba chumba kwanza kihakiki. Na njia nzuri ya kuhakiki chumba ni kuondoa kila kitu. Ukishaondoa samani, pazia na sanaa za ukutani basi unaiona sehemu kwa uwazi zaidi. Chunguza paa, ukuta madirisha na eneo lenye mbao. Je kuna kitu kinahitaji marekebisho? Mara nyingi bafuni na jikoni ndio kunakuwa na hitaji la marekebisho makubwa. Vipengele hivi vitatu vya paa, ukuta na sakafu ni kitovu cha muonekano wa chumba.  Hakikisha unafanya marekebisho yote yanayohitajika kabla ya kuanza kupamba.

Kama hujawahi kupamba kabisa, unaweza kujihisi kuwa hujui ni vipi au ni wapi pa kuanzia. Kama kupamba ni kofia ya zamani kwako, unaweza usijue ni wapi pa kumalizia. Lakini baada ya yote kusemwa na kufanyika, unataka muonekano mpya na unataka kuanza kazi ya kutafuta muonekano huo.

Kuna swali dogo sana juu ya ni kitu gani ufanye mwisho, lakini kuna vitu lukuki vya kuanzia. Kwa kuwa kupaka rangi kama nyumba ilishapakwa rangi kabla basi inakuwa sio kazi kubwa na rangi zipo za aina nyingi, unatakiwa kusubiri kununua rangi hadi uwe na vitu vingine vyote.
Lakini ni nini ufanye kwanza? Je ununue fenicha za kujaza chumba au ununue hicho kizulia kinachokuvutia? Je umeshachagua kitambaa cha kifahari utakachokitumia? Ni kweli kuwa unaweza kuanzia popote unapotaka na kuunganisha yote pamoja kwenye mpango mmoja.  Ila kiukweli inasaidia kama unaanza kwa mpango, vitu kinachokuhamasisha na mandhari ya rangi.

Tafuta vyanzo vya hamasa yako na anza kuufanyia kazi mradi wako huo wa kupamba. Utafurahi kuwa ulichukua muda kupanga.
Weka mpango wako kwenye karatasi. Ni kama tu mchanganuo wa biashara ni lazima uweke maono yako kwenye maandishi. Weka kwenye maandishi na tekeleza. Pambanua staili yako halafu chagua mpango wa rangi kwa mandhari yako. Je unachagua mapambo ya kizamani, ya kitamaduni au mapambo ya kisasa.  Chukua muda kupambanua vipengele vya staili inavyopenda na fanya mpango wa kuvileta nyumbani kwako.

Anza na ulichonacho. Sio kila mtu (kwa kweli ni watu wachache sana) wanaoweza kuanzia ziro, chumba kitupu na kuanza kupamba. Wengi wetu tayari tuna fenicha kadhaa au nyumba ina sakafu ya marumaru au vitu fulani fulani kwenye ujezi ambavyo usingependa kuvitupilia mbali kwenye upambaji wako. Kama kuna vitu unavipenda vizingatie na kuvifanya maalum. Kama kuna vitu usivyopenda lakini huwezi kuvibadili, tafuta njia za kuvififisha kwenye eneo lako jipya ulilopamba.
Kama una vitu vya kupambia, hivi vinaweza kuwa kianzio cha mpango wako wa kupamba. Kwa kuzingatia mpangilio wa rangi na mandhari ya kupambia unaweza kupambanua mwanzo wa mradi wako huo wa kupamba.

Labda ulichonacho cha kuanzia ni sanaa za ukutani, mara nyingi sanaa unayochagua itasema ni nini unapenda. Kwa mfano kama unapenda picha za rangi nyeusi na nyeupe huenda ikakubidi upambe ndani mwako kwa mtindo wa kisasa zaidi.
Kuna rangi unayopendelea zaidi? Kama una rangi unayopendelea itumie ikuongoze kwa mpangilio wa rangi za mapambo yako ya ndani. Itumie kwenye vitupio vyako. Chagua vitambaa vyenye rangi na michoro hiyo unayopendelea. Tumia rangi zilizopo kwenye vitambaa hivyo kupambanua rangi utakazotumia kwenye ukuta, kwenye fenicha na kwenye vitupio vingine  utakavyochagua kama vile taa za vivuli na kadhalika.

Au anza na kizulia. Kwa  rangi na michoro ya kitupio cha kizulia unaweza kuweka vipengele vingine rahisi kwa kuzingatia kizulia badala ya vitambaa au rangi za kuta
Kufumba na kufumbua unaanza kuona ndoto yako ikikamilika, nyumba iliyovishwa rangi na sanaa zilizopangwa zikapangika.

Makala hii imeandaliwa na Vivi O. Machange. Kwa maoni niandikie barua pepe viviobed@yahoo.co.uk au kwa simu 0755 2000 23

No comments:

Post a Comment