Umuhimu
wa feni ya stovu
Jiko ni kitovu cha nyumba ya kisasa. Jinsi nyumba inavyozidi kuwa za kisasa, ndivyo inavyokuwa na jiko lenye
vifaa na muonekano wa kisasa pia. Katika makala hii jiko litamaanisha chumba
chenyewe na stovu itamaanisha pale panapobandikwa sufuria. Ili kufanikisha
uingizaji wa hewa jikoni nyumba za kisasa zina vifaa vya jiko vya kisasa.
Mojawapo ya vifaa hivi ni feni ya stovu.
Feni ya stovu ni kifaa kinachofungwa juu ya stovu
kwa ajili ya kukusanya moshi, harufu, mvuke na ghasia nyingine zizalishwazo
hewani wakati wa kupika. Kwa ufanyaji kazi wa kuridhisha feni ya stovu
inatakiwa kuwa na upana sawa na wa stovu yenyewe. Kuna feni ambazo zinanyonya
moshi na mvuke na kutoa nje ya nyumba na kuna ambazo zimetengenezwa kwa jinsi ambayo
moshi na harufu zinanyonywa ndani kwa ndani hata kama mfumo wa kutoa nje ya
nyumba haupo. Kwa hiyo usijali kuwa jiko lako halina mfumo wa kukuwezesha kutoa
uchafu huo wa mapishi nje ya nyumba, bado unaweza kufunga feni hii aina ya pili
yaani ya kuvuta uchafu ndani kwa ndani.
Ndio, nyumba yako inaweza kuwa na harufu za mapishi
ambazo hazikukoseshi faraja lakini ni ukweli kuwa harufu hizo sio nzuri kwa
afya yako. Wakati unapopika, mvuke, gesi na moshi zinaachiliwa hewani kama
uchafu na kwenda kutulia kwenye fenicha, makabati, nyavu za jiko na hata
ukutani. Uchafu huu unaharibu samani za nyumba yako na pia hewa ya jikoni.
Inawezekana jiko la bibi yako lilikuwa kwa jinsi
ambayo uingizaji wa hewa ulikuwa rahisi, lakini kwa nyumba za kisasa zenye jiko
humo humo uingiaji wa hewa jikoni unaweza kuwa wa taabu. Kwa maana hiyo ni
vyema kufunga feni ya stovu ili kuwezesha hewa safi ndani ya nyumba. Kwa jinsi ambavyo nyumba zetu zinakuwa kubwa,
jiko linakuwa ndio sehemu ya kuwezesha starehe ndani ya nyumba kuanzia kuandaa chakula cha wageni
jumapili na vyakula vingine vyote vya familia. Jifunze njia sahihi za kuwezesha
uwepo wa hewa safi ndani ya jiko lako mara zote.
Hewa safi jikoni wakati wa kupika ni usafi, na ni afya
kwa wakaaji na hufanya mazingira na
harufu safi ya nyumba kwa ujumla. Wakati wa kupika kwa gesi, hewa ukaaa
inazalishwa hewani kama uchafu kutokana na kuungua kwa hiyo gesi ya kupikia.
Hewa hii inaweza kusababisha matatizo kadhaa kama maumivu ya kichwa na hata
kifo. Kwa hivyo leo hii kuna njia nyingi za uwekaji wa hewa safi ndani ya jiko
na mojawapo ni hii ya kufunga feni ya stovu. Ukienda kwenye maduka ya vifaa vya
umeme ukaulizia feni ya stovu huenda usieleweke kirahisi. Jina ambalo
limezoeleka na ni maarufu kwa wauzaji wa vifaa hivyo ni “hood” na huwa zipo za
ukubwa mbalimabali kuendana na ukubwa wa stovu yako. Kama nilivyosema awali feni
hizi zipo ambazo uwekaji wake unatakiwa uwe ulikuwa kwenye mpango wa ujenzi wa
jiko ambapo hizi ni zile zenye bomba maalumu la kutoa moshi na harufu nje ya nyumba,
na zipo zile ambazo harufu mvuke na moshi hunyonywa ndani kwa ndani na chujio maalumu zilizojengewa kwenye feni
hiyo kwa hivyo hata kama mpango wa jiko haukuweka mfumo wa feni ya stovu bado
utaweza kuifunga feni yako.
Feni ya stovu inafungwa kwa jinsi ambayo gesi,
mvuke, moshi na mafuta vinavyotoka kwenye hiyo hewa ya moto wakati wa kupika
zinadakwa na feni hiyo. Upana wa feni unavyozidi upana wa jiko ndivyo uchafu
mwingi unavyodakwa. Moja ya nyanja muhimu sana kwenye kuwa na hewa safi ndani
ya nyumba ni kwa kudhibiti kiasi cha unyevu. Kwa kuwa ni unyevu mwingi
unaotokana na mapishi ni vyema kukumbuka kuwasha feni yako kila unapopika. Mfumo
wa uingizaji hewa kwenye nyumba yako kwa jinsi ulivyowekwa wakati wa ujenzi kwa maana ya madiridha na
kadhalika unaweza kudhibiti kiasi fulani cha unyevu, lakini kama huna feni ya
stovu utaanza kusikia kiwango cha hewa safi ndani ya nyumba kikishuka wakati wa
kupika. Unyevu ukiruhusiwa kujijenga unazalisha vumbi, ukurutu wa mafuta, uozo
na hata fangasi ambavyo huweza kusababisha maradhi ya ngozi, macho na hata matatizo
kwenye mfumo wa kupumua wa binadamu.
Ingawa kufungua madirisha inaweza kusaidia kuondoa
moshi na harufu kwa kiwango fulani, bado haitoshi kutoa uchafu wote uzalishwao
hewani wakati wa kupika na kuleta hewa safi jikoni.
Ili kufanya kazi vyema mfumo wako wa uingizaji hewa
jikoni inabidi uwe unasafishwa mara kwa mara. Chujio za feni zisafishwe kila
baada ya miezi mitatu na mfumo mzima usafishwe mara moja kwa mwaka.
Karibia hood zote zina taa, kwa hivyo hii inasaidia
pia kuongeza mwanga kwenye sufuria yako wakati wa kupika na kuwezesha kuona
chakula kilicho chini ya feni. Fanya mazingira na hewa ya ndani ya jiko na nyumba yako kwa
ujumla yawe safi kwa kuweka feni ya stovu leo!
Makala
hii imeandaliwa na Vivi O. Machange. Kwa maoni niandikie barua pepe viviobed@yahoo.co.uk au kwa simu 0755200023
No comments:
Post a Comment