Thursday, November 7, 2013

My artice for newspaper: Uanzishaji na utunzaji wa bustani




Utaijua bustani yenye afya wakati unapoiona: laini, kama vile ni zulia la kijani limetandikwa chini, ukitembea humo hamna majani makavu yanayojaa miguuni kukufanya uchafuke miguu na viatu vyako. Sasa, kwa nini bustani yako haionekani hivyo? Kupata muonekano maridhawa wa bustani huenda ikatakiwa ubadili fikra zako, anasema mtaalamu na mbunifu wa bustani Hadija Adam. “Unajua jinsi wanavyosema utamu wa ngoma uingie ucheze? Vyema, unatakiwa ugeuke ukoka. Unatakiwa ufikiri ni nini ukoka unahitaji,” anasema Hadija. 
Vitu vya msingi anasema ni vya kawaida sana: jua, maji na mbolea. Ukishapata hivyo hapo ni furaha tu - kwako na kwa bustani yako.

Kuanzisha bustani mpya ni mchakato wa raha na changamoto pamoja. Inabidi maandalizi na mipango. Unatakiwa kuandaa eneo kwa kuondoa magugu yote na kujaza udongo kama itahitajika. Sasa hapa nikisema kujaza udongo kumbuka sio kila udongo unafaa. Bi Adam anasema hatua ya muhimu sana ambayo watu wengi wanaruka ni hii ya kujaza udongo. Ni muhimu sana kuweka udongo unaofaa na mbolea ya ng’ombe (sio ya kuku kwa kuwa ina tindikali kali kwa hivyo haifai kwa kuoteshea ukoka). Bi Hadija anashauri kama kiasi cha udongo ni robo tatu basi mbolea iwe robo. Katika kuchanganya na kusawazisha kwa kureki usilazimishe sana tambarare fuatilia ardhi ilivyo na mwelekeo wa maji ili usijesababisha kuweka dimbwi kwenye bustani yako wakati wa masika. Kuwa makini sana kwa kuwa ukishaotesha ukoka wako hutarudi nyuma tena na kuanza kung’oa kwa ajili ya makosa yaliyofanyika mwanzo.

Kuna aina nyingi za ukoka (majani) unazoweza kuotesha kwenye bustani yako. Nyingine ni laini na nyembamba sana (fikiria uwanja wa golfu na wa mpira wa miguu), wakati ukoka nyingine unaweza dhania umekanyaga nyasi kavu miguuni. Majani ni mengi na yanagundulika kila mwaka. Kwa majani haya yote hali ya hewa inachangia unawiri wake.

Hakuna swali ya kuwa kuweza kupata zulia zuri la ukoka lililofunga kila mahali kwa wakati mmoja ni kwa kuotesha mbegu kila mahali wakati wa mwanzo. Lakini hii inaweza kuwa gharama hasa kama unataka kufunga eneo kubwa. Badala yake unaweza kununua mbegu chache ukaotesha kitaku nawe ukaanza kujipatia mbegu zako kwenye kitalu hicho. Kumbuka hii ni kama kununua mbegu za kuweza kutosha eneo lako ni gharama sana. Kwa mfano, tukichukulia huu ukoka unaoitwa Canadian; mbegu za kujaa mfuko mmoja wa saruji zinauzwa kati ya elfu 30-40. Sasa kama eneo lako utahitaji mbegu mifuko hamsini kwa mfano, inaweza kuwa ni gharama kubwa kwako. Kwa hivyo nunua mifuko michache uoteshe kitalu uvune mbegu mwenyewe.

Sasa ukoka wako umeshaota na umeshafunga kila mahali na umerefuka kiasi ya kuwa unahitaji kuukatia. Inapokuja kwenye swala la kukata ukoka wa bustani wenye nyumba wengi wanashindwa kujua urefu sahihi. “Watu wengi wanakata ukoka wao kwa kuuacha mfupi sana, kitu ambacho kinayasababishia majani msongo,” anasema Bi Hadija. Anashauri usetie mashine  ya kukatia kwenye alama ya juu kabisa. Majani yakibaki marefu yanafanya mizizi ikue vizuri na pia inasaidia ardi isichomwe na jua la moja kwa moja na kuwa kavu kwani utaingia gharama ya kuongeza umwagiliaji. Na usiamini kuwa ukiacha majani yawe marefu ina maanisha kuyakata mara kwa mara kila baada ya muda mfupi, anasema Hadija. “Lakini hii ni uongo kabisa "kuna upotofu kwa watu wengi kuwa kama wakiyakata yakawa mafupi hautakata mara kwa mara, huu ni uongo; yanaota haraka mno kiasi kwamba hayakupunguzii muda wowote wa kukata tena.

Maji, maji, maji kila mahali. “Maji mara mbili kwa wiki ila maji mengi” kwa Hadija hii ndio kanuni ya msingi. Maji ya kuzama yanasaidia mizizi kupenya kina kirefu ardhini, wakati  maji kidogo kidogo kila siku yanasababisha vishina kukauka na kuzalisha majani makavu (ambayo ndio yanachafua miguu). Kumwagilia kwa kina pia kunafukuza wadudu wanaojishika kwenye majani. Kwa bustani mpya iliyooteshwa ukoka mwagilia maji mengi kila siku hadi mizizi ishike.

Bustani, hata ile unayoiona ina afya inahitaji chakula imara na hewa. Mara mbili au tatu kwa mwaka wakati wa masika wataalam wanashauri ndio wakati wa kuiwekea bustani mbolea. Kwa wakati huu mbolea ya kuku ndio inafaa zaidi hasa kuweza kutunza ule ukijani wa ukoka unaohitaji.

Magugu kwaheri, sio ajabu kuwa karibia kila bustani itakuwa na magugu. Njia nzuri ya kuangamiza magugu kwenye bustani ni kuchagua ukoka unaofunga kiasi kwamba utayazuia magugu kushamiri. Yale machache yatakayopenya dawa yake ni kuyang’oa.

Zingatia kanuni hizi za uanzishwaji na utunzaji wa bustani na kila mmoja atakuwa na furaha -- wewe na bustani yako.
Makala hii imeandaliwa na Vivi O. Machange. Vivi ni mjasiriamali upande wa usafi wa mazulia, nguo na magari; pia ana mapenzi makubwa ya mitindo na mapambo ya nyumbani. Kwa maoni au maswali tuma kwenda 0755 200023 au viviobed@yahoo.co.uk



No comments:

Post a Comment