Jinsi
ya kuwezesha zulia lako lidumu na kuwa maridadi kila wakati
Kwa jinsi ambavyo utaweza kuweka zulia lako safi
ndivyo litakavyoweza kudumu. Kwa madhumuni ya makala hii zulia litamaanisha
lile la kufunika ukuta kwa ukuta na vitupio vya zulia ama vizulia ni yale
mazulia madogo madogo ya kuweka maeneo yaliyoainishwa kwa mfano chini ya meza
ya kahawa na kadhalika.
Sasa basi ingawa zulia safi na maridadi ni sehemu
muhimu sana ya muonekano wa nyumba, kuweka jipya mara kwa mara ni gharama
kubwa. Makala hii itakuonyesha ni kwa jinsi gani unaweza kufanya zulia na
vizulia vyako vidumu na kuonekana vipya kwa muda mrefu.
Uchafu unafanya nyuzi za zulia lako zichakae.
Safisha kwa mashine ya upepo ili kunyonya mchanga na vumbi kwenye zulia lako
kila siku kwenye zile sehemu zinazokanyagwa kila wakati na walau mara moja au
mbili kwa wiki kwenye zile sehemu zisizokanyagwa mara kwa mara. Asilimia 80 ya
uchafu kwenye zulia ni taka kavu kwahivyo zinadakwa moja kwa moja na aina hii
ya usafishaji wa zulia. Wakati wa kutumia mashine hii hakikisha unatumia brashi
sahihi kuendana na unene na urefu wa manyoya ya zulia lako na pia iwe imesetiwa
kwa urefu sahihi kwani kama utaipitisha juu juu tu haitakuwa inasafisha
ipasavyo na kama iko chini sana inaweza kuharibu zulia kwa kung’oa manyoya.
Kumbuka kusafisha mfuko wa taka wa mashine ili kuiwezesha kufanya kazi vizuri.
Maeneo ya mlangoni weka vizulia vidogo vya kukanyagia kabla mtu hajaingia
ndani. Utunzaji huu wa mara kwa mara utaboresha muonekano mzima na kuongeza
maisha ya zulia lako .
Teua maeneo ya kulia chakula. Matone ya vyakula
yanaleta mafuta kwenye zulia ambapo haya mafuta yanavuta taka nyingine na
kufanya zulia lipoteze mvuto. Kwa jinsi ambavyo vyakula vinaliwa maeneo
yasiyokuwa na zulia ndivyo kunavyokuwa na nafasi kubwa ya kuepuka matone matone
kwenye zulia. Weka sera ya kwamba
vitafunwa vyote vitaliwa jikoni au mezani ili hata kama ni kwa watoto wadogo
wakae mezani mabaki yadondoke mezani na sio juu ya zulia. Hata kama familia
yako itaandamana kuhusu sera hii, bado ni njia pekee kuzuia matone yasifanye
madoa kwenye zulia lako. Kama una watoto hakikisha kuwafahamisha wakujulishe
mara wamwagapo kitu kwenye zulia ili usafishe mara moja. Michuzi, chokoleti na
juisi ni mauaji kwenye zulia lako la thamani. Kama chakula kitapata njia ya
kuelekea kwenye zulia basi hakikisha unasafisha mara hiyo hiyo. Tumia povu la
shampoo ya kusafishia zulia ili kuepuka kulilowesha chepechepe na sugua kwa
brashi laini kuondoa uchafu wote. Mabaki yoyote yatavuta uchafu mwingi zaidi.
Usiruhusu uchafu kuingia ndani. Weka mazingira ya
nje ya nyumba na njia zote za kuingilia ndani safi. Hii itapunguza sana kiasi
cha uchafu unaoweza kuingia ndani ya nyumba. Uchafu wote ubaki nje ya nyumba
kwani uchafu unazeesha zulia. Ingawa unaweza kujisikia ugumu wa kuwaambia wageni
wako wavue viatu kuingia ndani, kuacha viatu mlangoni kunapunguza kiasi kikubwa
cha uchafu ambao ungeingia ndani. Kuvua viatu kabla ya kuingia ndani ni tabia
nambari moja ambayo sio tu itapunguza ratiba za kusafisha zulia bali pia
kuongeza maisha ya zulia lako. Chukua muda kuweka njia za kuingilia ndani safi.
Ni vyema kuhamisha fenicha zako kila baada ya muda fulani
fulani ili kupunguza shurba kwa yale maeneo yanayokanyagwa mara kwa mara. Zulia
linachakaa haraka zaidi maeneo watu wanapokanyaga kila mara. Badilisha muonekano
wa vyumba ambapo utaleta njia mpya za kupitia ili kupumzisha baadhi ya maeneo
kwahivyo zulia lako kuwa jipya maeneo yote na sio tu maeneo kadhaa. Weka
vizuizi kwenye miguu ya fenicha hasa zile nzito
kuzuia zisiharibu zulia. Kama ukihamisha fenicha na kukuta kuwa imeweka
alama kwenye zulia chukua kipande cha barafu weka juu ya hilo eneo acha iyeyuke na polepole sugua kwa brashi
laini. Kutegemea na jinsi nyumba yako ilivyo bado pengine kuna maeneo ambayo
yanabakia kukanyagwa zaidi hata kama ungebadisha badilisha fenicha kiasi gani.
Hivyo basi maeneo haya yanayokanyagwa zaidi tupia vizulia.
Maeneo ya zulia chini ya mlango wa kutokea nje huwa
yanajenga mstari wa uchafu. Hii ni kwa ajili nje kuna uchafu mwingi wa mavumbi
na udongo ambao ukinyonywa na zulia hufanya mstari huo. Ukienda kwenye maduka
ya vifaa vya usafi wa majumbani utapata dawa maalumu za mazulia za kuondoa
uchafu wa aina hii. Wekeza kwenye zulia nzito za kukanyagia mlangoni kuzuia
uchafu wa ziada usiingie ndani.
Uji wa mishumaa hung’ang’ania sana kwenye zulia kwa
hivyo epuka mshumaa unaowaka kudondosha uji wake moja kwa moja kwenye zulia.
Kuondoa uzi au nyoya lililochomoza tumia mkasi
kukata badala ya kuvuta ambapo kwa kuvuta unaweza vuta zaidi ya uzi mmoja hivyo
kuharibu zulia.
Maeneo ya zulia yanayopigwa na jua moja kwa moja,
usiweke pazia wazi ili kuzuia kupauka au kufanya rangi ya kahawia.
Tembea kwenye zulia ukiwa umevaa soksi. Wakati
kutembea bila viatu itafanya zulia lidumu, hutakiwi kutembea kwenye zulia lako
miguu mitupu. Mafuta na majasho yanayotoka kwenye ngozi ya miguu yanang’ang’ania
kwenye zulia na kuvuta takataka zaidi.
Pamoja na yote hayo hapo juu ya kuwezesha zulia lako
liwe maridadi kila wakati na lidumu, jinsi lilivyowekwa pia inahusu. Hakikisha
unatafuta wawekaji wenye ujuzi wa kuweka zulia hasa lile la ukuta kwa ukuta.
Safisha zulia lako usafi wa kina wa mashine ya umeme ya mvuke ya kusafishia
mazulia walau mara moja kwa mwaka. Huduma hii utaipata kwa wataalam wa usafi wa
mazulia na wala huna haja ya kuwekeza kwenye mashine hii kwa kuwa utahitaji
huduma yake mara moja tu kwa mwaka.
Makala
hii imeandaliwa na Vivi O. Machange. Kwa maoni niandikie viviobed@yahoo.co.uk , simu 0755 200023