Thursday, April 11, 2013

My article for newspaper: Ukuta wa nje ya nyumba


Jinsi ya kupamba ukuta wa nje ya nyumba  yako

Kupamba ukuta wa nje ya nyumba kunahitaji mpango ulioandaliwa. Unatakiwa uangalie vitu kama hali ya hewa, sanaa za mapambo na rangi ya ukuta. Muunganiko wowote wa rangi, mimea na  sanaa za ukutani vinaweza kutumika kama nyenzo za kutengeneza ladha yako binafsi kwenye ukuta wa nje wa nyumba. Kumbuka kama nyumba ni ya kupanga hakikisha unapata baraka za mwenye nyumba!

Moja ya njia rahisi zaidi za kuhuisha au kubadili muonekano wa kuta za nje ni kupaka rangi.  Kabla fundi rangi hajaanza kazi yake hakikisha marekebisho yote yanayohitajika kwenye ukuta yamefanyika kwanza, kwa mfano kuziba nyufa na kadhalika. Kwa ujumla maandalizi ya ukuta kabla ya kupaka rangi sio kitu rahisi sana kwa hivyo hakikisha unapangilia vyema ili kupata matokeo unayohitaji. Kama kuta hizo hazijawahi kupakwa rangi hakikisha unafikiria kwa makini juu ya nini unachotaka kama umeamua kuzipaka rangi.

Paka rangi ambayo ni maalumu kwa kuta za nje na shirikisha wataalamu wa mambo ya rangi, uchanganyaji  na upakaji wake. Hii ni muhimu kwani rangi za kuta za nje ya nyumba ni tofauti na zile za kuta za ndani kwani hizi za kuta za nje zina uwezo wa kupambana na hali ya hewa ya nje, wadudu kama fangasi na pia zinasafishika kirahisi kwa maji. Mara kuta zako zinapokuwa zimepakwa rangi zingatia kuzitunza kwa kuwa mradi wa kupaka rangi ni mkubwa kwahivyo sio kazi ungependa kufanya kila baada ya miezi kadhaa.

Mifereji ya maji ya mvua ijulikanayo kama gata nayo isisahaulike kupakwa rangi. Iwe gata ni za chuma au plastiki kuna rangi zake mahsusi kwa nje na ndani hasa ukizingatia kuwa ndani inakuwa inaloa maji kila mvua zinaponyesha. Maeneo ambayo yana chuma kwenye mifereji hii nayo yanaandaliwa kitaalamu kuzuia kutu kama nilivyosema awali kuwa hakikisha unafanya kazi ya kupaka rangi na wataalamu.

Kuta zilizopo karibia na majani, otesha vichaka vya maua na miti  katika uwiano utakaoleta rangi nzuri ya muonekano wa maua ya asili. Kama ni muhimu unaweza pia kuotesha maua kwenye vyungu vidogo vya maua vya kuninginiza ukutani.

Kuna nyenzo nyingi zilizopo za kuweza kuweka urembo ukuta wa nje ambazo ni pamoja na mbao, tofali, marumaru au mawe kama yale ya Tanga. Tumia nyenzo hizi kwa ukuta mzima au kwa maeneo ya chini tu. Kona ambazo hazina kitu zinaweza kupendezeshwa kwa urembo wa mawe au chuma.
Mapambo mengi ya sanaa kwenye nyumba mara nyingi yanawekwa sebuleni au zile sehemu ambazo burudani inafanyika.  Lakini wakati  kuta za ndani zinaweza kuwa za kupendeza kwa sanaa za aina mbalimbali, watu wengi wanaweka juhudi kidogo kupamba kuta  za nje ya nyumba  wakati kiukweli ndizo wageni wanazoona kwanza.

Kupamba kuta za nje kutafanya hata  zile za ndani yavutie zaidi. Kupamba ukuta wa varanda kwa mfano, kwa sanaa nzuri za kuta za nje itasaidia kusisitiza uzuri wa mazingira ya eneo hilo.  Kuna aina nyingi za kuchagua ambazo zitaendana na jengo na pia ladha ya mwenye nyumba.  Vinyago vya ukutani pia vinaweza kuongeza staili kwenye ukuta wa nje uliokaa bila pambo. Na mapambo haya hayatakiwi kuwa ghali, kwa mpango mzuri na umakini hata ile sanaa ya bei rahisi kabisa inaweza kuleta mvuto wa ajabu. Kinachotakiwa tu ni kuchagua mandhari fulani na chagua sanaa sahihi za kuendana na mandhari uliyochagua.
Fremu kubwa kwa mfano inasaidia kuleta mvuto maalumu kwenye ukuta mtupu. Chagua fremu kubwa za picha za kanvasi zenye mandhari uliyochagua kupamba ukuta wako wa nje ya nyumba. Sanaa chache tu zilizowekwa kimkakati kwenye ukuta wa nje zitaleta tofauti kubwa.

Mapambo ya ukuta wa nje yanapendezesha nyumba yako kama vile ya ukuta wa ndani. Njia mojawapo ya kupata sanaa za kupamba ukuta wa nje ya nyumba ni kupiga picha makazi yako na kujitengenezea picha kubwa za fremu. Fremu hizo  pambia  kwenye kuta za  maeneo ya varanda, bwawa la kuogelea na hata zile  za bustani. Zingatia ubora wa sanaa ambao utaweza kupambana na kupauka kutokana na jua na pia unyevu na kubanduka rangi.
Makala kama hii, katalogi na mtandao vinakuwezesha kupata mawazo ya mapambo ya ukuta wa nje. Mara nyingine mapambo haya kama picha za fremu za kanvasi zinaweza kuwa ghali lakini hutajutia hela yako kama ni tamanio la moyo wako kwani mapambo haya yatakufanya kujisikia raha na kuridhika na jinsi ambayo mahali unapoishi panavyoonekana.
 
Makala hii imeandaliwa na Vivi O. Machange. Vivi anajishughulisha na usafi wa mazulia na nguo aina zote; pia ana mapenzi makubwa ya mitindo na mapambo ya nyumbani. Kwa maoni au maswali tuma kwenda viviobed@yahoo.co.uk au 0755 200023

No comments:

Post a Comment