Jinsi
ya kupata sofa zitakazokufaa
Kama unataka kupata kiusingizi cha mchana, kuangalia
filamu au hata kujisomea kitabu, sofa mara nyingi ni sehemu panapopendwa zaidi
kwa wanafamilia. Sofa ni fenicha muhimu nyumbani kwako na mara uinunuapo utakaa
nayo walau kwa miaka mitano au zaidi. Kwa hivyo ni muhimu kuchagua sofa sahihi
unapoamua kununua moja. Makala hii itakupa dondoo za kukuwezesha kununua sofa
sahihi! Endelea kusoma.
Kila nyumba ni matokeo ya ndoto ya anayeimiliki,
ambapo maslahi na ladha za mmiliki huyo zitaonekana kila kona ya nyumba hiyo.
Iwe ni rangi au kifaa cha fenicha kitakuwa kimepata baraka za mmiliki kuwa
ndani ya nyumba yake. Ni ukweli kuwa kila chumba kinaweza kuwekwa katika hali
ya juu kabisa kwa kuwekwa fenicha na samani sahihi. Sofa linachukua sehemu
muhimu kubadilisha chumba kilichozubaa kuwa cha muonekano wa kuvutia. Kuna aina
nyingi ya sofa ambazo unaweza kuchagua kuanzia za kuweka sehemu iliyonyooka
hadi sehemu ya mduara na kwenye kona, na kazi yako haitakuwa rahisi kama
unataka sofa sahihi za kuendana na ndani mwako, kufanya sebule yako au chumba kingine rasmi kiwe cha
kuvutia. Kuchagua sofa sahihi haiwezi kuwa kazi ngumu kwako kama unajua baadhi
ya miongozo muhimu.
Kabla hujapanga kununua sofa, unatakiwa ujue ukubwa
wa chumba ukoje na unataka sofa ichukue nafasi kiasi gani. Jiulize kama sofa
husika zitatosha familia yako yote ama laa. Matumizi ya nafasi ni kipaumbele
kati ya vipengele vya kuzingatia kabla hujanunua sofa.
Wakati unapoenda kutafuta sofa za kununua, tafuta
zile zenye muonekano na mtindo ambao utaoana vyema na samani nyingine zilizopo
hapo chumbani. Kuna chaguzi kadhaa kutoka sofa za kitamaduni hadi za kisasa.
Unaweza ukapata zilizotengenezwa tayari au unaweza kutoa oda kwa waseremala
wakakutengenezea kwa kadri ya hitaji lako. Sofa yoyote iwe ni ndefu, ama ya
kona ama ya mtindo wa sofa kitanda inaweza kuleta mvuto kwenye chumba chako.
Rangi na michoro ya sofa vinahusu, mara nyingi rangi
ya sofa inapendekezwa iwe sawa na ya ukuta wa chumba. Hata hivyo kama unataka
kuongeza mtindo na staili chagua sofa zenye rangi na michoro iliyokolea. Hii
itafanya macho yavutwe kuzitizama badala ya kuwa tu kama mojawapo ya fenicha
chumbani. Zingatia ladha na matamanio yako binafsi vilevile.
Chagua sofa zenye kitambaa kinachoendana na maisha
unayoishi. Kwa mfano usithubutu kuchagua kitambaa cheupe kama una watoto
wadogo. Kuwa na wanyama kama vile paka na mbwa ndani ya nyumba ni mapenzi ya
mtu binafsi na kama wewe ni mmoja wa wenye mapenzi hayo si busara kuchagua sofa
za kitambaa cheupe kwani wanyama hawa wanaweza kuleta maafa kwenye sofa zako za
gharama. Kwa hivyo zingatia rangi na ubora wa kitambaa cha sofa kabla ya
kufanya manunuzi.
Kabla ya kununua sofa zijaribu kwa kuzikalia wewe
mwenyewe. Tafuta mawazo ya mtu wa pili kama itahitajika. Kama wakati wa kukaa
sofa zinatoa mlio ni dalili kuwa hazijatengenezwa vizuri. Angalia kama kiti
kinaendana na urefu wa miguu yako na eneo la kuegemezea mkono. Hata hivyo kadri
sofa inavyotumika ndivyo inavyokaa vyema na kukidhi mahitaji.
Wakati wa kuchagua sofa hakikisha kuwa fremu zake ni
imara na gundi za mbao zimesambazwa na kugundishwa vyema. Ubora wa mbao ni
jambo la kuzingatia sana hasa kama unaweka oda ya kutengenezewa. Mara kadhaa waseremala wanaweka
mbao za matenga ya nyanya na kwakweli mbao hizi si imara kwa matumizi ya sofa.
Kwa hivyo mara baada ya kukabidhiwa sofa zako na kuzipeleka nyumbani kwa ajili
ya matumizi hazikai hata miezi mitatu zinavunjika vunjika.
Mito ambayo haijaunganishwa kwenye sofa ni mizuri
zaidi kwa starehe na pia urahisi wa kuvua foronya na kuzifua. Mito iwe imejazwa
ujazo sahihi ili isibonyee na kusinyaa kadri siku zinavyoenda.
Mwisho wa yote kumbuka kuwa usinunue sofa kwa ajili
tu ya kukalia, bali pia kwa ajili ya starehe!
Makala
hii imeandaliwa na Vivi O. Machange. Kwa maoni niandikie viviobed@yahoo.co.uk au kwa simu 0755 2000 23
No comments:
Post a Comment