Wednesday, March 27, 2013

My article for newspaper: Jinsi ya kufanya zulia lidumu


Jinsi ya kuwezesha zulia lako lidumu na kuwa maridadi kila wakati

Kwa jinsi ambavyo utaweza kuweka zulia lako safi ndivyo litakavyoweza kudumu. Kwa madhumuni ya makala hii zulia litamaanisha lile la kufunika ukuta kwa ukuta na vitupio vya zulia ama vizulia ni yale mazulia madogo madogo ya kuweka maeneo yaliyoainishwa kwa mfano chini ya meza ya kahawa na kadhalika.

Sasa basi ingawa zulia safi na maridadi ni sehemu muhimu sana ya muonekano wa nyumba, kuweka jipya mara kwa mara ni gharama kubwa. Makala hii itakuonyesha ni kwa jinsi gani unaweza kufanya zulia na vizulia vyako vidumu na kuonekana vipya kwa muda mrefu.
Uchafu unafanya nyuzi za zulia lako zichakae. Safisha kwa mashine ya upepo ili kunyonya mchanga na vumbi kwenye zulia lako kila siku kwenye zile sehemu zinazokanyagwa kila wakati na walau mara moja au mbili kwa wiki kwenye zile sehemu zisizokanyagwa mara kwa mara. Asilimia 80 ya uchafu kwenye zulia ni taka kavu kwahivyo zinadakwa moja kwa moja na aina hii ya usafishaji wa zulia. Wakati wa kutumia mashine hii hakikisha unatumia brashi sahihi kuendana na unene na urefu wa manyoya ya zulia lako na pia iwe imesetiwa kwa urefu sahihi kwani kama utaipitisha juu juu tu haitakuwa inasafisha ipasavyo na kama iko chini sana inaweza kuharibu zulia kwa kung’oa manyoya. Kumbuka kusafisha mfuko wa taka wa mashine ili kuiwezesha kufanya kazi vizuri. Maeneo ya mlangoni weka vizulia vidogo vya kukanyagia kabla mtu hajaingia ndani. Utunzaji huu wa mara kwa mara utaboresha muonekano mzima na kuongeza maisha ya zulia lako .

Teua maeneo ya kulia chakula. Matone ya vyakula yanaleta mafuta kwenye zulia ambapo haya mafuta yanavuta taka nyingine na kufanya zulia lipoteze mvuto. Kwa jinsi ambavyo vyakula vinaliwa maeneo yasiyokuwa na zulia ndivyo kunavyokuwa na nafasi kubwa ya kuepuka matone matone kwenye zulia. Weka sera ya  kwamba vitafunwa vyote vitaliwa jikoni au mezani ili hata kama ni kwa watoto wadogo wakae mezani mabaki yadondoke mezani na sio juu ya zulia. Hata kama familia yako itaandamana kuhusu sera hii, bado ni njia pekee kuzuia matone yasifanye madoa kwenye zulia lako. Kama una watoto hakikisha kuwafahamisha wakujulishe mara wamwagapo kitu kwenye zulia ili usafishe mara moja. Michuzi, chokoleti na juisi ni mauaji kwenye zulia lako la thamani. Kama chakula kitapata njia ya kuelekea kwenye zulia basi hakikisha unasafisha mara hiyo hiyo. Tumia povu la shampoo ya kusafishia zulia ili kuepuka kulilowesha chepechepe na sugua kwa brashi laini kuondoa uchafu wote. Mabaki yoyote yatavuta uchafu mwingi zaidi.

Usiruhusu uchafu kuingia ndani. Weka mazingira ya nje ya nyumba na njia zote za kuingilia ndani safi. Hii itapunguza sana kiasi cha uchafu unaoweza kuingia ndani ya nyumba. Uchafu wote ubaki nje ya nyumba kwani uchafu unazeesha zulia. Ingawa unaweza kujisikia ugumu wa kuwaambia wageni wako wavue viatu kuingia ndani, kuacha viatu mlangoni kunapunguza kiasi kikubwa cha uchafu ambao ungeingia ndani. Kuvua viatu kabla ya kuingia ndani ni tabia nambari moja ambayo sio tu itapunguza ratiba za kusafisha zulia bali pia kuongeza maisha ya zulia lako. Chukua muda kuweka njia za kuingilia ndani safi.

Ni vyema kuhamisha fenicha zako kila baada ya muda fulani fulani ili kupunguza shurba kwa yale maeneo yanayokanyagwa mara kwa mara. Zulia linachakaa haraka zaidi maeneo watu wanapokanyaga kila mara. Badilisha muonekano wa vyumba ambapo utaleta njia mpya za kupitia ili kupumzisha baadhi ya maeneo kwahivyo zulia lako kuwa jipya maeneo yote na sio tu maeneo kadhaa. Weka vizuizi kwenye miguu ya fenicha hasa zile nzito  kuzuia zisiharibu zulia. Kama ukihamisha fenicha na kukuta kuwa imeweka alama kwenye zulia chukua kipande cha barafu weka juu ya hilo eneo  acha iyeyuke na polepole sugua kwa brashi laini. Kutegemea na jinsi nyumba yako ilivyo bado pengine kuna maeneo ambayo yanabakia kukanyagwa zaidi hata kama ungebadisha badilisha fenicha kiasi gani. Hivyo basi maeneo haya yanayokanyagwa zaidi tupia vizulia.
Maeneo ya zulia chini ya mlango wa kutokea nje huwa yanajenga mstari wa uchafu. Hii ni kwa ajili nje kuna uchafu mwingi wa mavumbi na udongo ambao ukinyonywa na zulia hufanya mstari huo. Ukienda kwenye maduka ya vifaa vya usafi wa majumbani utapata dawa maalumu za mazulia za kuondoa uchafu wa aina hii. Wekeza kwenye zulia nzito za kukanyagia mlangoni kuzuia uchafu wa ziada usiingie ndani.
Uji wa mishumaa hung’ang’ania sana kwenye zulia kwa hivyo epuka mshumaa unaowaka kudondosha uji wake moja kwa moja kwenye zulia.
Kuondoa uzi au nyoya lililochomoza tumia mkasi kukata badala ya kuvuta ambapo kwa kuvuta unaweza vuta zaidi ya uzi mmoja hivyo kuharibu zulia.
Maeneo ya zulia yanayopigwa na jua moja kwa moja, usiweke pazia wazi ili kuzuia kupauka au kufanya rangi ya kahawia.
Tembea kwenye zulia ukiwa umevaa soksi. Wakati kutembea bila viatu itafanya zulia lidumu, hutakiwi kutembea kwenye zulia lako miguu mitupu. Mafuta na majasho yanayotoka kwenye ngozi ya miguu yanang’ang’ania kwenye zulia na kuvuta takataka zaidi.
Pamoja na yote hayo hapo juu ya kuwezesha zulia lako liwe maridadi kila wakati na lidumu, jinsi lilivyowekwa pia inahusu. Hakikisha unatafuta wawekaji wenye ujuzi wa kuweka zulia hasa lile la ukuta kwa ukuta. Safisha zulia lako usafi wa kina wa mashine ya umeme ya mvuke ya kusafishia mazulia walau mara moja kwa mwaka. Huduma hii utaipata kwa wataalam wa usafi wa mazulia na wala huna haja ya kuwekeza kwenye mashine hii kwa kuwa utahitaji huduma yake mara moja tu kwa mwaka.
Makala hii imeandaliwa na Vivi O. Machange. Kwa maoni niandikie viviobed@yahoo.co.uk , simu 0755 200023

No comments:

Post a Comment