Thursday, April 4, 2013

My article for newspaper: Mito ya sakafuni


Tumia mito ya sakafuni kwa kukalia na kama pambo

Mto wa sakafuni ni kusheni kubwa linalotumika sakafuni kama pambo au mahala pa kukalia. Mto huu huwa umejazwa zaidi na ni mgumu kuliko mito ya kawaida ya kwenye sofa ili kuweza kuhimili uzito wa mwili. Mara nyingi mito hii ni mikubwa na hutumika kukalia wakati wa burudani kama vile wakati wa kutazama  luninga na pia ni nyongeza ya mahali pa kukalia kwenye vyumba vya michezo ya watoto.

Mto wa sakafuni unaweza kuwa na umbo lolote liwe ni duara, boksi ama mraba. Weka mito yako mitatu juu ya kizulia chako cha kutupia na mara utagundua kuwa umetengeneza sehemu ya nyongeza ya kukalia wakati wa burudani au mahali poa pa kusoma na kustarehe. Chagua mito ambayo itaendana na kizulia chako. Mpangilio wa kizulia hicho na mito yenye rangi za kukolea utaleta mvuto. Pia unaweza kupendezesha sakafu yako ya marumaru au mbao kwa kutupia mito ya sakafuni. Chagua rangi za ladha yako kuendana na rangi ya sakafu ili kuleta muonekano wa mapambo ya kisasa.

Mito ya sakafuni ni pambo rahisi ambalo kila nyumba inaweza kuwa nalo. Kama wazo lako la mito ni kuweka kwenye sofa  tu; basi unahitaji kuchukua muonekano mwingine. Mito hii inakuja kwa saizi mbalimbali kwa jinsi ambayo inaweza kumfurahisha kila mtumiaji awe ni mtoto, kijana ama mtu mzima. Unakutana na matumizi mengi ya mito mikubwa ya sakafuni na utashangaa ni kwa vipi unaweza kuishi bila hiyo. Hata kwa kukaa tu na kutulia kutafakari maisha au kucheza karata karibu na meza ya kahawa, mito ya sakafuni inafanya kukaa sakafuni kuwa ni raha na shughuli zako kuwa za starehe zaidi

Watoto wanaipenda! Ni muhimu wakati wa kucheza na watoto. Ukiwa unakaa karibu na watoto mara kwa mara utaanza kugundua ni muda mwingi kiasi gani wanaoutumia sakafuni.  Na pia ni muda mwingi kiasi gani wanapenda ukae nao hapo sakafuni! Kama una mtoto mdogo utakugundua kuwa mto mkubwa wa sakafuni ni sehemu tosha kwa usingizi kwa mchana.
Pia kwa swala la usalama, watoto wadogo hawako makini kihivyo; na hasa wanapokuwa wanakimbia na kuishia kujirusha kwenye sofa. Ndio hapo wapohitaji mto mkubwa wa sakafuni kuangukia. Na hata wanapong’ang’ania kubembea kwenye mikono yako hadi unaposikia kama mikono inataka kung’oka, basi sehemu ya kuwatulizia ni kwenye mito ya sakafuni.
Kwa kuhurumia magoti yako idadi ya mito inavyoongezeka ndio na uzuri wake unavyoongezeka. 

Kwa nini ukae tu juu ya kizulia uumizwe na sakafu wakati kuna mto mkubwa wa kunesa ambao ungeweza kuukalia? Wakati familia yako ikiendelea kukua na sehemu ya kuweka fenicha imeshajaa, mito mikubwa ya sakafuni ni mbadala tosha wa viti. Kwa mikutano ya familia na marafiki wakati ambapo hamna viti vya kutosha hufurahii wale wanaoshia kukaa sakafuni wapate starehe (hata kama ni watoto?)

Mito ya sakafuni inayokunjika ni chaguo zuri. Hii ina sehemu tatu, kunjua wote kama unataka kulala kwa tumbo; halafu kama unataka kukaa kwa muda; ukunje zile sehemu mbili ili usaidie mgongo na sehemu ya tatu kalia. Mito ya aina hii pia ipo ya kufanana kama fenicha kabisa ambayo ina hadi sehemu za kupumzisha mikono.

Je una kimnuso cha binti yako mdogo nyumbani? Ni nini kinachoweza kuwa rahisi zaidi ya kuweka nusu dazeni ya mito hii kwenye sakafu ya sebule yako. Wacha waangalie katuni hadi wasinzie halafu waache hapo, ukijua kuwa wana kitanda na mto pamoja! Kwa hivyo kama isivyo kwa mapambo mengine ya ndani, mito ya sakafuni inawekwa kwenye matumizi ya kukalia na mapambo kwa wakati mmoja.

Mito ya sakafuni inaweza kuwa kwenye kitambaa chochote utakacho hadi kwenye ngozi na hata plastiki kwa ajili ya ile ya kwenye varanda. Baadhi ya watu wanapenda kuoda mito ili watengenezewe kuendana na mapambo yao mengine ya ndani au hata mapambo ya chumba husika. Ingawa hii inaweza kuwa gharama zaidi lakini inakuwezesha kupata foronya za rangi upendayo na utakazoweza kubadilisha kadri upendavyo.
Kama unataka kuburudisha nje ya nyumba kwenye varanda yako tafuta mito ya sakafuni ya nje. Mito hii ya sakafuni ya kwenye varanda inatengenezwa kwa foronya za kudumu kwa mfano za kanvasi, ngozi ama plastiki, ili kujikinga na unyevu maji na hata kuzuia kupauka kirahisi. Wakati usioihitaji ihifadhi stoo ili kuiwezesha idumu.

Mito ya sakafuni inatumika kama pambo na mahali pa kukaa pale ambapo urefu wa kiti ama usaidizi wa kina wa mgongo hauhitajiki. Kama unavyoweza kuona, jinsi ambavyo mto wa sakafuni unavyoweza kutumika kama pambo au kama fenicha nyumbani kwako ubunifu tu ndio unahitajika. Wageni wako watu wazima wanaweza kuunganisha mito ya sakafuni kadhaa wakavuta shuka na tayari kuwa kitanda bandia  cha mgeni Kwa hivyo unasubiri nini kuwa na mito ya sakafuni?

Makala hii imeandaliwa na Vivi O. Machange. Vivi anajishughulisha na usafi wa mazulia na nguo aina zote; pia ana mapenzi makubwa ya mitindo na mapambo ya nyumbani. Kwa maoni au maswali tuma kwenda viviobed@yahoo.co.uk au 0755 200023

No comments:

Post a Comment